MIMBA ZA WANAFUNZI ZAMTIA MATATANI OFISA MBEYA...

Serikali mkoani Mbeya imetoa muda wa siku saba kwa ofisa mtendaji wa kata ya Nanyala, Theofrida Hankungwe kuhakikisha amewasilisha taarifa zilizochukuliwa kwa wanafunzi watano waliopata mimba mwaka jana katika shule ya sekondari ya Shikula.

Agizo hilo pia linamkabili  Mkuu wa shule hiyo ya sekondari, Chonge Dafa ambapo kwa pamoja viongozi hao wanapaswa kueleza ni hatua zipi zilichukuliwa kwa wanafunzi waliopata mimba na pia waliosababisha mimba hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alitoa agizo hilo alipotembelea shule hiyo na mkuu wa shule kumweleza kuwa mimba ni moja ya changamoto zinazoikabili shule yake.
Alisema katika mwaka 2013 wanafunzi watano walipata mimba akiwemo mmoja aliyepewa na mwanafunzi mwenzake ambapo wote walifukuzwa shule.
Kutokana na taarifa hiyo, Kandoro alitaka kusikia hatua zilizochukuliwa kwa waliopata na waliosababisha mimba na hapo ndipo ofisa mtendaji na mkuu wa shule walipoanza kurushiana mpira huku ofisa mtendaji akisema hana taarifa na mkuu wa shule akisema taarifa zote aliziwasilisha katika uongozi wa kata.
Malumbano hayo yalimfanya Kandoro kuwaagiza kutoa taarifa ya hatua walizowachukulia wahusika wa mimba hizo ndani ya siku saba na kuziwasilisha ofisini kwake mara moja.
Alisema kumekuwa na mchezo wa baadhi ya wazazi kumaliza kesi za mimba kiundugu kwa kupeana pesa au mali nyingine badala ya kupeleka kesi hizo mahali husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

No comments: