PINDA ATANGAZA VITA NA WALAFI SERIKALINI, 866 WASHUGHULIKIWA...

Mizengo Pinda.
Watumishi 866 wa serikali wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika halmashauri mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akisoma hotuba ya kuahirisha shughuli za Mkutano wa 14 wa Bunge lililofanyika mjini hapa.
Pinda alisema watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za umma wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi, kushushwa vyeo na kufikishwa mahakamani.
Aidha, alisema kesi za watumishi hao ziko katika mahakama na vyombo vya nidhamu vya Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao.
Alisema kutokana na hali hiyo, kati ya mwaka 2011/12 hadi Septemba, mwaka huu jumla ya wakurugenzi 52, wakuu wa idara 65 na watumishi wengine 746 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika halmashauri mbalimbali nchini.
“Waliofukuzwa kazi ni 232, waliosimamishwa 186, waliovuliwa madaraka 33, waliopunguziwa mshahara ni mmoja , walioshushwa cheo 32, waliopewa onyo 113, waliofikishwa mahakamani 233 na waliofikishwa polisi na TAKUKURU 36.
“Serikali itaendelea kuhimiza nidhamu katika matumizi ya kifedha na vilevile itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watumishi wote watakaokuwa wabadhirifu,” alisema.
Aidha, alisema pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa watumishi hao mmoja mmoja, serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana na tatizo la ubadhirifu wa mali za umma katika halmashauri.
Pinda alizitaja hatua za kukabiliana na ubadhirifu huo kuwa ni kuongeza uwezo kwa kuajiri wahasibu wa kutosha katika halmashauri, kuanzisha kamati za mapato na matumizi katika ngazi zote za halmashauri, kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa kamati za mapato na matumizi za halmashauri zote na kufanya ukaguzi maalumu kubaini ufisadi na ubadhirifu wowote uliojitokeza.
Alitoa mfano katika mwaka wa fedha 2011/12 ulifanyika ukaguzi maalumu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 14 ambazo ni Kilindi, Kiteto, Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda.
Hali ya chakulaAkizungumzia hali ya chakula nchini alisema tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, mwaka huu  katika maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula na lishe inaonesha  watu 828,063 wanakabiliwa na upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi Februari 2014.
Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya tani 16,119 za chakula cha mgawo kwa Halmashauri zenye mahitaji ya chakula cha msaada.
Waziri Mkuu alisema hadi kufikia  Desemba 16 mwaka huu, tani 13,716 zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika huku  Tani 2,402 zilikuwa hazijachukuliwa na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na Manyoni.
“Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua chakula hicho kufanya hivyo kabla ya  Januari 15, mwakani na ambao hawatatekeleza maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Aliwahakikishia wananchi pia kuwa serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.
Pinda alieleza mwenendo wa bei za vyakula nchini kutokana na miezi hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua.
“Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika soko hapa nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi kikubwa.
Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Sh 536.86 kwa kilo mwezi Oktoba, mwaka huu  hadi kufikia Sh 538.26 kwa kilo mwezi Novemba, mwaka huu,” alisema.
Kwa upande wa mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Sh 1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, mwaka huu  hadi Sh  1,191.10 kwa kilo mwezi Novemba, mwaka huu na kuongeza kuwa pamoja na hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa na zile za kipindi kama hicho mwaka jana.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha  kwa  mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu,” alisema.
Alisema  halmashauri zihakikishe kuwa zinadhibiti ununuzi holela wa chakula kutoka mashambani na majumbani mwa wakulima kwa lengo la kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha.
Operesheni TokomezaKuhusu Operesheni Tokomeza alisema  matatizo yaliyochunguzwa kuhusiana na operesheni hiyo ni pamoja na mateso dhidi ya watuhumiwa, matumizi mabaya ya silaha, uchomaji wa nyumba za wananchi na kuua mifugo kikatili.
Pinda alisema  taarifa ya Kamati ilitoa mapendekezo mbalimbali, waheshimwa wabunge walipata fursa ya kuchangia na kutoa ushauri kwa serikali.
“Napenda kukubaliana na kamati na waheshimiwa wabunge kwa ujumla kuwa pamoja na nia nzuri ya operesheni hiyo, utekelezaji na usimamizi wake ulikuwa na kasoro kubwa,” alisema.
Alisema serikali imesikia na ndio maana mawaziri wanne wameona ni vyema kujiuzulu ili kulinda heshima na imani ya wananchi kwa serikali yao. 
Mawaziri hao ni  Shamsi Vuai Nohodha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Emmanuel J. Nchimbi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk David Mathayo David, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na  Balozi Khamisi S. Kagasheki  Waziri wa Maliasili na Utali ambapo Rais ameridhia kujiuzulu kwao.
“Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru waheshimiwa mawaziri hao kwa ujasiri wao na kwa kutambua dhamana yao, nawatakia kila la heri katika shughuli zao za ubunge na nyingine kadri watakavyojaliwa,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya kamati na ya bunge kwa ujumla kuhusiana na yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza.
Pinda aliahirisha Bunge hilo hadi Mei 6 mwakani, litakapokutana tena katika mkutano wa 15 wa bajeti.

No comments: