![]() |
| Nyumba ya Mzee Mandela kijijini kwake, Qunu ambako anatarajiwa kuzikwa. |
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Collins Chabane, alisema jana kuwa viongozi wa mataifa mbalimbali, wameshauriwa kupitia balozi zao kuhusu ufinyu wa eneo hilo la Qunu, ili kuwapa fursa ya kuchagua siku, ambayo wangependa kushiriki katika msiba huo.
Tangu juzi balozi nyingi zilikuwa zikisubiri taarifa ya mwisho kuhusu utaratibu wa maziko, kabla hazifanya mipango ya viongozi wa mataifa yao kuwasili nchini hapa kushiriki maziko hayo ya kihistoria.
“Hatumzuii mtu yeyote kwenda Qunu kwa sababu kwa desturi za Kiafrika huwezi kumzuia mtu kwenda kushiriki maziko," alisema mwanadiplomasia mmoja aliyekuwa katika mkutano huo na waandishi wa habari.
Mwanadiplomasia huyo alionya pia kuwa hata eneo la Uwanja wa Ndege wa Mthatha ulio kijijini hapo ni dogo, hali ambayo inaweza kuleta kizazaa wakati ndege za viongozi hao zitakapokwenda kutua.
Kutokana na udogo huo, Mwanadiplomasia huyo alisema watashauri kampuni za ndege, kuhakikisha kuwa ndege zao haziegeshwi katika uwanja huo wa Mthatha ili kuepuka msongamano.
Tutawataka wakishusha abiria, waondoke na kwenda kuegesha ndege hizo katika viwanja vya East London au kile cha Port Elizabeth.
Eneo hilo la mji, pia linaelezwa kuwa lina hoteli chache na huduma zingine za muhimu upatikanaji wake sio mkubwa.
Katika mkutano huo, Chibane aliwaambia waandishi wa habari kwamba Wizara ya Mambo ya Nje, bado inashughulika na namna viongozi wa mataifa mbalimbali watakavyoshiriki katika ibada ya kitaifa, kesho Jumanne na siku ya maziko ambayo yatafanyika Jumapili huko Qunu.
Chama cha ANC kimetangaza mapema wiki hii, kuwa kutakuwa na matukio 54 ya maombolezo ya kifo cha Mandela katika maeneo mbalimbali nchini ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kutoa heshima za mwisho.
Chabane alisema Serikali itaimarisha ulinzi katika siku zote za maombolezo ili kuhakikisha shughuli za msiba huo, zinafanywa katika usalama mkubwa.
“Ni lazima tuwe na wasiwasi, lakini kwetu sisi hii haimaanishi kuwepo kwa changamoto yoyote ile kubwa," alisema Chabane na kuongeza; "hatutalala usiku."
Viongozi wengi duniani wanatarajia kumiminika Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki katika kuuaga mwili wa Nelson Mandela, isipokuwa Dalai Lama.
Shughuli mbalimbali za msiba huo, zinaendeshwa na Serikali. Kwa sasa Serikali bado inaendelea na mipango kwa ajili ya huduma ya ibada ya kitaifa, ambayo itaendeshwa katika Uwanja wa FNB ulioko Johannesburg.
Wananchi wameshauriwa kujipanga pembeni ya barabara, ambazo mwili wa marehemu utapitishwa wakati ukitokea katika Hospitali ya kijeshi ya Pretoria kwenda katika majengo ya Muungano yaliyoko huko Pretoria.
Mwili wa Rais huyo wa zamani utawekwa kwa siku tatu katika majengo hayo, ambako wananchi watapewa fursa ya kutoa heshima za mwisho. Siku ya kwanza itakuwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi wa mataifa mbalimbali.
Siku ya maziko itakuwa Desemba 15 Qunu na yatahudhuriwa na watu wachache walio karibu naye na mamilioni ya watu ulimwenguni kote, kama sio watu zaidi ya bilioni moja, wanatarajiwa kushuhudia kupitia matangazo yatakayorushwa moja kwa moja katika luninga.
Kwa mujibu wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, katika siku hizo 10 za maombolezo, kutakuwa na dhifa za kitamaduni kutoka jamii ya Thembu ya ukoo wa Mandela, na hakutakuwa na matukio ya umma yatakayofanyika mpaka siku tano zipite tangu kifo chake.
Jana katika Kanisa la Methodist Johannesburg, kulikuwa na ibada maalumu ya kumuombea na kumkumbuka Mandela, ambapo watoto walibatizwa na nyimbo mbalimbali za kumsifu Mungu, ziliimbwa kwa mahadhi ya Kiafrika Kusini na waombolezaji waliimba huku wakicheza.
Akizungumza katika ibada hiyo, Rais Zuma alimsifu Mandela na kuwataka Waafrika Kusini wasisahau mafundisho yake. “Maombi haya yatasaidia kuponya taifa letu,” alisema.
Mtaliki wa Mandela, Winnie Madikizela-Mandela, alihudhuria ibada hiyo wakiwemo wanasiasa kutoka chama kipya cha Economic Freedom Fighters.
Misa nyingine ilitarajiwa kuanza jana jioni katika Kituo cha Kumbukumbu cha Nelson , Johannesburg, ambako aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, alitarajiwa kushiriki.
Katika misa iliyofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Ngangelizwe Rotary, Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe alisema watu hawapaswi tu kuomboleza, bali wanapaswa pia kusherehekea maisha yake.
"Tunapaswa pia kusherehekea kuliko kuomboleza kwa kuwa aliishi maisha yaliyojitosheleza…alituongoza kufika katika mji wa ahadi,” alisema.
Kesho kutakuwa na huduma ya kumbukumbu ya kitaifa, kumuenzi itakayofanyika kwenye Uwanja wa FNB, ambao pia unajulikana kama Soccer City katika Mji wa Soweto, ambayo itahudhuriwa na maelfu ya watu.
Uwanja wa FNB ni mahali ambapo Mandela alionekana mara ya mwisho kwa umma wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, wakati huo kukiwa na shaka kuwa huenda asingeweza kuhudhuria kutokana na matatizo ya afya yake.
Kati ya Desemba 11 na 13, mwili wa Mandela utawekwa katika majengo ya Muungano huko Pretoria kwa siku tatu, sehemu ambayo aliapishwa kama Rais wa kwanza baada ya utawala wa ubaguzi wa rangi Mei 10 mwaka 1994.
Siku ya kwanza itatumika na viongozi kuaga mwili, wakati umma utaruhusiwa kupita kwenye jeneza nyakati za mchana kwa siku mbili zilizobaki.
Siku ya tisa baada ya kifo chake, ndege ya jeshi itaondoka Pretoria na kuelekea Kusini mwa Mthatha, mji maalum Mashariki wa Cape Province.
Wazee wa Thembu na wanafamilia ya Mandela wataaga mwili kwa kupita kwenye jeneza la Mandela, wakati mamia ya waombolezaji wataaga kwa kujipanga kwenye mitaa kutoka uwanja wa ndege wa Mthatha na kushuhudia jeneza likisafirishwa na gari la jeshi hadi katika Kijiji cha Qunu, mahali ambapo kiongozi huyo alikulia tangu utoto wake.
Mwili utakapofikishwa kwenye nyumba ya Mandela, jeshi hilo litaacha majukumu yaliyobakia kwa familia.
Bendera ya Afrika Kusini itaondolewa kwenye jeneza na kuwekwa blangeti la kijadi la Xhosa, ikiwa ni ishara ya kurudi nyumbani.
Nyakati za jioni, kiongozi wa ANC, viongozi wa machifu na familia ya Mandela wanatarajia kukusanyika kwa ajili ya mkesha binafsi kabla ya maziko siku inayofuata (Desemba 15).
Shughuli za maziko zitafanyika Qunu nyumbani kwa Mandela, ambako maelfu ya watu, pamoja na marais wa nchi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika maziko hayo yatakayofanyika chini ya hema kubwa, lililotengenezwa kwenye vilima eneo ambalo Mandela alikuwa akikimbia na kucheza akiwa mtoto.
Shughuli za maziko zitaoneshwa moja kwa moja na kushuhudiwa na mamilioni ya watu duniani kote.
Saa sita mchana mwili wa Mandela utahifadhiwa kwenye udongo wa miamba katika ardhi aliyotoka, eneo ambalo liliandaliwa na baadhi ya wanafamilia wakiwemo wanawe, walizikwa hapo.
Maziko hayo yatahudhuriwa na mamia ya watu walio karibu na familia na yatafuata taratibu za mila na desturi zao.

No comments:
Post a Comment