MBOWE ADAIWA KUPORA SAFARI YA MBUNGE WA KIKE...

Mwigulu Nchemba (kushoto) na Freeman Mbowe.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), amemshambulia na kumshitaki bungeni, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, kuwa amehusika kumzuia mmoja wa wabunge wake, kwenda safari aliyogharimiwa na ofisi na badala yake kwenda kwingine. 
Pamoja na mbunge huyo wa viti maalumu, Joyce Mukya (Chadema), pia hali ilichafuka bungeni hapo, ambapo wabunge kadhaa nao walirushiwa kashfa za kupokea fedha za safari na ‘kuingia nazo mitini’.
Nchemba alisema hayo jana baada ya kuomba Mwongozo wa Spika, akitaka matukio ya wabunge hao, kutoweka na fedha za Serikali yasihusishe wabunge wote na kulichafulia taswira Bunge hilo.
“Mwongozo ninaotaka kuomba ni kwamba Kiti chako kinachukua hatua gani stahiki ya kupambanua kwamba mambo yaliyofanywa na mbunge binafsi yashughulikiwe kwa mbunge binafsi mwenyewe, kuliko kuacha Bunge zima tuonekane ni wa ovyo,” alisema Nchemba.
Alisema tangu kuibuka kwa sakata hilo, vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taswira hasi kwa Bunge zima.
Alifafanua kwamba baadhi ya vyombo vilibainisha kuwapo baadhi ya wabunge waliopangiwa safari za kiofisi na Bunge wakalipwa fedha za safari lakini hawakwenda safari hizo.
“Kinachonisikitisha, ni kwa jambo hili kuchukua taswira kama ni Bunge lote …limevunja heshima ya Bunge na jambo hili linatuvunjia heshima hata watu ambao tuna maadili ya uongozi tunaoliheshimu Taifa letu,” alisisitiza.
Alitolea mfano wa gazeti kuandika kwamba kuna kigogo alimzuia hawara yake (mbunge) kusafiri huku  tayari akiwa amelipwa kila kitu.
Alisema ingawa suala hilo ni  la kibinafsi, lakini kuna ujumbe ambao aliupata kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani, Mbowe ndiye aliyemzuia mbunge wake ambaye magazeti yameandika kuwa wana uhusiano.
“Mimi sipendi kwenda kwenye uhusiano, nataka kwenda kwenye taswira ya Bunge na Taifa, kwamba mnapopanga wabunge mnapanga wa chama tawala na wapinzani, ili kuweka uwakilishi lakini walikwenda wa CCM wengine wakazuiwa,” alisema.
Alimnukuu Mbowe katika barua yake aliyomwandikia Ofisa wa Bunge anayeshughulikia masuala ya Bunge Kabunju S Kabunju: “Rejea mazungumzo yetu Bwana Kabunju kuhusu mheshimiwa Joyce Mukya ambaye yuko safarini.
“Nitashukuru kama utambadilishia ‘booking’ yake ili aweze kurudi, aondoke New York Desemba mosi na kurejea Dubai baadaye ataunganisha kurejea Dar es Salaam. By Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Nakala kwa  Joyce Mukya.”
Alisema pamoja na kwamba hayo ni mambo binafsi aliitaka ofisi ya Bunge, itoe tamko kuwa inakuwaje mbunge aliyetumwa kuwakilisha Taifa kisha mtu binafsi kwa kutumia nafasi yake anamrudisha wakati tayari ametumia fedha za serikali na ameshakatiwa tiketi.
“Ameziba nafasi ya kwenda kuliwakilisha Taifa kule, anamwita arudi Dubai na ni mbunge Maalumu, je, hili lina taswira gani kwa Taifa na Kiti chako kinatoa kauli gani kwa watu ambao wanakwenda kutumia fedha za Serikali kwa mambo binafsi Dubai?
“Taifa langu lina bahati gani mbaya … kiasi gani mtu ambaye anatakiwa atoe ‘check and balance’ wanaitana kwa fedha za Serikali kwa burudani Dubai,” alihoji Nchemba.
Baada ya Mwongozo huo, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), alibainisha kuwa Nchemba, ameainisha tatizo hilo, kwa upande mmoja wa upinzani na kusisitiza kuwa wapo wabunge wa CCM ambao pia wamekuwa wakichukua fedha za safari lakini hawaendi.
“Taarifa za wabunge wengi ambao wanachukua fedha bila kwenda si wa upande wa upinzani pekee, wapo wa CCM ambao ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya  akiwamo Zambi (Mbunge wa Mbozi Mashariki),” alisema Silinde.
Alisema Zambi alichukua fedha za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) lakini  hakwenda na wenzake na akawa anazunguka kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana mkoani Mbeya.
“Kinachotakiwa kifanyike ni Bunge lako kuchukua hatua stahiki na wala si kuainisha upande mmoja na wapo wabunge wengine wengi tu ambao wajumbe wanawafahamu na wataendelea kuwataja, tunaomba Mwongozo wako namna gani hili suala litachukuliwa hatua na wala si kufanya propaganda za kisiasa ndani ya Bunge lako,” alisisitiza.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), alisema ni jambo la aibu kwa  Bunge kuingia katika utovu wa nidhamu wa  namna hiyo na kujiwekea taswira mbaya kwa wananchi, kuhusu fedha za umma huku akihoji namna ambavyo chombo hicho kitashughulikia tatizo hilo.
Alisema PAC ambayo inahusika na masuala ya fedha za umma tayari imeshamwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) afanye uchunguzi kuhusu safari zote za Bunge ili jambo hilo liweze kufika mwisho na kuahidi taarifa hiyo kuwasilishwa kwa Spika.
“Tutaileta taarifa hiyo kwa Spika na kama atapendezwa ataileta bungeni ili mambo hayo tuweze kuyamaliza; ni aibu sana kuanza kuyajadili bungeni,” alisema Zitto.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (Chadema), alionesha kushangaa suala la watu kusafiri na wapenzi wao ligeuke mjadala bungeni na kuhoji mbona kuna mbunge aliiba mkufu lakini hawakumjadili.
Akitolea Mwongozo suala hilo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alisema amepokea Mwongozo huo, na kubainisha kuwa suala hilo ni la kiutawala na masuala yote yanayohusu fedha yanatawaliwa na sheria na kanuni za fedha.
“Suala hili ni la kiutawala na kama nilivyosema, kuna kanuni na sheria za Bunge za fedha, kama hayo yanayosemwa yatathibitika, watatakiwa kurejesha fedha hizo,” alisema.

No comments: