HIVI NDIVYO MWENYEKITI WA CHADEMA ALIVYOCHUNGULIA JEHANAMU...

Mhudumu wa Hospitali ya Muhimbili akimrejesha Joseph Yona wodini baada ya kufanyiwa matibabu katika Kitengo cha Mifupa cha MOI, Dar es Salaam jana.
Mgogoro unaoendelea ndani ya Chadema una uhusiano na tukio la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Wilaya ya Temeke, Joseph Yona, Polisi imesema.

Hatua za awali za upelelezi wa tukio hilo kwa mujibu wa Polisi, kimazingira zinaonesha kuwa linatokana na mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho, huku kukiwa hakuna chanzo kingine kinachohusishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Dar es Salaam Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema kwa mujibu wa Yona, kabla ya tukio alikuwa mwenye hofu kutokana na kupokea simu nyingi na ujumbe mfupi wa maneno wa vitisho, kutoka kwa viongozi mbalimbali wa chama hicho ambao alidai kuwafahamu.
Kamanda alisema Yona alikamatwa na watuhumiwa hao akiwa na wenzake watatu eneo la Mtoni kwa Aziz Ally akinywa vinywaji katika duka la Mgumbini na baadaye kwenda kutupwa Ununio nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Kova aliongeza kuwa kwa mujibu wa maelezo ya mlalamikaji, juzi saa 5 usiku akimalizia kunywa na wenzake, walifika watu sita wakijitambulisha kuwa askari Polisi na kumtaka wafuatane kituo kikuu cha Polisi.
"Baada ya kujitambulisha kuwa polisi, hata hivyo kati yao alimtambua mmoja kwa sura na jina, kwamba ni mwanachama mwenzake wa Chadema, lakini alipohoji kuwapo mtu huyo, haraka walimwingiza katika gari aina ya Toyota Land Cruiser na kumfunga kitambaa usoni ili asiwaone," alisema Kamanda Kova.
Kutokana na maelezo ya Yona, Kova alisema watu hao walimhoji sababu za  kuendelea kumshabikia Kabwe Zitto  wakati ni mtu anayeharibu chama.
Aidha, walimtaka awaoneshe mahali aliko rafiki yake aitwaye Habibu Mchange, huku akiendelea kuhojiwa na kupigwa baada ya kutaka kujua sababu ya kutopelekwa  Kituo cha Polisi, mpaka alipopoteza fahamu.
"Alizinduka usiku wa manane na kujikuta kichakani sehemu asiyoitambua na kuanza kutangatanga akitafuta msaada akiwa na maumivu makali.
"Baada ya muda alimpata mlinzi aitwaye Ismail Swalehe na kumwomba msaada wa kumpeleka Kituo cha Polisi, lakini kabla ya kufanya hivyo,  alimpeleka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ununio," alisema.
Aliongeza kuwa juzi Ofisi ya Chadema Temeke, inayotumiwa na Yona, ilifungwa saa 10 jioni kwa kilichodaiwa kuwa ni maagizo kutoka ngazi za juu za uongozi wa chama hicho.
"Kutokana na tukio hili, nimeunda jopo la wapelelezi waliobobea katika fani mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu, ACP Jaffar Mohamed, ili kubaini na kuwakamata watuhumiwa," aliongeza.
Alitaka watuhumiwa hao wajisalimishe,  kwa kuwa mlalamikaji ametambua mmoja na bado anaendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi, huku akitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kova alitoa onyo kwa makundi yakiwamo ya dini kufuata taratibu za kisheria  kutatua migogoro badala ya kutumia nguvu na vitisho ikiwamo utekaji nyara.
Akizungumza akiwa kitandani, Yona alidai baada ya kumtesa kwa kipigo kikali, aliwasihi wasimwue kwani ana watoto watatu wadogo wanaomtegemea.
"Niliwaomba wasiniue, nikawaambia wakiniua watoto wangu watapata shidaÉkwani nao wana watoto kama mimi, niliwasihi waniachie roho yangu,"  alisema Yona.
Dhambi ya Yona ni kujipambanua kumwunga mkono Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho aliyeondolewa madarakani, Kabwe Zitto  kwenye mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho.
Yona baada ya Kamati Kuu kumvua madaraka Zitto mwezi uliopita, alijitokeza hadharani akatoa tamko kulaani hatua hiyo na kushauri uongozi wa chama hicho kuitisha Baraza Kuu la Chama ili liweze kutenda haki kwa wanachama waliovuliwa nyadhifa.
Yona alifanyiwa ukatili huo katika eneo maarufu kwa jina la 'Kwa Wasomali' kwa kupigwa mbavuni na kichwani hata kulazwa Muhimbili ambako alifikishwa jana asubuhi na polisi wa Kinondoni.
Akizungumza kwa taabu kitandani Muhimbili kabla ya kuingizwa wodini, Yona alisema alitekwa na watu sita akiwa katika maeneo ya karibu na ofisi ya chama hicho Kwa Aziz Ally.
Alisema alikuwa na watu wengine wanne, ndipo walitokea watu hao sita na kujitambulisha kuwa mapolisi na kumkamata kwa nguvu ambapo katika purukushani ile, simu yake ilidondoka ikaokotwa na watekaji hao.
Aliongeza kuwa watekaji hao licha ya kujifanya polisi, walimvua fulana na kumfunga nayo usoni na kuchukua kitambaa chake cha mkononi wakamfunga mikono kwa nyuma na kumpandisha garini. Alisema wenzake aliokuwa nao baada ya kuona hivyo walikimbia.
"Wakati wananipandisha kwenye gari walisema wananipeleka Polisi kwa mahojiano, lakini tukiwa ndani ya gari ambalo alisema hakumbuki aina yake aliingiwa na hofu baada ya kuhisi kuwa hapelekwi Polisi kutokana na gari kwenda umbali mrefu.
"Nikawauliza jamani kweli tunakwenda Polisi mbona hatufiki? Wakanitaka nitulie kwani kuna maswali wanahitaji kunihoji. Wakati tunaendelea na safari wakanilazimisha niwatajie password (nywila) ya simu yangu na nisipofanya hivyo wataniua," alisema Yona.
Alisema aliwatajia nywila ya simu yake ya Tigo wakaipekua huku wakieleza kuwa wanaamini watapata taarifa muhimu zitakazowasaidia kwenye kazi yao.
Alisema baada ya kama ya saa moja hivi tangu kutekwa kwake, walifika Ununio, Kawe ambako walimshusha na kumtesa huku wakimhoji maswali mengi kwa nini anaivuruga Chadema.
Alifafanua kuwa walimlazimisha awaambie uhusiano wake na Zitto na pia aombe msamaha kwa kitendo chake cha kusaliti chama; la sivyo watamwua. Alisema wakati wanamhoji maswali hayo waliendelea kumtesa na kisha kumchoma kwenye paji la uso na kitu cha ncha kali.
Alisema wakiwa wamemtoa ndani ya gari walimpiga kwa magongo na kumwumiza vibaya. "Niliwaomba wasiniue, kwani nina watoto watatu wanaonitegemea.
"Waliniuliza kwa nini nilitoa tamko la kupinga Kamati Kuu ya Chama, nami nikajitetea kuwa sikupinga Kamati Kuu ila nilishauri Baraza Kuu liitishwe ili  kutenda haki kwa pande zote," alisema Yona.
Yona alisema alitoa tamko lile akiamini kuwa ndani ya Kamati Kuu wanakaa watu wachache wenye uwezo, lakini Baraza Kuu lina wanachama wengi wenye mawazo tofauti na maamuzi yaliyochukuliwa na kikao hicho.
Mwana Chadema huyo alisema anaamini waliofanya kazi hiyo wamekodiwa na uongozi wa chama hicho makao makuu wamtese, kwa vile ametofautiana nao katika suala la Zitto.
Yona alisema aliteswa kuanzia saa tano usiku hadi saa tisa alfajiri na kuzirai lakini akazinduka saa 11 alfajiri na kujikongoja kwenda kwenye nyumba za watu kuomba msaada.
"Niligonga nyumba ya kwanza hawakufungua, nikaenda ya pili hawakufungua pia, sikukata tamaa nikaenda nyumba ya tatu ndipo akatokea msamaria mwema," alisema Yona.
Mkuu wa Ulinzi wa Ununio, Abdul Ally, alisema alipata taarifa saa 9 alfajiri juzi  kutoka kwa mlinzi wa zamu, Seleman Salehe, kwamba kuna mtu analia akihitaji msaada ambaye anadai ametekwa na kupigwa na watu wa Chadema.
Ally alidai, Yona alijikokota kutoka porini alikotupwa na kufika kwenye mlango mkubwa wa nyumba aliyokuwa akilinda na kuomba msaada, huku amevuliwa shati na damu ikimbubujika kichwani.
Mashuhuda hao walidai kuwa baada ya kufika kwenye nyumba hiyo, walimsikiliza na kumpa shati kwani alikuwa hajiwezi. 
Mwandishi alilifika ofisi za Chadema makao makuu Kinondoni na kukuta viongozi na wafuasi wa chama hicho wakiwa kwenye maandalizi ya kwenda mahakamani, lakini Ofisa Habari wa Chama hicho, Tumaini Makene alizungumza:
"Hapa kwa leo hatuwezi kuongea, kwani watu unaona wana vikao vyao, ila kuhusu suala hilo tayari naandaa taarifa na naomba tu nikutumie kwenye anuani ya barua pepe yako," alisema Makene.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tukio hilo, Chadema ilitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili ukweli ujulikane na haki itendeke kwa sheria kuchukua mkondo wake.
"Chama kinataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kutulia, hasa pale ambapo watu wenye hila na malengo yao, wanaanza kukihusisha chama na tukio hilo. Watambue kuwa pamoja na mtu yeyote kuwa kiongozi wa chama, bado ana maisha yake na uhusiano na watu wengine katika jamii," ilisema taarifa hiyo.
Ilisisitiza kuwa Polisi inapaswa kuyachukulia uzito mkubwa na unaostahili, matukio ya namna hii ambayo yanaanza kuota mizizi, kutokana na watu waovu wanaoyatekeleza kutochukuliwa hatua za kisheria ambazo zingesaidia kuzuia yasitokee tena.
Chadema katika taarifa hiyo ilitolea mifano ya kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, ikisema Watanzania bado wanakumbuka kuwa hadi sasa Polisi imeshindwa kutoa taarifa za kina na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
"Ni kutokana na Jeshi hilo kushindwa kuwajibika ipasavyo katika matukio mengine ya namna hiyo, watu waovu wanaweza kutumia mwanya wa kinachoendelea ndani ya Chadema,  kwa chama kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanachama wasio waadilifu, kufanya matukio ya namna hiyo ili kujenga taswira ya kukihusisha na uhuni huo unaobeba kila sifa ya kuitwa ukatili dhidi ya binadamu," iliongeza taarifa.
Ilisema kushindwa kwa Polisi kuwajibika ipasavyo katika uchunguzi wa matukio hayo na mengine ya namna hiyo, Jeshi hilo linazidi kujiweka katika wakati mgumu wa kukwepa tuhuma za baadhi ya watendaji wake, kujua na kushiriki masuala haya, hususan kwa kurejea tukio la kutekwa kwa Dk Ulimboka.
Saa chache kabla ya tukio la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti huyo wa Chadema, Temeke, Ofisa Habari, Makene, alituma ujumbe wa simu kwa wahariri kwenye vyumba vya habari akiwapa 'tip (dokezo)' kwamba:
"Waweza kuifanyia kazi uwezavyo kupata stori  genuine (habari halali). Mwenyekiti wa  Chadema Temeke akishirikiana na mtu anayedaiwa kuwa Kambaya (Abdul-Naibu Mkurugenzi na Uhusiano wa Umma) wa CUF wanaratibu kuleta watu mahakamani, wanawapa tisheti (fulana) za M4C na Sh 20,000.
"Wameleta wahuni kabisa wanavuta bangi hadharani wamepewa visu na mapanga, tuombe Mungu tumalize salama. Hii yote ni kazi ya uratibu wa team (timu) ya Zitto (Kabwe). Lengo ni kutaka kumwaga damu za watu, ionekane Chadema wamekatana mapanga kwa sababu ya hiyo. Hiyo ni mbali ya wahuni walionunuliwa kwa ajili ya kubeba mabango na waimbe nyimbo mahakamani. Kama ilivyokuwa Kigoma."

No comments: