SERIKALI YAWAPOZA WAFANYABIASHARA, SASA KUSHUGHULIKIA MASHINE ZA EFDs...

Serikali imewapoza wafanyabiashara wanaopinga matumizi ya Mashine za Kielektroniki ya Kukusanya Kodi (EFDs), na kuwaahidi kufanyia kazi ushauri wao.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, alisema jana mbele ya wafanyabiashara hao, kwamba Serikali imepokea ushauri wao kwa uzito mkubwa na itaufanyia kazi na kutoa mrejesho katika vikao vitakavyofuata.
Dk Kigoda alisema ili kumaliza matatizo yao, kunahitajika ujasiri na uvumilivu mkubwa kwa kufuata hali halisi ilivyo na kuwahadharisha wasipotoshwe na wanasiasa kwani matatizo ya uchumi humalizwa kwa mfumo wa uchumi.
“Angalieni kiuchumi linawaathiri kwa kiwango gani…wanasiasa wasijeingilia kwani wao kazi yao ni kutafuta umaarufu kwa watu,” alisema Dk Kigoda na kuongeza, kuwa mikutano kati ya Serikali na wafanyabiashara kama huo, itamaliza kutoaminiana baina yao.
Alisema yeye ni daraja na yote yaliyosemwa na wafanyabiashara hao ameyasikia na yatafanyiwa kazi kwa kuwa sera ya Serikali  ni kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini.
Wafanyabiashara hao wameendelea kupinga matumizi ya mashine hizo, wakidai kuwa zina upungufu ukiwamo wa kutunza kumbukumbu za mauzo pekee.
Wanadai mashine hizo hazina uwezo wa kutunza kumbukumbu ya ununuzi, matumizi, hasara na hata mikopo ambayo mfanyabiashara amekopa kutoka taasisi za fedha.
Walisisitiza kulipa kodi, lakini wakiomba mfumo wa ulipaji ubadilishwe huku wakitoa ujumbe kuwa ‘kodi bila mashine inawezekana’.
Mshauri wa Jumuiya ya Wafanyabiashara hao Mkoa wa Dar es Salaam, Johnson Minja, alisema wafanyabishara hawataki mashine hizo kwa kuwa mfumo huo unatoa mwanya wa rushwa na  ndiyo maana Jumuiya ya Wafanyabishara iliandika waraka kwa Wizara  ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Ikulu ili mfumo huo upitiwe upya.
Alisema katika waraka ulioandikwa mwaka jana, Jumuiya iliomba Tume ya Kuchunguza Usahihi wa Mashine iundwe kwani wanaona kama ni mpango wa kuendeleza rushwa.
“Sheria ya kutumia mashine hizo haina tofauti na mfumo ulioanzishwa wa udhibiti wa mwendo kasi wa mabasi –Speed Govenor- ambao baadaye ilibainika kuwa ni dili la watu wachache,” alisema Minja  na kuongeza kuwa  ni vema ingeundwa Tume shirikishi.
Alisema licha ya Jumuiya hiyo kuomba kuundwa kwa Tume, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, aliona ni vema kuundwa kwa kikosikazi ambacho kingeangalia mfumo wa utendaji wa mashine  hizo kwa mwezi mmoja na walikubaliana kutokubaliana.
Minja alisema wao wanasisitiza iundwe Tume huru ambayo itafanya kazi kwa miezi sita na ndani ya muda huo, mashine hizo zisitumike.
Pia walilalamikia Mamlaka ya Usimamisi wa Bandari (TPA)  kuwa imekuwa kiini cha tatizo la ukusanyaji kodi kwa kuchelewesha mizigo yao.
Malalamiko mengine yalielekezwa kwa askari Polisi wa Kikosi cha Doria ya Pikipiki  kwamba wamekuwa kero kwao kwa kuona mashine hizo kama mpango wao wa kujipatia kipato  na  wakati mwingine wakiona mfanyabiashara na mzigo hufikia hata kumtoza Sh 500,000.
Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Lazaro Benedict, alitaka wafanyabiashara watakaokutana na askari wanaowatoza fedha kinyume cha sheria, wakatae na kutoa taarifa kwenye vituo vya Polisi.

No comments: