MBUNGE 'AMCHANA VIPANDE' WAZIRI MWAKYEMBE...

Dk Harrison Mwakyembe.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha amemtaka Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, aache kufanya kazi na vyombo vya habari na badala yake awajibike katika kutatua masuala ya uchukuzi.
Pia, Mbunge wa Nkasi Kusini, Kessy Ali Mohammed, amewataka wabunge wenzake waache kuwaita mawaziri mizigo, wakati viongozi hao hawawezeshwi kushughulikia maeneo yao.
Pamoja na wabunge hao, wabunge wengine waliochangia wametaka Serikali isiharakishe kujenga kwanza Bandari ya Bagamoyo, hadi pale itakapokamilisha kukarabati bandari zilizopo, ikiwemo ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.
Akichangia katika mjadala wa taarifa za Kamati ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini zilizowasilishwa bungeni hapo mapema leo, Msabaha alisema hatompongeza Mwakyembe kwa kuwa hakuna kazi yoyote aliyofanya hadi sasa.
Katika hotuba yake ambayo ililenga kumchafua Mwakyembe, alisema tangu waziri huyo aingie madarakani, amekuwa akiahidi kushughulikia masuala ya uchukuzi ikiwemo bandari, lakini hakuna mafanikio yoyote yaliyoonekana.
“Nakuheshimu sana Mwakyembe, lakini kwa leo hapana, kila siku tunazungumzia masuala ya magati tu, hakuna lolote unalofanya, kazi kufanya kazi na waandishi wa habari tu, haya hao viongozi uliowafukuza umepata mabadiliko gani? Alihoji.
Kuhusu suala la Kampuni ya Ndege Tanzania (ATC), alisema nchi nyingine za Afrika
Mashariki zina ndege hadi pa kuegesha hakuna lakini Tanzania tangu shirika hilo lianzishwe sasa lina ndege moja tu, ambayo nayo ina hali mbaya.
“Jamani naomba tusimpe Rais wetu wakati mgumu, tumekaa hapa tunasema mawaziri wetu ni mabomu, huyu ni bomu la petroli, nashangaa watu wanamsifia, Waziri ni mjumbe wa Kamati ya Bunge, lakini Mwakyembe hahudhurii vikao, hata salamu hatoi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Kessy alisema anashangazwa na watu wanaowaita mawaziri mizigo, wakati mawaziri hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, kutokana na uhaba wa fedha uliopo.
Alisema ili sifa ya umzigo kwa mawaziri iweze kuwa ya kweli, inabidi wawezeshwe kwanza kushughulikia maeneo yao ndipo wanyooshewe vidole.
 “Sasa nyie mmekaa hapa, eti Waziri fulani bomu, hajawezeshwa, mnataka atoe fedha zake mfukoni ndio muone anafanya kazi?
Alishauri Serikali itafutie ufumbuzi wa haraka tatizo la Reli ya Kati, kwa kuwa pamoja na kuwa mkombozi wa kiuchumi, lakini pia ndio kimbilio pekee la usafiri kwa
wananchi wa kipato cha chini, ambao hawawezi kumudu usafiri wa ndege na mabasi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Lucy Nkya aliitaka Serikali ibainishe wazi utaratibu wa kutoa na kusimamia vibali vya kuchimbia madini, kwa kuwa kumekuwa na madai ya kuwepo kwa wageni kutoka nje wanaoingia nchini
kinyemela na kujishughulisha na shughuli za uchimbaji.
Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) alisema alitaka mkakati unaotajwa wa mara kwa mara wa kufufua na kuboresha Reli ya Kati
uharakishwe ili kuokoa Bandari ya Dar es Salaam.

No comments: