MVUA YASITISHA USAFIRI RELI YA KATI, ABIRIA WALETWA DAR KWA MABASI...

Abiria hao wakiwa hawajui la kufanya kabla ya kutangaziwa watasafiri kwa mabasi.
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imetangaza kusitisha huduma za usafiri wa treni kwa muda usiofahamika kutokana na kuharibika kwa miundombinu yake eneo la Godegode na Gulwe, Dodoma.
Usitishaji huduma hizo ulitangazwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Paschal Mafikiri wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam.
Mafikiri alisema kuharibika kwa miundombinu hiyo kulitokana na mvua zinazoendelea Dodoma, Morogoro, Iringa na Singida na hivyo kuwasiliana na serikali na kufikia makubaliano ya hatua hiyo.
Aidha, alisema mvua hizo zimesababisha kujaa maji katika eneo kati ya stesheni ya Godegode na Gulwe.
"Tunasitisha mpaka tutakapotangaza tena, wahandisi wamekwenda kuangalia jinsi na muda gani tatizo linaweza kutatuliwa, kwa sababu mvua bado ni kubwa," alisema Mafikiri.
Alisema ili kusaidia abiria waliokwama Dodoma, mabasi 16 yalikodishwa kuchukua baadhi yao kuwafikisha Dar es Salaam huku waliosalia wakitafutiwa utaratibu mwingine.
Aliongeza kuwa abiria walio Dar es Salaam walirudishiwa nauli zao tangu jana. Akizungumzia kuharibika kwa reli mara kwa mara Godegode alisema reli imepita bondeni.
"Pale Godegode reli imepita kwenye bonde, hivyo mvua zinaponyesha maji hujaa, lakini tumeshafanya utaratibu na kuna Wajapani wako pale kuangalia njia inayoweza kutumika kukwepa bonde," aliongeza.
Abiria waliozungumza na gazeti hili walisema ni tatizo kwao, kwani baadhi yao wametoka   mbali na hawana fedha za kutosha kujikimu.
Gifat Mahundi alitaka TRL iangalie utaratibu wa kuwasaidia ili wafike waendako kwani ni vigumu kurudi walikotoka kwani walishajipanga kwa safari.
Fauzia Msando alisema juzi waliambiwa kuwa safari imeahirishwa hivyo wangeondoka jana saa 10 jioni, lakini haikuwa hivyo na badala yake wakarudishwa nauli.
Ili kuwaondolea usumbufu abiria waliokwama Dodoma, uongozi wa TRL jana ulisafirisha kwa mabasi abiria 1,600 wa treni ya Kigoma - Dar es Salaam kutokana na njia ya reli kuendelea kujaa maji.
Baadhi ya abiria waliiomba Serikali iboreshe miundombinu ya reli kama inavyofanya kwa viwanja vya ndege ambavyo hata hivyo vinatumiwa na watu wachache ikilinganishwa na wanaotumia reli.
Mkuu wa Stesheni ya Dodoma, Zacharia Kilombele alisema TRL kwa kushirikiana na Serikali Dodoma waliamua abiria hao wasafirishwe kwa mabasi na mpaka jana mchana zaidi ya mabasi 17 yalikuwa yamepakia abiria wa Dar es Salaam huku mabasi mengine 10 yakisubiriwa kusafirisha waliobaki.
Alisema changamoto kubwa ni baadhi ya abiria kuwa na mizigo mingi na mikubwa hali inayosababisha ugumu katika kuwasafirisha.
Juzi baadhi ya abiria waliandamana kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi kutaka watafutiwe usafiri mbadala baada ya kusota stesheni mbalimbali kwa zaidi ya siku saba.

No comments: