MAFURIKO YASOMBA BARABARA MOROGORO-DODOMA...

Daraja la Mkundi likiwa limebomolewa kabisa na mafuriko hayo.
Mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha katika milima ya Kiteto mkoani Manyara, yamesababisha maafa katika Wilaya ya Kilosa na kukata mawasiliano ya barabara kati ya Morogoro na Dodoma.

Mawasiliano hayo ya barabara yalikatika baada ya mafuriko hayo yaliyotokana na mvua za usiku wa kuamkia jana, kuvunja tuta la Daraja la Mkundi eneo la Dumila katika barabara kuu ya Dodoma-Morogoro-Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliyefika kujionea maafa hayo jana, Diwani wa zamani wa Magole, Shaaban Mdunda, alisema mafuriko hayo yameathiri wananchi wa vijiji vya Mateteni, Mbigiri, Mabana na Kituo cha Elimu Dakawa.
Maji kutoka milima ya Kiteto, yalianza kuingia kwa wingi na kwa kasi katika vijiji hivyo saa 12 asubuhi na kusababisha wananchi kukimbia kuokoa maisha yao na hakuna aliyeokoa mali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema amepata taarifa ya kifo cha mkazi wa Kijiji cha  Mateteni.
Kutokana na hali kuwa mbaya, Mkuu wa Mkoa aliagiza helikopta ya Polisi iliyowasili saa tisa alasiri na Kamishna wa Polisi, Paul Chagonja ambapo Bendera, Shilogile na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, walitumia usafiri huo kuzungukia maeneo yaliyoathirika.
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Dorothy Mtenga, alisema tuta la daraja hilo limeathirika upande wa Morogoro kwa urefu wa meta 40 na upande wa Dumila, meta 10.
Kwa mujibu wa Mtenga, kazi ya kurejesha daraja hilo itachukua zaidi ya wiki mbili na madereva wametakiwa kutumia barabara inayopita Kilosa kwenda Iringa na kutokea Dumila kwenda Dodoma.
Kutokana na mafuriko hayo, baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo walilazimika kupanda kwenye mapaa ya nyumba na miti kuokoa maisha yao, huku baadhi ya mali zikielea majini.
Majengo ya huduma za umma ikiwamo Shule ya Msingi Magole, Mahakama ya Mwanzo na Msikiti, yalizingirwa na maji mengi yaliyokuwa yakiingia ndani kupitia madirishani.
Barabara ya Magore-Turiani pia iliharibiwa na kusababisha abiria wengi kukwama njiani, huku baadhi wakitumia usafiri wa bodaboda hadi eneo la Feri Dumila ambako walipata usafiri wa Morogoro.
Mabasi yanayotoka Dodoma kwenda Morogoro na Dar es Salaam na ya Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma na mikoa mingine ya Kaskazini, yalilazimika kufuata ushauri wa Tanroads, na kuendelea na safari.
Baadhi ya waathirika, Hassan Changi na Omari Musa, kwa nyakati tofauti walilalamika kupata hasara ambayo hawajaibaini, kwa kuwa hawakuwa wakijua hatma ya nyumba  na mali zao na kuomba mahema  na vyakula.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, ilisema jana itapeleka mahema hayo na chakula kwa ajili ya waathirika.
Akizungumzia hali hiyo, Bendera alisema Serikali inafanya tathmini na itatoa maelezo kamili baada ya kupata taarifa za hali halisi.

No comments: