WAZIRI MUHONGO AMSHUKIA REGINALD MENGI KUHUSU UMILIKI WA VITALU...

Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) na Reginald Mengi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema baadhi ya wazalendo nchini wanamiliki vitalu kwa asilimia 70 lakini baadhi yao wanashindwa kuendeleza maeneo na kusisitiza kwamba si kweli kuwa vingi vinamilikiwa na wageni nchini.

Muhongo alikuwa akijibu jana hoja za wabunge wakati akichangia taarifa  ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. 
Alitaja baadhi ya wanaomiliki vitalu kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi akisema anamiliki kampuni tano zenye ukubwa wa kilometa 3,888.18. 
Wengine ni Al Hussein Danan, kampuni 19 na vitalu vyenye ukubwa wa kilometa 25,589 na Hassan Abdul kampuni 19 na vitalu vyenye ukubwa wa kilometa 14,238. 
Akizungumzia hoja hiyo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mengi alisema anamiliki kwa ubia na Watanzania wenzake mgodi mmoja tu wa uchimbaji madini ya tanzanite wenye eneo lisilofikia hata kilometa moja ya mraba.
“Profesa Muhongo hajakanusha hili, badala yake anaturudisha Watanzania kule kule kwenye maeneo ya utafutaji badala ya migodi,” alisema.
Kuhusu takwimu za eneo analomiliki, Mengi alisema eneo ambalo limeshatolewa kwa ajili ya mafuta na gesi lina ukubwa wa kilometa za mraba 243,000 ambalo ni sawa na karibu robo ya eneo la Tanzania nzima au mara 175 ya eneo la mkoa wa Dar es Salaam au eneo la mikoa tisa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Shinyanga na Kagera.
“Katika suala la gesi mimi sipiganii mambo yangu binafsi, kwa sababu mimi nimeshafanikiwa kibiashara. Ninachopigania ni Watanzania wenzangu nao wapate fursa. Naomba nieleweke, kwamba ninaposema Watanzania nina maana kuanzia mfanyabiashara mdogo wa sekta isiyo rasmi, mfanyabiashara wa kati na wafanyabiashara wakubwa.
“Nataka kuwepo sera ambayo itahakikisha wanawezeshwa na si kusema tu kwamba hawawezi. Nafanya hivyo kwa sababu ninaamini utajiri uliobarikiwa ni ule uliopatikana kwa njia halali na unatumika kusaidia wanaohitaji msaada,” alisema.
Katika kuonesha kuwa anakerwa na kauli ya Waziri, Mengi alisema: “Ni wazi kwamba Profesa Muhongo ana chuki binafsi na mimi.
Hii ni utashi wake, si lazima anipende na mimi si lazima nimpende. Lakini suala la gesi ni kubwa mno kuliko uhusiano kati ya Profesa Muhongo na mimi.
“Linagusa kila Mtanzania wa leo na wa vizazi vijavyo. Kwa hiyo napenda kumsihi ndugu yangu, Profesa Muhongo aache kuchanganya chuki binafsi kwenye suala la gesi,” alisema Mengi.

No comments: