KIFO CHA RAIS KAGAME WA RWANA UZUSHI MTUPU...

Rais Paul Kagame.
Ikulu ya Rais wa Rwanda imekanusha uvumi wa kifo cha Rais Paul Kagame, ambao umesababisha raia wa mji wa Goma kuingia barabarani kusherehekea taarifa hiyo.
Rwanda iliingia kijeshi mara kadhaa kwenye ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hasa ikiunga mkono waasi dhidi ya utawala wa DRC wakati wa vita iliyoibuka nchini DRC wakati  ikiitwa Zaïre katika miaka ya 1996-1997 na 1998 hadi 2003.
Rwanda jana ilielezea kwa mshangao uvumi huo uliozagaa, huku raia wa Mashariki ya DRC wakiandamana kuonesha kufurahia taarifa hiyo potofu.
Ofisa wa Ikulu ya Rais wa Rwanda, aliiambia AFP kwamba taarifa ya kifo cha Rais Kagame ni uvumi mtupu.
“Rais wakati huu anakutana kwa mazungumzo na wanafunzi wa chuo kikuu kutoka Marekani. Mko huru kuja kuhudhuria kikao hicho na mkutane naye,”  alisema ofisa huyo.
Kagame(56), ni Rais wa Rwanda tangu 1994, baada ya waasi wa RPF kushinda Jeshi la Rwanda lililokuwa likimwunga mkono Rais Juvenal Habyarimana. Chanzo cha kushindwa kwa Jeshi la Rwanda ni mauaji ya kimbari, ambayo yalihusisha Jeshi hilo. Watu 800,000, wengi wao kutoka jamii ya Watutsi waliuawa.
Wafuasi wa Rais Kagame wanamsifu kuwa mtu mwenye mtazamo katika masula ya uchumi, na lengo lake ni kuendeleza Rwanda, huku wapinzani wake wakimtuhumu kujihusisha na azma ya kutaka kufuta vyama vya upinzani.
Siku za karibuni alituhumiwa kujihusisha na mipango ya kuua mahasimu wake, akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda chini yake,  Jenerali Kayumba Nyamwasa na Mkuu wa zamani wa Usalama wa Taifa, Patrick Karegeya ambaye aliuawa hivi karibuni nchini Afrika Kusini.

No comments: