HIKI NDICHO KIINI CHA AJALI YA MELI YA MV KILIMANJARO...

Mawasiliano duni kati ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na nahodha wa meli ya MV.Kilimanjaro II, yanadaiwa kwa kiasi kikubwa yamechangia vikosi vya uokozi, kushindwa kufika katika eneo la ajali kwa haraka.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, Abdi Omar alisema mara baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa msukosuko wa dhoruba katika boti hiyo, walimtafuta nahodha wa meli hiyo, ambaye walishindwa kuwasiliana naye kwa ajili ya kujua hali ya boti na kama wanahitaji msaada wa dharura.
“Mawasiliano duni yalipelekea Mamlaka na vikosi vya uokozi kushindwa kutoa huduma za dharura kwa haraka katika boti hiyo ambapo jumla ya watu watano walifariki dunia hadi hivi sasa wakati zoezi la kuwatafuta watu wengine likiendelea,” alisema Omar.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundo Mbinu, Issa Haji Ussi alisema kazi ya kutafuta maiti zaidi, inaendelea kwa ajili ya kujiridhisha.
“Tunaendelea kuwatafuta watu wengine zaidi ambao wanahofiwa wamefariki dunia kwa ajili ya kujiridhisha zaidi,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hassan Msangi alisema juhudi za kutafuta maiti zaidi inaendelea kwa kushirikiana na wazamiaji wa Kijiji cha Nungwi na vikundi vya wazamiaji, wanaofanya kazi katika hoteli za kitalii.
Wanatumia vikosi mbalimbali, ikiwemo wanamaji wa KMKM na vikundi vya wazamiaji wa Ushirika wa Nungwi.
Boti ya Kilimanjaro 11 ilikuwa ikitoka Pemba, ikiwa na abiria wanaokisiwa 369, wakiwemo watoto 60 ambao walikuwa wanatoka likizo ya kila mwaka ya masomo, kufuatia kufunguliwa kwa shule za Unguja.
Ilipofika  katika mkondo wa Nungwi, ilikumbwa na dhoruba, iliyosababisha baadhi ya abiria waliokaa pembeni kudondoka.
Mzee Khamis Issa amepoteza watoto watatu, ambao walifariki dunia baada ya kudondoka katika boti hiyo kwa kupigwa na wimbi .
Watoto waliofariki na kuzikwa juzi ni Nadhif Khamis Issa, Nashra Khamis Issa na Akram Khamis Issa, wote wakiwa wanafunzi wa shule za Unguja.

No comments: