JAJI LIUNDI, MBUNGE HASHIM SAGGAF WAFARIKI DUNIA...

KUSHOTO: Mbunge wa zamani, Hashim Saggaf. KULIA: Jaji George Liundi.
Aliyekuwa Msajili wa Kwanza wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji George Liundi amefariki dunia na anatarajiwa kuzikwa kesho kutwa, katika makaburi ya Chang’ombe, Dar es Salaam karibu na walikozikwa watoto wake watatu waliofariki dunia Septemba 1978.

Mtoto wa Jaji Liundi, Taji, alisema hayo jana nyumbani kwao Keko Juu, Dar es Salaam alipozungumza kuhusu kifo hicho na kueleza kuwa baba yake alifariki dunia juzi saa sita mchana akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ baada ya hali yake kiafya kubadilika ghafla.
Taji alisema tangu mwaka jana, baba yake alikuwa akisumbuliwa na malaria na shinikizo la damu, lakini hali yake ilikuwa nzuri kila alipopata tiba lakini ilibadilika mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Siku tatu (nne) zilizopita-Ijumaa, alianza kulalamika  maumivu makali ya mgongo, daktari wake akamtibu akawa anaendelea vizuri kidogo, hakulazwa.
“Jumamosi hali ikabadilika tena daktati akaja nyumbani na kumfuatilia zaidi, Jumapili akaumwa zaidi mpaka akaitisha barafu awekewe mgongoni wamkande,” alisema Taji.
Alisema hali hiyo ilisababisha waamue kumpeleka TMJ na wakiwa njiani walihisi amezimia kutokana na namna alivyokuwa na walipofika hospitali, madaktari waliwaarifu kuwa ameshafariki dunia.
Taji alisema anamshukuru Mungu kwa maisha ya baba yake na kwamba amefariki dunia bila usumbufu mkubwa hivyo amekwenda kwa amani.
Hata hivyo, alisema amepoteza kiungo katika maisha yake hasa kutokana na ukweli kwamba, baada ya kifo cha wadogo zake watatu miaka zaidi ya 30 iliyopita, ndugu pekee wa karibu alikuwa baba yake.
Kwa mujibu wa Taji, kabla ya maziko, kutakuwa na ibada fupi nyumbani asubuhi na kisha mwili utapelekwa katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Kurasini kwa Ibada ya Misa kisha makaburini kwa maziko.
Jaji Liundi alikuwa mwanadiplomasia wa siku nyingi na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Alihusika pia kuandika Katiba ya sasa  mwaka 1977 na mwaka 2011 alizungumzia Katiba akisema iliyopo imepitwa na wakati na kinachohitajika ni wananchi kuunganisha nguvu ya pamoja kupata Katiba itakayolinda maisha ya watu.
“Hata mimi ambaye ndiye niliyeandika Katiba hii, naona imepitwa na wakati. Tunahitaji kuandika Katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya wananchi kwa miaka 50 ijayo,” alisema Jaji Liundi katika Tamasha la 10 la Jinsia lililofanyika katika Viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Mabibo, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Mchafukoge, Ilala, Dar es Salaam na Mbunge wa zamani wa Dodoma Mjini, Hashim Saggaf alifariki dunia jana Dar es Salaam na kuzikwa katika makaburi ya Kisutu jioni.

No comments: