BEI MPYA YA UMEME KUANZA MAKALI LEO, GESI YA MAJUMBANI NAYO BEI JUU...

Nyaya za umeme.
Maumivu ya huduma ya umeme leo yanaanza kuwapata wananchi baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kulikubalia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupandisha bei ya nishati hiyo kwa zaidi ya asilimia 40.

Wakati bei hiyo ikipanda, bei ya gesi ya kupikia pia imepanda kuanzia leo kutoka Sh 54,000 hadi Sh 63,000 kwa mtungi wa kilo 15. Hali hiyo itafanya wananchi kupata maumivu ya maisha kuliko ilivyokuwa mwaka jana.
Wananchi wengi wamekuwa wakitumia gesi kupikia kutokana na gharama za umeme kupanda, lakini hatua hiyo kutafanya wananchi wengi kuendelea kupikia mkaa hata kuni ambako kunachangia kukatwa kwa misitu ovyo.
Kuanzia leo watumiaji umeme majumbani watanunua uniti moja kwa Sh 306 badala ya Sh 221 za awali.  Hao ni walioko katika kundi la T-1.
Kundi hilo linajumuisha wateja wanaotumia vifaa vya umeme kama majokofu, televisheni, kupiga pasi na  wafanyabiashara wadogo kama wasusi, vinyozi, maduka, mashine za kusagisha na biashara zingine ndogo zinazotumia umeme.
Hao ndio wateja wengi wa Tanesco ambao pia wameongezwa tozo ya huduma kwa mwezi, kutoka Sh 3,841 hadi Sh 5,520 kwa mwezi. Kiasi hicho mteja anakilipa bila kujali kama ametumia umeme au la kwa mwezi.
Licha ya gharama hizo, mteja atalipa gharama za Ewura ambazo ni asilimia moja na gharama za Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambazo ni asilimia tatu na Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) asilimia 18.
Mfano ni kwamba mtu ambaye anatoa Sh 40,000 kununua umeme, atakatwa tozo ya huduma Sh 5,520 na kubakiwa na Sh 34,480, atakatwa asilimia 3 ya REA ambayo ni Sh 1,034 (Ewura Sh 344.80), na kodi ya VAT asilimia 18  ambayo ni Sh 6,206.40
Kwa maana hiyo jumla ya gharama za mtu ambaye atatoa Sh 40,000 ni Sh 13,105.20 hivyo umeme atakaonunua ni wa Sh 26,894.80 ambazo atapata uniti 87.89 badala ya 127.62 alizokuwa anapata awali.
Kwa upande wa watumiaji wadogo wa majumbani ambao wamekuwa wanatumia kati ya uniti sifuri hadi 50 ambao wengi wao wanaishi vijijini watalazimika kununua uniti moja kwa Sh 100 badala ya Sh 60 za sasa. Katika kundi hilo, Ewura imeongeza wigo kuwa sasa kikomo cha watumiaji kitakuwa hadi wateja wanaotumia uniti 75 kutoka 50.
Katika kundi hilo ambalo linajulikana kama D-1 mtumiaji ambaye atavuka matumizi ya uniti 75 kwa mwezi atalazimika kununua uniti moja ya umeme kwa Sh 350 badala ya Sh 275 za awali. Katika kundi hili hakuna tozo ya huduma kwa mwezi.
Katika mchanganuo kundi la tatu ni T-2 ambako uniti moja ya umeme imepanda kutoka Sh 132 hadi Sh 205. Kundi hilo ni la wateja wenye matumizi ya kawaida ambao hupimwa kwa volti 400 na matumizi ya wastani ni zaidi ya uniti 7,500 kwa mwezi. Tozo ya kutoa huduma  kwa mwezi imebaki Sh 14,233.
Kundi la T-3-MV ambao ni wateja waliounganishwa katika msongo wa umeme wa kati, bei ya uniti ya umeme itauzwa kwa Sh 163 kutoka Sh 118. Tozo ya kutoa huduma bei yake nayo imepanda katika kundi hilo kutoka Sh 14,233 hadi Sh 16,769.
Wateja wakubwa ambao wameunganishwa katika msongo wa juu ikiwa ni pamoja na mashirika kama ZECO, Bulyanhulu na viwanda vya saruji kamaTwiga ambao wako kundi la T-3-H, watanunua uniti moja kwa kwa Sh 159 kutoka Sh 106 za awali. Kundi hilo halitozwi tozo ya huduma.
Gharama za kuunganisha  wateja  ndani ya meta 30 kwa mijini itakuwa Sh 272,000, vijijini Sh 150,000 na kwa mikoa ya Lindi na Mtwara itakuwa  Sh 99,000. Umbali usiozidi meta 70 ambayo mteja ataweka nguzo moja, bei kwa mijini ni Sh 436,964, vijijini Sh 286,220 na umbali usiozidi meta 120 mijini ni Sh 590,398 na vijijini itakuwa Sh 385,300. Ada ya maombi ni Sh 5,000.
Katika eneo la kufunga mita, gharama za kufunga Luku zilizoharibika au kuchezewa na wateja kwa wateja wa kundi la DI na TI bei kwa njia moja ni Sh 60,000, njia mbili Sh 200,000 na njia tatu ni Sh 300,000. Bei zote hizo zitadumu kwa miaka mitatu hadi mwaka 2016.
Mjumbe wa Bodi ya CTI, Samuel Nyantahe alisema kabla Tanesco haijapandisha gharama hizo ingekusanya madeni yote na kuziba mianya ya wizi wa umeme. “Kuna mambo tulizungumza na Tanesco kuhusu kukusanya madeni na kuwabana wakubwa wote wanaowadai.
“CTI hatujaridhika na hatua ya Tanesco kwanza wajue ongezeko hilo lina madhara katika viwanda … ili viwanda viweze kujiendesha itabidi vipunguze wafanyakazi na kupunguza uzalishaji,” alisema Nyantahe.
Mjumbe wa CCC, Thomas Mnunguli, alisema ongezeko hilo ni kubwa na linakosa uhalali hivyo Tanesco ijitathmini na kujipanga upya ilenge kutoa huduma bora na nafuu. “Badala ya kupandisha bei ya huduma kila kukicha kwa kudhani kuwa hakuna mbadala wa huduma zao,” alisema Mnunguli.
Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa ni pamoja na wizi wa umeme unaoelezwa kuchangia kulididimiza shirika hilo na madeni makubwa ya wateja zikiwamo taasisi za Serikali.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema Ewura wamepandisha bei baada ya kubaini kwamba hali ya kifedha ya Tanesco si nzuri, kwani shirika limeendelea kupata hasara ambayo iliongezeka kutoka Sh bilioni 47.3 mwaka 2010 hadi Sh bilioni 223.4 mwishoni mwa mwaka juzi.
Alisema pamoja na upungufu kiufanisi, sababu kubwa ya ongezeko ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji umeme ambao Tanesco inanunua kutoka kwa wazalishaji binafsi. Mara ya mwisho kwa Tanesco kupandisha gharama za umeme ni Januari mwaka juzi.
Licha ya kupandisha bei hizo Tanzania bado inaonekana bei ziko chini ikilinganishwa na nchi zingine za Afrika Mashariki. Mfano kwa wateja wa majumbani Tanzania ni senti 0.19 za dola wakati nchi zingine ni senti 0.20.

No comments: