SERIKALI YASALIMU AMRI KWA MAJANGILI VITA DHIDI YA TEMBO...

Mabaki ya miili ya tembo waliouawa kikatili ikiwa ni matokeo ya ujangili.
Sensa maalumu kwa ajili ya tembo iliyofanyika nchini kati ya Oktoba na Novemba mwaka jana imeonesha kuwa, maeneo ya mfumo wa Ikolojia wa Selous-Mikumi na Ruaha-Rungwa yamebakiwa na idadi ya tembo 33,174 mwaka huu ukilinganisha na tembo  105,867 waliokuwepo mwaka 2006.
Akitangaza matokeo ya sensa hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema, hali hiyo imetokana na wimbi la majangili wanaoua wanyama hao kwa ajili ya kuchukua meno yao.
Kufuatia hali hiyo alisema Operesheni Tokomeza awamu ya pili itaanza kwa lengo la kukabiliana na majangili wanaoua tembo kwa lengo la kuchukua meno yao.
Hata hivyo, alisema kuanza kwa operesheni hiyo kutatangazwa muda ukifika.
Akifafanua idadi ya tembo waliokuwepo mwaka 1976 na hali ilivyo hivi sasa, Nyalandu alisema, Mfumo wa Ikolojia wa Selous – Mikumi mwaka huo kulikuwa na tembo 109,419.
Na kwamba idadi hiyo ilipungua hadi kufika 22,208 mwaka 1991 kulikotokana na wimbi la ujangili dhidi ya wanyama hao kulikoshamiri kuanzia mwaka 1984 hadi 1989.
Nyalandu aliongeza, baada ya Serikali kuona hivyo ilichukua hatua ambapo Operesheni Uhai ilifanywa pamoja na juhudi za kimataifa za uhifadhi ikiwemo kusitisha biashara ya meno ya tembo.
Matokeo ya operesheni hiyo yalifanya idadi ya tembo kuongezeka kutoka 22,208 hadi kufika  70,406 mwaka 2006 na kwamba idadi hiyo ikashuka tena hadi 38,975 mwaka 2009 na hivi leo imezidi kupungua hadi kufika 13,084 katika ikolojia ya Selous-Mikumi.
Kuhusu Ikolojia ya Ruaha-Rungwa, Nyalando alisema sensa ya mwaka 1990 ilionesha kulikuwa na tembo 11,712 idadi ambayo ni ndogo kutokana na wimbi la ujangili  uliokuwepo miaka ya 1984 -1989.
Hata hivyo baada ya kuwepo kwa Operesheni Uhai, idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia tembo 35,461 mwaka 2006 lakini kwa matokeo ya mwaka huu idadi hiyo imepungua na wamebaki tembo 20,090.
Nyalandu alisema kupungua kwa tembo kunathibitishwa na idadi ya mizoga pamoja na tembo hai waliohesabiwa ambapo utafiti umebaini pia kwamba vyanzo vya vifo vya tembo wengi ni vya kuuawa na sio vya asili.
“Jumla ya mizoga 6,516 na 3,496 ilihesabiwa katika mifumo ya Ikolojia ya Selous-Mikumi na Ruaha-Rungwa, tumebaini vifo vingi sio vya asili”,alisema Nyalandu.
Aidha, alisema kukamatwa kwa  meno ya tembo yenye uzito wa kilogramu 32,987 ndani na nje ya nchi katika kipindi mwaka 2008 hadi Septemba 2013 kumedhihirisha kwamba ujangili ni sababu kubwa ya kupungua kwa idadi ya tembo.
Akizungumzia hali ilivyo katika Pori tengefu la Kilombero, Nyalandu alisema kuongezeka kwa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa na shoroba za wanyamapori kumechangia tembo kufa.
Alisema pori hilo ni sehemu ya Ikolojia ya Selous –Mikumi na kwamba mwaka 2002 pori hilo lilikuwa na tembo 2,080, lakini katika matokeo ya sensa hii pori hilo halina tembo hata mmoja.
Akizungumzia hatua ambazo Wizara imechukua Nyalandu alisema  ulinzi unazidi kuimarishwa wa wanyamapori kwa kushirikiana na vyombo  vya ulinzi na usalama pamoja na wadau na taasisi nyingine, ili kuhakikisha wanyama hao wanalindwa.
Kadhalika, Wizara iko kwenye hatua za mwisho za uanzishaji wa Mamlaka ya  Mpya ya Wanyamapori, pamoja na kupitia upya sheria  za uhifadhi, na kuangalia jinsi ya kuanzisha  mfumo wa kijeshi kwa watumishi wa sekta ya wanyamapori.
Utafiti huo ulifadhiliwa na Serikali na wadau mbalimbali kama vile Shirika la Misaada ya Kiufundi la Ujerumani(GIZ),UNDP na wahisani wengine ambapo jumla ya dola za Kimarekani 160,000 zilitumika.

No comments: