![]() |
| Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dodoma. |
Wakizungumza nyakati tofauti jana wakati wa kujadili muswada huo, uliowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, wabunge wengi waliunga mkono kwa kusema hatua walizoafikiana viongozi wa vyama na Rais Kikwete, umeleta maridhiano ambayo yanapaswa kuungwa mkono.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) alimpongeza Rais Kikwete kwa kukutana nao kufanya maridhiano na kueleza kilichopo sasa ni wabunge, wananchi na vyama vyote kujenga utamaduni wa maridhiano ili kupata Katiba nzuri.
“Wote tunafahamu sintofahamu iliyotokea katika Bunge la 12 si mambo ya kujivunia wala kubezana kwani ni wazi hatukumaliza tukiwa wamoja, kwa niaba ya Kambi ya upinzani tunampongeza sana Rais Kikwete kuona haja hiyo kwani hali ile ilileta shida hata kwa watu wa nje.
“Mchakato wa Katiba unaweza kuendelea na kupingana katika baadhi ya mjadala, lakini siamini kama kuna mtu yeyote humu ndani anataka mchakato huu ulete vurugu ila tunapotofautiana na kuvumiliana tutafikia mwafaka, mambo tuliopigania serikali imeridhia ingawa hatuwezi kukubaliana yote ila maridhiano ni jambo muhimu,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe alipendekeza ukomo wa Tume ya Katiba usiishie kabla ya Bunge Maalumu la Katiba kama inavyopendekezwa kwenye muswada na kwamba ni vyema Tume hiyo ikabaki ili iwezeshe kutoa msaada wakati wa Bunge la Katiba hata kama si wapiga kura kwa kuruhusiwa na kanuni zitakazoongoza Bunge hilo ili waweze kutoa ufafanuzi.
Tofauti na ilivyokuwa awali kwamba vyama vya upinzani walikuwa wakiipinga Tume ya Katiba, Mbowe alisema wanakubali kuwa kwa kiasi kikubwa sana Tume hiyo imefanya kazi kubwa ya kukusanya maoni ya Watanzania wengi wakati wa kukusanya maoni na mchakato mzima hivyo ni vyema ikabaki wakati Bunge Maalum la Katiba likiendelea ili waweze kutoa ufafanuzi wa kitaalamu pale unapohitajika.
Mbowe alisema, suala la Katiba si la kufanywa kwa jazba kwa kuwa vyama vilivyopo vinaweza kupita, viongozi wakapita lakini Katiba ni kwa maslahi ya Watanzania wote hivyo hilo liwaongoze wabunge kumaliza suala la Katiba kwa usalama ili kulinda Taifa kwa kuwa nje ya amani hakuna maendeleo kwa taifa zima. Alisema Kambi ya Upinzani inaunga mkono hoja hiyo kwa maridhiano waliofikia na anaomba wamalize salama kwa umoja na si utengano.
Awali, Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) alimpongeza Rais Kikwete kwa maridhiano hayo na kueleza kuwa, muswada huo umekuwa shirikishi kwa Tanzania Bara na Zanzibar na kuongeza kuwa, lazima kuwa na tabia ya kuzungumza na kukubaliana katika masuala ya Kitaifa.
“Naishukuru Serikali ya Muungano katika hili Zanzibar imeshirikishwa kikamilifu, sisi kule Zanzibar tumezoea siasa za vurugu lakini kwa hili tumeshirikishwa, muswada huu utawezesha kusonga mbele na napendekeza kuwepo kwa Kamati Maalumu ikiwa Tume itavunjwa ili kanuni ziwaruhusu kuingia kutoa msaada wa ufafanuzi,” alisema Mnyaa.
Alisema muswada huo utawezesha kusonga mbele kwa Bunge la Katiba na kwamba makubaliano kwa zaidi ya asilimia 60 yaliyofikiwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wajumbe wa nje wasio wabunge kwa sasa kutoka 166 mpaka 201 ni la maslahi ya Taifa na la kupongezwa.
Naye Mbunge wa Magogoni, Kombo Khamis Kombo (CUF), alisema Muswada huo umepata baraka zote upande Zanzibar na kwamba katika historia jambo hilo limefanywa kwa kuzingatia matakwa ya umma na wana imani matarajio yao ni kuwa hatua hiyo italeta matokeo mazuri ya kupata Katiba mpya.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Katiba ni matokeo ya maridhiano ingawa yapo ya kukubaliana na kutokukubaliana, lakini alisema ni wakati wa kutumia hekima na busara na kumpongeza Rais Kikwete kwa mkutano wa maridhiano.
“Tujihadhari na siasa za kulipiza kisasi, tuepuke siasa za chuki za nje ili tupate Katiba kwa nia njema tuvuke hapa, mengi tuliyokubaliana na Rais Ikulu yamo katika muswada huu, maridhiano tuliofikia yamo humo, niombe tusing’ang’anie itikadi zetu za vyama bali Utaifa wetu na nitamke kwamba naunga mkono hoja hii,” alisema Mbatia.
Awali akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu Muswada huo, Tundu Lisu, Mbunge wa Singida Mashariki, alisema kwa asilimia kubwa maridhiano yamefikiwa baina yao na Rais Kikwete Ikulu na kwamba imani yao ni kupata Katiba bora ingawa yapo mambo ambayo watakubaliana ingawa mengi ikiwemo theluthi mbili ya wabunge wa pande mbili kupiga kura ndio iwe mwafaka ni sahihi na ya kuungwa mkono. Mengine upinzani waliokubali ni mabadiliko ya vifungu kadhaa na hoja ya kuongeza idadi kutoka 166 hadi 201 ingawa awali walipendekeza iwe 438.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alisema upinzani walipendekeza 438 lakini baada ya maridhiano walifikia angalau iwe theluthi mbili ya wabunge wa Bunge la sasa la Muungano na Wawakilishi ambao ni 438. Mapendekezo ya muswada ni kufikia watu 201 toka 166 ya awali.
Muswada huo pia uliungwa mkono na wabunge wa CCM akiwemo Jenista Mhagama wa Peramiho, Christopher Ole Sendeka wa Simanjiro ambao kwa pamoja walipendekeza muafaka uliofikiwa uzingatiwe ili kupata katiba nzuri yenye uwakilishi pia wa wanawake na watu wenye mahitaji maalum.
Muswada huo uliletwa bungeni kwa Hati ya Dharura ya Rais Kikwete Oktoba 28 mwaka huu baada ya Rais kukutana na viongozi wa vyama vya siasa Oktoba 15 mwaka huu na kufikia mwafaka wa mabadiliko kwa baadhi ya vipengele ikiwemo idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka 166 hadi 201.

No comments:
Post a Comment