NDEGE YA ETHIOPIA YATUA KWA DHARURA ARUSHA BAADA YA KUPOTOSHWA...

Ndege hiyo baada ya ajali mapema leo. Picha ndogo ni gurudumu la ndege hiyo likiwa limejikita ardhini.
Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia,  imetua kwa dharura katika uwanja mdogo wa Arusha baada ya kushindwa kutua katika uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kutokana na ndege nyingine ya TFC kukwama kwenye njia ya kurukia.
Aidha, ndege hiyo ya Ethiopia aina ya Boeing 767 namba ET- AQW iliyokuwa ikitoka Ethiopia ili kutua KIA na iliwasiliana na waongoza ndege wa KIA waliotoa maelekezo ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, lakini rubani huyo alishindwa kufika Nairobi na kulazimika kutafuta uwanja mwingine wa karibu ndipo alipotua uwanja mdogo wa Arusha.
Hata hivyo, ndege hiyo iliyotua saa 6 mchana uwanjani hapo, ilititia kwenye tope wakati rubani akijaribu kukata kona katika uwanja huo mdogo ambao hauruhusu kutua ndege kubwa.
Hali hiyo ilizua taharuki kwa wafanyakazi wa kiwanja hicho na abiria waliokuwa wakisubiri ndege zingine  kwenda sehemu mbalimbali  za utalii na safari za kawaida.
Baada ya kutua salama, abiria wa ndege hiyo zaidi ya 213 na wafanyakazi  23 waligoma kushuka kwa kutumia ngazi za kiwanjani hapo na kukaa ndani ya ndege kwa karibu saa tano wakisubiri ngazi kubwa kutoka KIA.
Kugoma kushuka kwenye ndege hiyo kulisababisha baadhi ya wafanyakazi wa ndege hiyo kufungua milango ya dharura ili abiria wapate hewa.
Kwa  mujibu wa wafanyakazi wa uwanja huo wa Arusha, ndege hiyo ililazimika kutua hapo kutokana na kuishiwa mafuta.
Mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakutaka jina lake liandike gazetini kwa madai ya kuwa si msemaji, alisema haijawahi kutokea ndege kubwa kama hiyo kutua uwanjani hapo salama, lakini kwa kuwa ni kubwa ilikwama kwenye tope na kusababisha hofu kubwa ila vyombo vya usalama vilikuwapo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ambaye alifika eneo la tukio alisema tukio hilo halijapata kutokea lakini akasisitiza kuwa kuna haja ya kuboresha uwanja huo  ili hata zinapotokea dharura zishughulikiwe kwa wakati.
“Rubani aliona uwanja akasema, waongoza ndege wa Kenya wakamwambia atue, kumbe ulikuwa ni uwanja mdogo wa Arusha, hivyo ni vema sasa uwanja huu ukaboreshwa,” alisema.
Baada ya dharura hiyo ambayo haikuwa na majeruhi, baadhi ya ndege ndogo  zilishindwa kuruka  tangu saa  sita mchana na ilipofika saa tisa alasiri ziliruhusiwa  huku ulinzi ukiimarishwa.
Baadhi ya mashuhuda wa Arusha na viunga vyake walisema haijawahi kutokea ndege kubwa kama hiyo kuruka chini chini huku kukiwa na mngurumo mkubwa,  hali iliyosababisha taharuki.

No comments: