SUMATRA YAZINDUA UTARATIBU MPYA WA RATIBA NA VIBAO MAALUM KWA MABASI...

Baadhi ya mabasi yafanyayo safari zake kati ya Dar na Kilimanjaro.
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imezindua utaratibu mpya wa ratiba  na vibao maalumu, vitakavyotumiwa na mabasi yanayotoa huduma ya usafiri kati ya Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra),  Ahmadi Kilima, alisema lengo ni kuboresha huduma kwa abiria.
Kilima alisema baadhi ya  wasafirishaji walikuwa wakihodhi ratiba, ambazo uhalali wake ni wa kutilia mashaka na vibali pia vilikuwa vinatumika bila kuzingatia kanuni za matumizi yake.
Alisema pamoja na kuwepo mabadiliko katika  ratiba, pia mamlaka iliona ipo haja ya kuboresha zaidi mfumo wa matumizi ya ratiba za mabasi kwa kuweka utaratibu kuwa kuanzia sasa kutatolewa vibao kulingana na gari husika.
Kilima alisema utaratibu wa vibao unaonesha namba ya huduma kwa basi la kawaida, vibao vitakavyotumika ni vyeupe ambavyo vina jina la kampuni ya mtoa huduma, na muda wa basi kuondoka.
Alisema kwa basi la daraja la kati vibao vyake vina rangi ya bluu na nyekundu na vya   daraja la kwanza, ni vya rangi nyekundu.
Kilima alisema mabadiliko hayo yatasaidia wasafiri kutambua basi la daraja husika kwa wepesi ili aweze kulipa nauli stahili, pamoja na kudhibiti matumizi ya muda kama ilivyoandikwa kwenye ratiba kwa lengo la kupunguza ajali.
Akizindua mabadiliko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alitaka jeshi la polisi kwa kushirikiana na Sumatra kufanya kazi kwa  kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji, kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wasafiri.

No comments: