TICTS YAKATAA MALIPO YA HUDUMA KWA SHILINGI KUANZIA JUMATATU IJAYO...

Huduma ya makontena bandarini Dar es Salaam inayofanywa na kampuni ya TICTS.
Kampuni ya Kuhudumia Kontena Bandarini (TICTS), imepiga marufuku wateja wake kulipa kwa Shilingi kuanzia Jumatatu na kutaka walipe kwa dola ya Marekani.

Aidha, imeagiza wateja hao kufanya malipo hayo kupitia tawi la benki moja pekee katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Tunawaarifu wateja wetu, kuwa kuanzia Januari 27, hati zote za malipo za TICTS, zitalipwa kwa dola za Marekani tu. Wateja wanaombwa kuendelea kulipa kupitia benki ya Standard Chartered, tawi la International House, akaunti namba 87-060-212922-01,” lilieleza tangazo la kampuni hiyo kwa wateja wake.
Kutokana na hatua hiyo, wateja wa huduma za bandari wameitaka Serikali kuingilia kati kwani inaweza kusababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi na kuongeza gharama za bandarini na hatimaye za maisha kwa wananchi wa kawaida.
Wadau hao-Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa Shehena Tanzania (TAFFA), Chama cha Wasafirishaji wa Mafuta Tanzania (Tatoa), Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania (TASAA) na Chama cha Bandari ya Nchi Kavu (CIDAT)-wameteua mwakilishi, Stephen Ngatunga kushughulikia hali hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wateja hao, Ngatunga ambaye ni Rais wa TAFFA, alisoma tamko la wadau hao, linataka mamlaka husika kuingilia kati ili pamoja na mambo mengine, wapate maelezo ya kampuni hiyo imepata wapi kibali cha kufanya uamuzi huo.
Tamko hilo lilisainiwa na Ngatunga, Makamu wa Rais wa CIDAT, Lucas Nengesti, Katibu Mtendaji wa TASAA, Elitunu Mallamia na Mkurugenzi wa Tatoa, Elias Lukumay.
“Haiwezekani kampuni zote zifanye malipo kwa dola, tunaagiza  wanachama wetu kuendelea kufanya malipo kwa Shilingi na si dola mpaka tutakapopata majibu kutoka mamlaka husika,” alisema Ngatunga wakati akisoma tamko hilo.
Pia alisema wameandika barua kwenda kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  na Waziri wa Fedha, ili kupata ufafanuzi wa uhalali wa malipo hayo.
Alisema wiki iliyopita walikutana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na kutoa malalamiko yao kuhusu gharama kubwa wanazotozwa na TICTS katika kubadilisha fedha.
Kwa mujibu wa Ngatunga, gharama za huduma za TICTS ziko kwa dola na wateja wanapolipia, hutakiwa kulipa kwa kutumia kiwango cha kubadilisha fedha za kampuni hiyo, ambacho kwa dola huwa juu kuliko kiwango cha kubadilisha fedha kinachotangazwa kila siku na BoT.
“Badala ya kushughulikia tatizo hilo ili kukuza thamani ya fedha yetu, tunashangaa wameamua kukataa kabisa Shilingi bila kushirikisha wadau na hata Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), haikushirikishwa,” alisema Ngatunga.
Makamu wa Rais wa CIDAT, Nengesti alisema haiwezekani mwekezaji afanye utaratibu kinyume na sheria za Tanzania ni vema kuangalia upya.
Makamu Rais wa TAFFA, Urio alisema ni lazima kuonesha uzalendo kwa Taifa kwa kulinda na kuheshimu sarafu kwa nia ya kulinda uchumi wa nchi, huku wakijiuliza mamlaka hayo wanapewa na nani na kwa vigezo gani.
Tangazo hilo la TICTS, na hata upangaji wake wa viwango vya kubadilisha fedha, ni kinyume na tamko la Serikali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni, lililotolewa Agosti 27, 2008 bungeni.
Tamko hilo lilinukuu Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 26 kinachoeleza kuwa Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo hakuna mtu au kampuni yoyote nchini inayoruhusiwa kuikataa kwa malipo yoyote.
“Vifungu vya sheria nilivyonukuu hapa vinajumuisha mambo ya msingi yafuatayo: Kwanza hakuna kipingamizi chochote cha sheria dhidi ya  wananchi kumiliki fedha za kigeni, iwe ni taslimu au  akaunti katika benki.
“Pili Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo haiwezi  kukataliwa kwa malipo nchini. Kwa hiyo, ni kosa kwa mtu kukataa malipo kwa fedha ya Tanzania au kumlazimisha mtu kufanya malipo kwa fedha tofauti na Shilingi ya Tanzania,” lilieleza tamko hilo.
Hata hivyo, ilifafanuliwa kuwa kutangaza bei za bidhaa za Tanzania katika fedha za  kigeni, hakukatazwi na sheria yoyote ya Tanzania na lengo ni kusaidia wazalishaji kupata masoko ya mazao nje ya nchi au kwa wageni, ili wanunuzi wa bidhaa hizo waelewe kirahisi bei za bidhaa au huduma hizo.
Tamko hilo lilieleza: “Viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka bei katika sarafu mbili iwekwe wazi na isizidi ya soko. 
“Ifahamike wazi kuwa ni benki na maduka ya fedha za kigeni tu,  yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na  ushindani katika soko la fedha za kigeni.”

No comments: