VIONGOZI WA NGAZI ZA JUU CHADEMA WASHITAKIWA KIGOMA...

Baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema. Kutoka kushoto ni John Mnyika, Dk Willibrod Slaa na Freeman Mbowe.
Wakati Chadema, ikitafuta hoja ya kukirudisha katika siasa zinazogusa watu katikati ya mgogoro wa uongozi unaoendelea, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Shaban Mambo ameamua kushitaki uongozi wa chama hicho kwa wananchi wa Kigoma.

Mbali na kushitaki uongozi huo, pia waasisi wake wameanza kukosolewa kwa kukosa busara katika mgogoro unaoendelea, huku baadhi ya vikao vikitumika kukosoa misimamo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Juzi Mambo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi ya Chama hicho, alihudhuria mkutano maalumu wa Chadema wa Wilaya ya Kigoma Mjini, ambako alitoa tamko la kutaka wajumbe wa Baraza Kuu kusimamia mustakabali wa chama hicho.
Mambo katika mkutano huo alisema kwa sasa uamuzi muhimu kwa wanachama na mustakabali wa chama, umekuwa ukifanywa na kikundi cha watu wachache hasa Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilibrod Slaa.
Alisema uamuzi wa kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na kufukuza uanachama viongozi wengine wawili, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, ulifanywa kwa jazba bila kuzingatia hali halisi ya tuhuma zinazowakabili.
Sababu kubwa ya adhabu kwa viongozi hao kwa mujibu wa Mambo, ni msimamo wao kuhusu demokrasia ndani ya chama, kupishana viongozi hao wawili wakuu wa chama.
Alitaka wajumbe wa Baraza Kuu, ambalo linasubiriwa kuamua hatma ya Zitto, kusimamia haki na mustakabali wa chama badala ya kukubali kuburutwa na uamuzi wa wachache kama ambavyo imetokea kwenye kikao cha Kamati Kuu.
“Chama kisimamie haki na ukweli badala ya watu kuchukua uamuzi kwa sababu ya chuki zao binafsi, nitasimama hadi dakika ya mwisho kupinga uamuzi unaofanywa na chama ambao hauzingatii tuhuma wanazokabiliwa wanachama wanaoadhibiwa,” alisema Mambo.
Mambo pia alizungumzia kitendo cha kupigwa na kutishiwa kuuawa kwenye kikao  cha Kamati Kuu huku viongozi wakuu wa chama wakiangalia bila kuchukua hatua zozote.
Baada ya kauli ya Mambo, Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Kigoma, Mwalimu Adam Shaban, alisoma tamko la wajumbe wa kikao hicho ambao walilaani vurugu na kupigwa kwa Mambo mbele ya viongozi wa kitaifa wa chama ambao walishuhudia bila kuchukua hatua.
Sambamba na hilo wajumbe hao wa mkutano mkuu wa wilaya walitaka uongozi wa Chadema makao makuu kutoa taarifa ya kina kuhusu tukio hilo na kuhakikisha usalama wa viongozi wao unadhibitiwa katika vikao vijavyo.
Pia walitaka uongozi wa Chadema kuandikia waraka unaoelekeza kutomtambua Zitto kama mbunge na kwamba bila waraka huo, hawatatambua maagizo hayo kupitia magazetini.
Adam alisema kuwa wataendelea kumpokea na kumheshimu Zitto kama mbunge wao hadi hapo watakapopata maelekezo rasmi ya kufanya hivyo na si kusikia kwa mdomo.
Wakati Kigoma wakiazimia kuendelea kumpokea Zitto kama mbunge wao kinyume na katazo la Dk Slaa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Peter Maina, juzi alinukuliwa akipingana na msimamo wa muasisi wa Chadema, Edwin Mtei kuhusu mgogoro huo.
Mtei alinukuliwa akimtaka Zitto kutafuta chama kingine na kwamba kwa sasa hana namna kwa kuwa hakubaliki tena ndani ya Chadema.
Lakini Profesa Maina mbali na kukosoa uongozi kwa kuchukua hatua bila kutumia busara, alisema msimamo wa Mtei unaiumiza zaidi Chadema kwa kuwa hauoneshi kuwepo kwa demokrasia ndani ya chama.
“Kauli ya Mtei inazidi kuonesha nia ovu waliyonayo baadhi ya watu ndani ya Chadema, kusema Zitto akatafute chama si maneno ya kuonesha ukomavu wa kidemokrasia, niseme kuwa Mtei anakiumiza zaidi chama … huu si wakati wa kulumbana ni wakati wa kutafuta suluhu,” alinukuliwa Profesa Maina akisema.
Wakati huo huo, chama hicho kimeanzisha harakati za kujikita katika siasa zinazogusa watu, ikiwemo hatua ya hivi karibuni kupinga nyongeza ya bei ya umeme na kushinikiza Serikali kuboresha huduma za maji kwa wananchi.
Hata hivyo, katika kikao cha Chadema kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Kilimanjaro, inadaiwa baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na Azimio la Arusha.
Katika mkutano huo ambao inadaiwa Mbowe na Dk Slaa walikuwapo, inadaiwa hali ngumu ya uchumi nchini, inatokana na kosa lililofanyika mwaka 1961, kwa kukubali uhuru wa bendera, badala ya uhuru wa uchumi.
Mbali na kuita uhuru wa 1961 kuwa wa bendera, ambao harakati zake ziliongozwa na Mwalimu Nyerere, pia ilidaiwa katika kikao hicho kwamba Tanzania chini ya TANU, ilifanya kosa kuanzisha siasa za Azimio la Arusha.
Siasa hizo zilidaiwa katika kikao hicho kwamba ziliharibu uchumi na kufanya maisha ya watu nchini kuendelea kuwa magumu mpaka leo.

No comments: