MICHAEL SCHUMACHER MAHUTUTI BAADA YA KUBAMIZA KICHWA KWENYE JABALI...

KUSHOTO: Schumacher alipokuwa akitamba kwenye Formula One. KULIA: Akiserereka kwenye barafu.
Bingwa wa zamani wa mbio za magari za Formula One, Michael Schumacher yuko hoi mahututi hospitalini baada ya kuanguka na kujibamiza kwenye mwamba wakati akicheza mchezo wa kuserereka kwenye barafu akiwa na mtoto wake wa kiume.

Bingwa wa upasuaji alionekana akiwasili kwenye hospitali hiyo huko Grenoble, nchini Ufaransa, ambako dereva huyo wa zamani wa Formula One alikokuwa akipatiwa matibabu.
Familia yake pia ilikuwapo hospitalini hapo, ambako vyazno vya kitabibu vilithibitisha Schumacher alikuwa katika 'hali mbaya' na alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya ubongo.
Mashuhuda walisema Schumacher alipoteza fahamu mara baada ya kuanguka na kubamiza kichwa chake kwenye mwamba.
Waliona damu ikichuruzika kutoka kwenye kofia yake ngumu ya helmet kwa kipindi cha dakika nane za kuanguka hadi walipowasili madaktari kwa helikopta kumchukua.
Ajali hiyo ilitokea wakati Schumacher alipokuwa akiserereka kwenye barafu nje ya eneo maalumu. Juzi msemaji mmoja wa sehemu hiyo alisema ilithibitisha 'unaweza kufanya chochote utakacho', na kwamba wasererekaji lazima wakae ndani ya mipaka.
Juzi usiku gazeti la Dauphine Libere la mjini Grenoble liliripoti kwamba maisha ya Mjerumani huyo yako hatarini.
Ripoti yake ilisomeka: "Afya ya dereva huyo mkongwe imekuwa mbaya na hali yake inachukuliwa kama ya kutishia maisha, kwa mujibu wa taarifa tulizonazo."
The Dauphine ni moja ya magazeti yanayoheshimika sana kwenye eneo hilo la milima ya Alps, huku likiwa na vyanzo vya kuaminika vya habari za kitabibu.
Schumacher, ambaye anatimiza miaka 45 Ijumaa ya wiki hii, alikuwa akiserereka sambamba na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 14, Mick huko Meribel, katika eneo la kusererekea la Trois Vallees kwenye milima ya Alps nchini Ufaransa.
Anamiliki jumba la kifahari katika eneo hilo.

No comments: