Mawaziri waliotimuliwa, kutoka kushoto ni David Mathayo, Shamsi Vuai Nahodha, Emmanuel Nchimbi na Khamis Kagasheki. |
Mawaziri waliokumbwa na kadhia hiyo Ijumaa iliyopita ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo).
Jana Nahodha ambaye hakupata kusema neno tangu aondolewe madarakani, alikuwa wa mwisho kuzungumzia hali hiyo, aliposema kwamba kuwajibishwa kwake ni mtihani ambao Mwenyezi Mungu ameuweka katika dunia, ambayo ni wajibu wake kumpata binadamu yeyote.
“Kujiuzulu nafasi ya uwaziri ni mambo ya kawaida ambayo ni sehemu ya mitihani iliyopangwa na Mwenyezi Mungu ambaye ameiweka kwa waja wake walimwengu,” alisema. Hata hivyo hakujiuzulu, bali uteuzi wake ulitenguliwa na Rais.
Nahodha alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa CCM wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, ambako ni mlezi wa chama.
Kiongozi huyo ambaye alipata kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), alisema pamoja na hatua hiyo, hana kinyongo na ataendelea kuwa mwaminifu kwa Serikali ya Muungano na SMZ.
Alisema yeye ni mtiifu na mwaminifu kwa Serikali ya Muungano chini ya Rais Kikwete na kuwajibishwa kwake ni sehemu ya mitihani ya kazi za kawaida katika utumishi wa Serikali, kama kiongozi aliyekabidhiwa dhamana. “Mimi naahidi nitakuwa mwaminifu na mtiifu kwa serikali zote mbili; ya Muungano na ya Mapinduzi. Kujiuzulu kwangu katika nafasi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, si kigezo cha kushindwa kutii viongozi wangu akiwamo Rais Kikwete,” alisema. Alimpongeza Rais kwa kumwamini na kumkabidhi majukumu makubwa ukiwamo uwaziri wa Mambo ya Ndani na baadaye wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Jana pia baadhi ya vyombo vya habari, vilinukuu taarifa ya Dk Nchimbi aliyoweka juzi katika mtandao wa Facebook kuzungumzia pamoja na mambo mengine, shukrani ya kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa kwake.
“Kama Mungu ataniuliza leo ni kitu gani anipatie kwa muda huu, jibu langu litakuwa rahisi, nitamwambia Mungu wangu naomba moyo wa upendo kwa kila mmoja na moyo wa kusamehe kila mmoja, bila kujali kinachotokea na kunipa kiu ya kuhudumia wanadamu wenzangu kwa saa 24 kwa siku,” aliandika Dk Nchimbi.
Kagasheki alipata nafasi ya kuzungumza muda mfupi kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza uamuzi wa Rais kwake na wenzake, akisema aliamua kujiuzulu kutokana na yaliyojiri kwenye ripoti ya Lembeli.
“Mimi ni mtu mzima, nimesikia hisia nyingi sana zilizotolewa na wabunge, wengine wamesema mimi ni lazima nichukue uamuzi wa kisiasa, nasema Rais Dk Kikwete, aliponiteua katika wadhifa huu ilikuwa ni kwa furaha yake,” alisema.
“Naamini anaamini kuwa ningeweza kufanya kazi hii kadri nilivyoweza, kutokana na operesheni hii yametokea yaliyotokea, na uhakika utaratibu utafanywa ili kujua hali halisi, naomba nijiuluzu,” alisema na kusisitiza kuwa atachukua hatua inayostahili ya utaratibu wa kujiuzulu. Hata hivyo kabla ya utaratibu huo, Pinda alitangaza kuwa uteuzi wake umetenguliwa.
Dk Mathayo kama ilivyo kwa Kagasheki, alipata wasaa wa kuzungumza muda mfupi kabla ya uamuzi wa Rais kutangazwa na Pinda, akajitetea huku akisema taarifa ya Operesheni Tokomeza Ujangili haijamgusa kokote na tuhuma alizotupiwa na wabunge hazikuwa na uhusiano na wizara yake.
“Ripoti nzima sikuonekana, ila nimeonekana kwenye mistari ya mwisho kwamba nijipime… hakuna tuhuma zozote dhidi yangu. Sikuitwa sehemu yoyote na Kamati hii.
“Watu wanasema Mpare anauza ng’ombe kwa kesi ya kuku, hiyo ni kwa sababu anataka haki, yaliyosemwa yote ipo mipango ya kuyatekeleza. Tatizo kubwa lipo katika ardhi na wizara yangu haihusiki na kupima ardhi.
“Katika hili nimeonewa, nawashukuru sana, jambo lingine tatizo lililopo ni uhaba wa fedha ambayo wizara inapewa ndiyo maana mambo mengine yanashindwa kutekelezeka,” alisema.
Ripoti hiyo inaainisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kupata kutokea katika historia ya nchi.
Mbali na kutokea mauaji ya watumishi sita na watuhumiwa 13, ripoti hiyo ilibainisha udhalilishaji na mateso kwa binadamu.
Miongoni mwa mateso hayo, ni kuwa viongozi wa vijiji na vitongoji na watumishi wa Serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza.
“Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa, walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao.
“Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Ulanga, alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanawe wa kiume wa umri wa miaka 11 akishuhudia,” ilieleza taarifa hiyo.
Nyenge pia kwa mujibu wa taarifa hiyo, alidai kutakiwa kuchora picha ya chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake.
“Baadhi ya kinamama walidai kubakwa na kulawitiwa, mfano Kata ya Iputi, mwanamke alidai kubakwa na askari wawili usiku.
“Mama mkazi wa Kata ya Matongo, Bariadi, alibakwa na askari watatu huku ameshikiwa mtutu wa bunduki,” taarifa hiyo ilieleza.
Kwa viongozi, Diwani wa Sakasaka, Meatu, Peter Samwel, alidai kuadhibiwa akiwa mtupu, kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa nyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti.
“Baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa jina kama vile Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajenga (Serengeti),” ilieleza ripoti hiyo.
No comments:
Post a Comment