Kabwe Zitto katika moja ya mikutano yake Kigoma. |
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye eneo la Mwandiga, ambako ni nyumbani kwao na ngome yake kuu, Zitto alisema kuwa kinachotokea sasa ndani ya Chadema ni viongozi kutokubali demokrasia na uwajibikaji kutawala ndani ya chama hicho.
Alisema siyo usaliti hata kidogo kwa yeye kama mwanachama au mtu wa Kigoma kuwa na nia ya kugombea Uenyekiti wa Chama na kwamba woga wa viongozi kutotaka kuruhusu demokrasia kutawala, imesababisha chama hicho kuendeshwa kidikteta.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alisema kuwa kama Mwenyekiti wa kamati ya hesabu za serikali, anasimamia uwajibikaji wa viongozi kwa fedha za umma, jambo ambalo baadhi ya viongozi wa chama chake wanatafsiri kwamba ni usaliti.
Zitto alisema hata vurugu na kuvuana madaraka vinavyotokea sasa ndani ya chama hicho ni kutoaminiana kwa viongozi na kwamba hata mashitaka aliyovuliwa madaraka siyo ambayo anatuhumiwa nayo.
Alisema kuwa kupitia vikao halali vya chama ambavyo vinajumuisha wenyeviti wa mikoa na wilaya wa chama hicho atapigania haki yake ya kuhukumiwa bila kupewa nafasi ya kujieleza wala kusikilizwa.
Alisema kuwa licha ya jitihada zitakazofanyika za kupigania haki yake nahatimaye kuvuliwa ubunge kutokana na jitihada za kumvua uanachama zinazoendelea alisema kuwa hatima yake ya kisiasa itakuwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma ambao wataamua nini afanye kwa wakati huo.
Alisema kuwa wakati wa kikao cha kamati kuu alihojiwa kuhusu kauli zake kuhusiana na taarifa za fedha za ruzuku za chama hicho lakini anashangaa kwamba katika mashitaka 11 aliyopewa kwa maandishi kuwasilisha maelezo yake, yote yanahusiana na kwa nini anataka kugombea uenyekiti wa chama.
Mbunge huyo alisema kuwa kwa sasa liko kundi ndani ya Chadema ambalo hata lifanye nini halitaguswi kwa kwenda kinyume na chama, lakini wapo baadhi ya wanachama na viongozi ambao tuhuma ndogo kwao inakuwa ni ejenda kubwa ya chama.
“Yote yanayotokea ni mchakato wa kuimarisha demokrasi ndani na nje ya chama chake, jambo ambalo baadhi ya viongozi wenzangu hawataki kukubaliana nalo, tutapigania hilo hadi mwisho wake kuhakikisha demokrasia na uwajibikaji vinatawala na kuleta mabadiliko katika nchi.”
Zitto amezungumzia ziara zinazofanywa na viongozi wa chama hicho maeneo mbalimbali nchi na kusema kuwa maneno yanayozungumzwa na viongozi hao tayari yametoa hukumu kwake kuhusu sakata linaloendelea ndani ya chama hicho.
Amewaomba wananchi, wanachama na wapenzi wa Chadema ambao wanamuunga mkono kuwa na subira wakati wakiwa kwenye mapambano makubwa ya kutafuta haki kwa njia ya demokrasia.
Awali Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Jafari Kasisiko alisema kuwa viongozi wa chama hicho mkoani humo wako tayari kupambana kwa namna yoyote kupitia vikao vya chama hicho kuhakikisha Zitto Kabwe anarudishiwa nyadhifa zake alizovuliwa.
Kasisiko alisema kikao cha baraza kuu ambacho hujumuisha viongozi mbalimbali wa wilaya na mikoa kitatoa hatima ya kisiasa ya mbunge huyo kuhusiana na mgogoro wa kuvuana uongozi zinazoendelea ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, alisema kuwa kama itatokea Zitto kuvuliwa uanachama ndani ya Chadema viongozi hao wa mkoa na wananchi kwa jumla watakuwa pamoja naye kuona hatua gani ambazo zinaweza kufuata kwa wakati huo.
Awali alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma msafara wa mbunge huyo ulitanguliwa na msafara mrefu wa waendesha pikipiki maarufu kama boda boda, midundiko na watembea kwa miguu katika msafara ambao unaelezwa kuwa hakuna kiongozi aliyewahi kuwa na msafara mrefu kama huo.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa mapokezi hayoyamevunja rekodi aliyoweka mwaka 2006 aliporejea mkoani humo kutoka bungeni Dodoma ambako aliibua sakata la Buzwagi.
No comments:
Post a Comment