ATISHIA KUJITUPA KUTOKA JUU YA MNARA KUSHINIKIZA AONANE NA RAIS KIKWETE...

Jamaa huyo kama anavyoonekana katika picha mbalimbali wakati wa tukio hilo.
Mkazi wa Kipera mkoani Morogoro, Hassan Kibwana jana alifunga mwaka kwa mtindo wa aina yake, baada ya kupanda juu ya mnara wa simu na kutishia kujirusha chini, akishinikiza kutaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili afikishe madai aliyonayo.

Tukio hilo lililodumu  kuanzia saa 5.10 hadi saa 6.50 mchana,  lilitokea eneo la Ubungo ndani ya eneo la Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ulipo mnara huo na kusababisha mamia ya wananchi kuacha shughuli ili kushuhudia kioja hicho.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi inayolinda eneo la TBS, ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema awali mtu huyo alionekana akirandaranda katika eneo hilo huku akiwa na ngazi yake fupi mkononi.
Alisema ghafla alimuona mtu huyo akiweka ngazi hiyo pembeni ya uzio, uliozunguka nguzo hiyo na kuanza kupanda, ambapo hata hivyo alifanikiwa kumfukuza.
“Lakini wakati naendelea na shughuli zingine ghafla alipanda ngazi kwa haraka na kurukia ndani ya uzio na kuanza kupanda mnara huo kwa kasi huku tukimpigia kelele za bila mafanikio tukimtaka ashuke,” alisema mlinzi huyo.
Hatua hiyo ilisababisha wananchi walioko eneo hilo, wakiwemo wasafiri waliokuwemo ndani ya mabasi, kupigwa na butwaa, kutokana na kitendo cha mtu huyo huku baadhi wakionekana kuwa na hofu ya pengine mtu huyo angetimiza ahadi yake ya kujirusha, kama mamlaka za usalama, zingechelewa kufika eneo hilo.
Hata hivyo, askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Halmashauri la Jiji la Dar es Salaam, wakiwa na gari Namba SM 9484 walifika katika eneo hilo na kupanda juu ya mnara huo na kufanikiwa kumshusha chini huku akiwa amefungwa kamba mikononi na kumwingiza katika gari la Polisi  na baadaye gari hilo, kuondoka naye katika eneo hilo .
Iliwalazimu askari hao wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, kutumia nguvu za ziada ili kumdhibiti mtu huyo, aliyeamua kuanzisha mapambano dhidi ya askari hao huku akiwa juu ya mnara huo kabla ya kuzidiwa nguvu na kushushwa.
Akielezea sababu za kufanya tukio hilo, Kibwana alisema kusudi la yeye kupanda juu ya mnara huo ni kumtaka Rais Kikwete afike hapo ili aweze kusikia kilio chake.
“Polisi walinisingizia kesi ya kuua na kusababisha nifungwe jela miaka sita huko Morogoro, nimekwenda kumuona Mkuu wa Mkoa Kalembo hajanipa msaada wowote zaidi ya kunitaka nifikishe malalamiko yangu kwa Rais, sasa mtu kama mimi ningewezaje kumuona Rais, ndiyo maana nimeamua kufanya hivi ili aje,” alisema Kibwana.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alithibitisha kuwepo tukio hilo. Alisema  wanaendelea kumhoji mtu huyo na baadaye watamfikisha mahakamani, kujibu tuhuma za kupanda juu ya mnara huo na kutishia kujiua.

No comments: