VIJIJI VYOTE LINAKOPITA BOMBA LA GESI KUPATIWA UMEME...

Moja ya vijiji lilikopita bomba la gesi.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema njia pekee ya kuondokana na hujuma dhidi ya bomba la gesi linalosafirisha gesi Mtwara - Dar es Salaam ni kuviwekea umeme vijiji vyote bomba hilo linamopita.

Hivyo ameigiza Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya miradi ya umeme katika maeneo hayo ili wananchi wajione ni sehemu ya mradi huo badala ya kuona bomba la gesi linapita bila kuwa na manufaa nalo.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alifafanua kuwa wanavijiji hao hawatawekewa umeme bure majumbani, bali watalipia gharama za uunganishaji kama ilivyo kwa Watanzania wengine vijijini.
Alisema huduma ya uwekaji umeme nyumbani Lindi na Mtwara kwa sasa ni Sh 99,000 na mwisho wa bei hiyo ni Juni na baada ya hapo watalazimika kulipia bei mpya iliyotangazwa na Tanesco hivi karibuni.
“Baada ya Juni watalipia kama Watanzania wengine wanavyolipia Sh 177,000 kwa umeme kwenye nyumba kama ilivyo kwa maeneo mengine vijijini, hawawezi kuwekewa umeme bure, tukifanya hivyo kila kona ya Tanzania kuliko na viwanda vya umeme watadai wawekewe bure,” alisema Muhongo.
Waziri alilazimika kutoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari ili kuondoa dhana, kwamba wanavijiji hao ambako bomba la gesi linapita watapewa umeme bure.
Awali, Pinda alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ndio wenye mradi huo wa bomba la gesi hivyo wanatakiwa kubeba jukumu  la kuhakikisha angalau kila mwaka zinatengwa Sh bilioni 2 kwa ajili ya kuvipa umeme vijiji ambamo bomba la gesi linapita.
“Tukifanya hivyo hawa watakuwa walinzi wazuri wa bomba hili na kama atatokea mtu anataka kufanya hujuma ni wazi kuwa watatoa ushirikiano kwa Serikali,” alisema Pinda na kumwagiza Waziri Muhongo kushughulikia suala hilo.
Bomba hilo linapita katika baadhi ya vijiji vya Mtwara, Lindi, Pwani katika wilaya za Rufiji, Mkuranga na hatimaye Dar es Salaam. Ujenzi wake unafanywa na kampuni ya maendeleo ya mafuta ya China (CNPC).
Pinda ambaye alikuwa na ziara ya siku mbili kukagua ujenzi wa bomba hilo, alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha Lindi, Mtwara na Ruvuma zinapewa nishati ya uhakika ya umeme na miongoni mwa miradi hiyo itatokana na bomba hilo.
Profesa Muhongo alisema kwa kuanzia, wizara imetenga Sh bilioni 20 ili kuvipatia baadhi ya vijiji umeme ambako bomba hilo linapita na kuongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinavyopitiwa na bomba hilo vinapewa umeme.
Profesa Muhongo alisema kutokana na uchumi wa gesi kuanza, ni wazi viwanda vingi vitajengwa Lindi lakini pia akawahakikishia wananchi kuwa mpango wa Serikali ni kuona wananchi wanawekewa mabomba ya gesi majumbani.
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha miradi yote inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini inakamilika Juni mwakani na kiasi cha Sh bilioni 881 zimetengwa kwa ajili hiyo.
“Watu wa Lindi na Mtwara hatujawasahau, gesi ipo ya kutosha hapa kwenu na ili kuhakikisha mnaingiza umeme katika nyumba nyingi tumewapunguzia gharama za kuunganisha hadi Sh 177,000,” alisema na kuwataka wananchi hao kuhakikisha wanajenga nyumba bora ambazo zinaweza kuwekwa   umeme.
Kuhusu gesi majumbani, Profesa Muhongo alisema Lindi itaanza na Songosongo na akawahakikishia wasiogope kwani ulipaji wake ni mdogo kuliko kununua gunia la mkaa.
 “Watu ambao tumewaunganishia wanalipa Sh 15,000 kwa mwezi wakati gunia la mkaa ni kati ya Sh 40,000 na Sh 50,000, hivyo gesi hii ni  rahisi kuimudu,” alisema Waziri na kuongeza kuwa watajenga viwanda ambavyo vitasindika gesi kwenye mitungi ili wananchi wengi wafaidike na gesi ya Mtwara.

No comments: