DIWANI WA CHADEMA AMFUNGIA OFISINI MKURUGENZI ILEMELA...

Abubakar Kapera.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Zuberi Mbyana amefungiwa ofisini na Diwani wa Nyamanoro, Abubakar Kapera (Chadema) na kusababisha vurugu.
Diwani Kapera alimfungia Mkurugenzi huyo jana wakati akiwa ofisini kwake na madiwani watano wa Chadema ambamo awali Kapera naye alikuwa akihudhuria kikao hicho, lakini muda mfupi baadaye alitoka na kurudi na kufuli.
Sakata hilo lilitokea saa 4.45 asubuhi wakati madiwani hao wakiwa katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya kushiriki kikao maalumu cha kupitisha bajeti ya mwaka 2014/15.
Kapera alipohojiwa sababu ya kufanya hivyo, alisema ataendelea kufanya hivyo hadi haki ya wananchi itakapopatikana na baada ya hapo alikwenda katika ofisi ya Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia na ndipo vurugu zikaanza.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza alitoka ofisini kwake na kuwataka watu warudi sehemu zao za kazi huku akisisitiza aliyefunga mlango wa Mkurugenzi aufungue
Mgambo wa Halmashauri walimfuata Kapera na kumfikisha katika ofisi ya Mkurugenzi ili afungue mlango huo huku watu wakimshambulia kwa maneno na hata kurushiwa ngumi na Mstahiki Meya wa Ilemela, Henry Matata.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya sakata hilo, Kapera alidai kuwa walijiandaa kumfungia Mkurugenzi huyo kwa lengo la kutetea wana Ilemela na pia atambue kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi.
Mbunge Kiwia alisema kilichotokea ni mwendelezo wa huduma za viongozi wa mkoa, wilaya na Meya dhidi ya Chadema.
Alisema kwa muda mrefu kanuni na taratibu za halmashauri zimekuwa zikikiukwa tangu uchaguzi wa Meya na hatua zimechukuliwa lakini bila ufumbuzi kupatikana.
Kiwia aliongeza kuwa madiwani watatu wa Chadema walifukuzwa kinyume na utaratibu ambao ni Danny Kahungu wa Kirumba, Marietha Chenyenye wa Ilemela na Kapera na kusababisha wananchi kukosa maendeleo.
 “Haki inayocheleweshwa ni sawa na iliyopotea na huu unaonekana ni mkakati wa kuidhoofisha Chadema kisiasa, tunahitaji uchaguzi halali na tutaendelea kudai haki ili itekelezwe,” alisema Kiwia na kuongeza kuwa suala la madiwani hao liliishatolewa uamuzi na Waziri Mkuu.
Baada ya vurugu hizo kikao cha bajeti kiliendelea bila madiwani wa Chadema kushiriki ambapo wajumbe wa kikao hicho walipitisha bajeti ya Sh bilioni 35.4 ya mwaka 2014/15.
Akisoma bajeti, Mweka Hazina wa Manispaa ya Ilemela, Lainie Kamendu alisema bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 18.8 ikilinganishwa na mwaka 2013/14 ambayo ilikuwa zaidi ya Sh bilioni 29.8.
Hata hivyo, Kiwia alidai kuwa bajeti hiyo ilipitishwa bila kuzingatia idadi ya madiwani walioshiriki.
Alisema haikuwa nia yao kutoshiriki kwa sababu walikuwa na maswali ya kuhoji lakini wakati wakijiandaa kuingia kwenye kikao walishanga kuona kimemalizika.
Wakati madiwani wa Chadema wakijiandaa kuondoka, nje walikuta gari la Polisi likiwa na askari kanzu tayari kumchukua Kapera kwenda naye Polisi kutoa maelezo  juu ya kumfungia Mkurugenzi ofisini.
Diwani huyo aligoma kupanda gari akidai kuwa angekwenda mwenyewe lakini polisi hawakuwa tayari kuondoka bila yeye, ingawa mwenzake, Chenyenye alipanda.

No comments: