BALOZI WA PAPA ATAKASA KANISA LILILOPIGWA BOMU ARUSHA...

KUSHOTO: Askofu Fransisco Padilla. KULIA: Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti siku lilipopigwa bomu.
Hatimaye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti jijini hapa lililopigwa bomu Mei 5 mwaka huu na kuahirishwa uzinduzi wake, limezinduliwa jana na Balozi wa Papa na Mwakilishi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Fransisco Padilla.

Kabla ya uzinduzi wa kanisa hilo, ibada hiyo ilianza kwa kubariki makaburi matatu ya Regina Laizer (50), James Kessy (16) na Patricia Assey (10), ambao wote waliuawa Mei 5 mwaka huu, wakati walipokuwa kwenye ibada ya uzinduzi wa kanisa hilo, baada ya bomu kurushwa na mtu asiyejulikana na kusababisha majeruhi zaidi ya 60.
Akizungumza wakati wa mahubiri, Askofu Padilla alisema mara baada ya tukio hilo alikwenda kwa kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis anayeongoza Kanisa hilo lenye wafuasi bilioni 1.2, naye alimwamuru arudi Tanzania mkoani Arusha, ili awape pole waumini wote waliofikwa na tukio hilo.
"Sasa nawapa pole sana na amenituma nije kupatakasa mahali hapa, pawe patakatifu kwa ajili ya utoaji wa huduma za Kimungu," alisema Askofu Padilla.
Askofu Padilla alisema alitumia muda mwingi kuwaasa waumini kuwa na umoja na mshikamano katika kujenga kanisa, ili kuwe na matunda mazuri kwa kanisa.
"Nasema hivi sababu nitafurahi kuja kuona watoto wenu wametoka hapa kuwa watawa, masista na mapadri na wakiongoza ibada hapa, nitafurahi sana," alisema Askofu Padilla.
Alisema kuwa Kanisa hilo baada ya kuzinduliwa litumike kuwa msingi wa kusaidia wasio na uwezo na siyo kulitumia jengo hilo kwa njia isiyofaa wala kuleta matunda kwa kanisa.
Aidha alisema pindi wanapopata majaribu ya shetani, wasikate tamaa, kwani hawana budi kuimarisha imani zao, kwani shetani hana mamlaka ya kuangusha nguvu za Mungu kwa sababu anawalinda kila wakati.
Alisisitiza kuwa ni vema kanisa hilo ambalo limekumbwa na tukio la  aina yake, likatumika katika kuibua vipaji vya miito na kuwahubiria wengine juu ya wokovu ili nao waokoke.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu, aliyekuwa mwenyeji wa Balozi huyo, alisema ni vema waumini wakajua kuwa mipango ya Mungu haiwezi kuangamizwa na shetani, hivyo walishindwa kuzindua kwa wakati ule uliopangwa kwa sababu ya vikwazo vya shetani na sasa wamemshinda shetani na wamezindua kanisa hilo.
"Mjue wazi mpango wa Mungu hauwezi kuangamizwa na mtu yeyote na ndio sababu leo tupo hapa tukiweka wakfu katika kanisa letu na kubariki makaburi ya waumini wetu waliofia imani yao ya Katoliki," alisema Askofu Lebulu.
Alisema hata katika Biblia inasema wakati ule Mfalme Herode alipanga kuangamiza watoto wote wa kiume ili amwangamize Yesu, lakini alishindwa na ndivyo hata leo shetani atajiinua na atashindwa.
Askofu Lebulu alisema watu wote watatu waliofariki kwa kupigwa na  bomu kanisani hapo, walifariki, lakini waliobaki wamepata uponyaji na nguvu ya maombi zaidi ya hapo mwanzo kabla ya tukio hilo.
Baada ya kueleza maneno hayo aliongozana na Askofu wa Jimbo la Mahenge, Agapite Ndorobo na Askofu Fransisco Padilla, kwenda kwenye makaburi yaliyopo mbele ya kanisa hilo na kuyanyunyizia maji ya baraka.
Uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Jubilei ya Jimbo la Arusha, ambayo kilele chake, kinatarajia kufanyika leo  katika Kanisa la Mtakatifu  Theresia wa Mtoto Yesu na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na maaskofu na mapadri mbalimbali kutoka ndani ya mkoa, nje na ughaibuni.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema kwa furaha kubwa amefarijika sana kumwona Balozi wa Papa  akirudi Arusha kukamilisha kazi aliyoacha kwa sababu ya kukatishwa na mwovu shetani .
"Nakukaribisha sana hapa Olasiti na nakuhakikishia mwovu shetani ameshindwa kabisa na ametoweka na ameshindwa kabisa na wakati wote wa misa nilifurahi na kuruka kusikia kuwa hakuna jambo lingine," alisema Mulongo.

No comments: