Vuai Ali Vuai. |
Moja ya mambo yatakayoathiri kipato cha wananchi wa Zanzibar, ni kuondolewa kwa suala la elimu ya juu katika mambo ya Muungano.
Akizungumza jana na wanachama wa CCM katika Jimbo la Amani, Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alitaka Wazanzibari wajiandae kusomesha watoto wao elimu ya juu.
“Wazazi wajiandae kutoa fedha zaidi kusomesha watoto wao, kwani Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar haina uwezo mkubwa wa kugharimia masomo ya wanafunzi wengi wa Zanzibar,” alisema.
Alisema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar mwaka 2012/13, ilitoa mikopo kwa wanafunzi wa Zanzibar wapatao 860, lakini Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Muungano ilitoa mikopo kwa Wazanzibari 1,024.
“Sisi CCM katika Tume ya Marekebisho ya Katiba, tulitaka suala la elimu ya juu libaki kuwa mambo ya Muungano kwa sababu Wazanzibari wanafaidika na fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi zote mbili,” alisema.
Pia alisema CCM inaamini, kwamba mfumo wa serikali mbili ndio imara zaidi utakaolinda Muungano, kwa sababu Watanzania wengi na Wazanzibari kwa zaidi ya miaka 50 sasa, wamekuwa wakiishi chini ya muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kuna mambo 22 ya Muungano ambayo yamepunguzwa katika Rasimu ya Pili na kubaki saba.
Katika Katiba ya sasa, mambo ya Muungano ni pamoja na Katiba ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Mambo ya Nchi za Nje; Ulinzi na Usalama; Polisi; Mamlaka Juu ya Mambo Yanayohusika na Hali ya Hatari; Uraia; Uhamiaji; Mikopo na Biashara za Nje.
Pia kuna Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Kodi ya Mapato Inayolipwa na Watu Binafsi na Mashirika, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa Zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha.
Mengine ni bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, Posta na Simu; Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti); benki (benki za kuweka akiba) na shughuli zote za benki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha hizo.
Pia ipo leseni ya viwanda na takwimu; elimu ya juu; maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya magari na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia.
Mengine ni Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yote yanayohusika na kazi za Baraza hilo; Usafiri na usafirishaji wa anga; Utafiti; Utafiti wa hali ya hewa; Takwimu; Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano; Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo.
Katika Rasimu ya Pili ya Katiba, mambo saba yanayopendekezwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Uraia na Uhamiaji; Sarafu na Benki Kuu; Mambo ya Nje; Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Pamoja na athari ambazo CCM inaziona, mmoja wa watetezi wa mfumo wa serikali tatu, Mwenyekiti Msaidizi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Augustino Ramadhani, alikaririwa hivi karibuni akisema serikali tatu ndiyo itakayonusuru Muungano.
Kwa mujibu wa Jaji Ramadhani, serikali tatu haziepukiki kwa kuwa tayari Katiba ya Jamhuri ya Muungano iliyopo, imeshavunjwa.
Alifafanua, kwamba Zanzibar tayari ina Katiba yake inayoitambulisha kama nchi kamili, hatua ambayo alieleza kuwa inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inayotambulisha Tanzania ni nchi moja inayotokana na muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar.
“Leo hii Zanzibar wana Katiba inayotambulisha nchi yao na ukisema unataka serikali mbili au moja, utakuwa unaizima Katiba ya Zanzibar na kukaribisha matatizo makubwa katika Muungano,” alikaririwa Jaji Ramadhani.
Sababu ya pili ya kupendekezwa serikali tatu kwa mujibu wa Jaji Ramadhani, ni maoni kutoka Zanzibar ya Muungano wa Mkataba, ambapo watoa maoni wanataka kuwe na makubaliano fulani tu huku Zanzibar ikibaki kuwa nchi kamili yenye kiti Umoja wa Mataifa.
Jaji Ramadhani alikaririwa akisema tatizo la watoa maoni hao hawakuweka bayana nani atasimamia makubaliano hayo, lakini pamoja na upungufu wa watoa maoni, waliona ili kunusuru Muungano, bora kufuata maoni na utashi wa wengi wa kuwa na serikali tatu.
Sababu ya tatu iliyotajwa ni uwezekano wa sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, kutupiliwa mbali na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Jaji Ramadhani alikaririwa akisema sheria zinazotungwa na Bunge, lazima zijadiliwe upya na Baraza la Wawakilishi na wakati mwingine zinakataliwa na hivyo kujikuta sheria inafanya kazi upande mmoja wa Muungano, wakati imetungwa na chombo cha Muungano.
Vuai katika mkutano huo, ambapo pia aliweka jiwe la msingi la tawi ambalo awali lilichomwa moto na wafuasi wanaodaiwa kuwa wa Uamsho, alisema watapitia upya Rasimu ya Pili ya Katiba na kutoa mapendekezo yao kwa wabunge na wawakilishi watakaoshiriki Bunge Maalumu la Katiba linalotarajiwa kuanza karibuni.
“CCM Zanzibar itakutana katika kikao ambacho tutajadili upya Rasimu ya Pili ya Katiba iliyopendekezwa na Jaji Warioba (Joseph, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba)...kazi yote tutawatwika mzigo wabunge wetu na wawakilishi watakaokwenda Bunge Maalumu la Katiba,” alisema.
Alisema licha ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuja na msimamo wa serikali tatu, bado CCM haijaridhishwa na msimamo huo.
No comments:
Post a Comment