Jeneza lenye mwili wa Mzee Nelson Mandela wakati wa heshima za mwisho kijijini Qunu. |
Baada ya matangazo yaliyokuwa yakirushwa moja kwa moja na televisheni duniani kukatika pale jeneza liliposhushwa kaburini, hakuna kilichoendelea zaidi ya kuachiwa familia na ndugu wa karibu kukamilisha maziko.
Kilichoendelea ni masuala ya kimila ambayo hufanywa faragha na hivyo watu wasiokuwa wanafamilia na pengine wa ukoo wa Mandela na kabila la Waxhosa, kushindwa kujua kilichojiri baada ya hapo.
Hali hiyo ilizua hisia tofauti ampapo wengine waliamini kwamba mwili wa Mandela uliondolewa kwenye jeneza na kuzikwa huku wengine wakiamini kinyume chake.
Kwa kuwa Mandela alikuwa wa kabila la Waxhosa, kuna mambo yalifanyika kwa imani za kabila hilo siku ya maziko, kwa kuzingatia pia kuwa alikuwa kiongozi katika kabila hilo.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa utamaduni wa Kixhosa, Somadoda Fikeni, katika utamaduni huo, mtu kama Mandela anapofia nje ya nyumbani kwao kwa asili, matambiko hufanywa kama ishara ya kurejesha roho nyumbani kwa wahenga.
Fikeni alisema inaaminika, kwamba roho ya mtu huhitaji kurudi nyumbani na kuunganika na wahenga wakati wa maziko kwa lengo la kurejesha utulivu wa kiroho katika jamii.
Kutokamilishwa kwa utaratibu huo kunaweza kusababisha roho hiyo kuhangaika katika familia bila kupumzika na kusababisha maafa kwa wanafamilia kama ishara ya kuonesha kutoridhika kwake.
Kama matambiko haya yatafanyika, inaaminika kwamba itakuwa ni faraja kwa Muumba na wahenga ambao ni kiunganishi cha Muumba na walio hai na hivyo kuleta bahati na ulinzi kwa familia.
Iwapo hatua moja katika utaratibu huo itarukwa, basi matambiko mengine ya kujisahihisha na kuwatuliza wahenga na Muumba yatafanyika.
Wakati mabaki ya mwili yakiwa yanarejeshwa nyumbani, kiongozi au mtaalamu huchaguliwa kufanya matambiko ambayo ni lazima katika kuomba kurejea kwa roho.
Hii miongoni mwa mambo mengine, inahusisha kuzungumza na mwili, kumaanisha kuwa safari ya kurudi eneo ulikozaliwa na eneo ambako kitovu kilizikwa imeanza.
Dawa maalumu za kienyeji wakati mwingine hutumika kwenye mchakato huo. Roho inaongozwa nyumbani hapo kwa kutajwa majina ya mito na maeneo ulikopita.
Hiyo pia huhusisha kukaribisha izibongo (nyimbo za pongezi za familia au kundi la rika fulani) na kutaja majina ya wahenga waliotangulia mbele za haki ambao marehemu atakwenda kukutana nao.
Mwili unapowasili, roho hufahamishwa juu ya kuwasili huko na kuahidi kusaidia katika upatanishi na Muumba na kuhimiza wahenga katika kazi hii ya kulinda familia na Taifa.
Kuhusu maziko yenyewe, ng’ombe anachinjwa na watu maalumu walioteuliwa ambao hutumia mkuki wa jadi wa familia au ukoo.
Muda baada ya mtu kuwa ameondoka, matambiko ya jadi mara nyingi huhusisha kukaribisha roho ya marehemu kama mhenga kufanya makubaliano kati ya walio hai na Muumba.”
Kama ng’ombe, dume au fahali atachinjwa na kutoa mlio wa mngurumo, hiyo huchukuliwa kama alama ya wahenga kufarijika na kumpokea marehemu.
Katika baadhi ya matukio, mnyama mwingine atachinjwa badala ya wa awali endapo atakuwa ameshindwa kutoa mlio unaotakiwa.
Kama marehemu atakuwa anatoka familia ya kifalme au atakuwa ni chifu au mfalme, matambiko haya yatakuwa hayana tatizo.
Mathalan, jeneza litafunikwa ngozi ya chui kama marehemu alikuwa chifu-kama Madiba- na litafunikwa ngozi ya simba kama alikuwa mfalme.
Viongozi wa kimila au kifalme, watajipanga karibu na jeneza wakati maziko yakifanyika.Kwa wakati mwafaka, mtambaji anayejua historia ya marehemu atamtambulisha kwa kutaja majina ya kimila na kuelezea tabia yake.
Katika maeneo ambako mila zinafutwa kikamilifu, mwili mwa marehemu, hususan kiongozi wa kimila, utafunikwa kwa ngozi ya mnyama.
Ngozi ya ng’ombe hutumika-mara nyingi ni yule anayekuwa amechinjwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
Marehemu huzikwa na baadhi ya mali zake muhimu na vitu walivyovipenda na kuvitumia wakati wa uhai wao.
Mikuki, ngao na tumbaku vilikuwa baadhi ya vitu vilivyotumika enzi za zamani. Baadhi wanazikwa wamekaa na wengine wamelala.
Pia baadhi ya matambiko huhusisha utoaji sadaka za kijadi kwa wahenga ikiwa ni pamoja na vinywaji wakati wa maziko ambapo humwagwa juu ya kaburi.
Matambiko hayo hufanywa kwa lengo la kuhakikisha roho inarejeshwa kwenye mwili na kurejeshwa katika nyumba ya wahenga, kwa ajili ya utulivu wa kiroho.
Mvua ikitangulia kunyesha kabla ya siku ya maziko au siku yenyewe, ni dalili njema, kwamba mbingu na dunia ya kiroho inamkaribisha marehemu.
Wakati wa mazishi, kondoo au mbuzi huchinjwa, na dawa za kimila hutumika ili kutakasa familia za marehemu na kuomba ulinzi ambapo hufanywa asubuhi ya siku ya maziko na wiki moja baadaye.
Tukio hilo pia hutumika kutoa hotuba za wazee na wanafamilia waandamizi ambao huwapa nguvu wengine kwa maneno ya faraja na busara wakati wakiwambukusha majukumu yao, wazee na watoto, kwamba itakuwa muhimu kwa familia kuendelea kudumu.
Pia ni wakati ambao maelezo muhimu hutolewa ya jinsi familia itakavyoendelea kuomboleza. Mara nyingi waombolezaji hawatashiriki shughuli za kijamii kwa kipindi chote.
Baadhi ya familia za Waxhosa zitavaa mavazi meusi kwa kipindi chote na yatachomwa moto baada ya maombolezo kumalizika.
Katika baadhi ya familia, wajane wakati wa kipindi hicho hawapiki-atakuwapo mtu mwingine wa kufanya kazi hiyo kwa niaba yao.
Baada ya miezi sita au mwaka, maombolezo humalizika kwa sherehe nyingine ambapo familia na marafiki hupeleka zawadi kwa mjane (wajane) au watoto kuchukua nafasi ya vitu vilivyochakaa, ambavyo yawezekana vikahusishwa na marehemu, mathalan kitanda au mablanketi.
Wakati huo, msisitizo pia huwekwa kwenye uhuru, kwamba mwombolezaji atarejea kwenye furaha tena lakini kwa staha na heshima kwa ajili ya kuheshimu marehemu na familia.
Baada ya muda mrefu wa kumalizika maombolezo, matambiko ya familia yatahusika na kurejesha roho ya marehemu kama mhenga kwa ajili ya kuwasiliana na walio hai na muumba wao.
Heshima kama hiyo hutolewa kwa watu waliojipambanua wenyewe au walikuwa na umuhimu mkubwa wakati wa uhai wao.
Hapana shaka kwamba Madiba atakuja kuwa mhenga kama hao, akiendelea kutoa uongozi na ulinzi kwa familia aliyoacha.
No comments:
Post a Comment