Friday, December 13, 2013

MAHAKAMA YASEMA LIYUMBA ANA KESI YA KUJIBU...

Amatus Liyumba.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuona aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba ana kesi ya kujibu.
Liyumba anakabiliwa na kesi ya kukutwa na simu wakati alipokuwa gerezani kutumikia kifungo chake cha miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.
Hakimu Mkazi Augustina Mmbando alitoa uamuazi huo  jana baada ya kupitia na kuridhika na ushahidi wa mashahidi sita pamoja na vielelezo vya upande wa mashitaka.
Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa, Mahakamani imemuona Liyumba ana kesi ya kujibu na anatakiwa kuanza kujitetea Jumatatu ijayo.
Liyumba kupitia kwa Wakili wake Hudson Ndusyepo alidai kuwa atajitetea mwenyewe hatakuwa na shahidi mwingine.
Ilidaiwa kuwa Julai 27, mwaka jana Liyumba akiwa mfungwa katika Gereza la Ukonga, alikutwa na simu aina ya Nokia 1280 nyeusi yenye laini namba 0653 004 662 akiwa nyuma ya tangi la maji lililopo karibu na pampu ya maji kwenye gereza hilo.
Liyumba alisomewa mashitaka hayo wiki mbili kabla ya kumaliza kifungo chake ambapo Septemba 23, mwaka jana alitoka gerezani baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili gerezani.

No comments: