KIFO CHA MAMA MJAMZITO CHAZUA TAFRANI SUMBAWANGA...

Kifo cha mjamzito aliyekuwa akijifungua katika kituo cha afya Mtowisa, wilayani Sumbawanga,  kimezua tafrani baada ya wananchi kushambulia gari la kubeba wagonjwa  wakitaka kulichoma kwa madai kwamba limechangia.

Wananchi walidai gari hilo lililotolewa  kama msaada na Shirika lisilo  la Kiserikali la Africare kwa kituo hicho, lilichelewa kufika na hivyo kusababisha kifo cha mwanamke huyo aliyekuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Mtowisa A.
Baada ya kifo cha Mwalimu Lea Mgaya juzi, inadaiwa wakazi wa eneo hilo, walishambulia kwa mawe na kuvunja moja ya vioo vya gari baada ya kushindwa kumnyang’anya funguo dereva wa gari hiyo aliyefika kituoni kumchukua mjamzito huyo anayedaiwa kupoteza damu nyingi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,  Ofisa Tarafa ya Mtowisa, Peter Masindi alisema awali, mwalimu huyo alipelekwa kituoni hapo asubuhi akiwa katika hali uchungu wa kujifungua lakini baadaye ilionekana anahitaji kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Rukwa, mjini Sumbawanga. Masindi alisema ililazimu adhuhuri kupiga simu Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya kuomba msaada wa gari lakini gari ilichelewa kufika kutokana na kukwama njiani ambako kulitokana na hali ya mvua iliyosababisha magari kushindwa kupita hadi saa 1 usiku lilipofika eneo la tukio na kukuta mjamzito huyo akiwa amefariki.
Miongoni mwa waliozungumza na mwandishi, walidai hasira zao zilitokana na kukerwa na kitendo cha gari hilo lililotolewa kwa ajili ya kituo chao, kutokukaa kituoni hapo.
“Hasira za wananchi hao zilionekana baada ya kufika kwa dereva wa gari hiyoaliyefika huku akiliza king’ora, lakini alipokewa na vijana waliokuwana mabango ndipo walipomsimamisha wakiwa wamewekamagogo njiani,” alisema Mwaipungu. Aliendelea kusema, “Walimtaka kuwapa funguo za gari lakini dereva huyoalifanikiwa kupita pembeni kukimbia na gari hilo huku wananchi haowakilishambulia kwa mawe.”
Kwa mujibu wa wakazi hao, kumekuwapo matukio matatu mfululizo ya vifo vya wajawazito katika miezi miwili  kutokana na kukosa msaada wa haraka wa gari kuwapeleka hospitali ya mkoa.
Inadaiwa usiku huo lilipita  gari la Bohari ya Madawa (MSD) wakalikimbilia na kuanza kulishambulia wakidhani ni gari la halmashauri kabla ya dereva wake kusimama na kujitetea ndipo walipomwachia.
Hata hivyo uongozi wa serikali wa eneo hilo, ukiongozwa na Katibu Tarafa, Masindi, ulilazimika kuingilia kati kutuliza vurugu zilizokuwa zikiendeshwa na vijana hao.
Mwili wa mwalimu huyo ulisafirishwa na gari ya idara ya elimu kwenda kuzikwa nyumbani kwao Uyole, Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Rukwa, Jacob Mwaruanda  alisema hakuna mtu aliyekamatwa  kuhusiana na  tukio  hilo.
Alisema uchunguzi  unaendelea  kubaini  waliohusika na vurugu hizo sheria ichukue mkondo wake.

No comments: