![]() |
| Baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo waliofunga maduka yao kugomea mashine za risiti juzi. |
Alisema hayo jana wakati akizindua mradi wa maji katika Shule ya Msingi Olomitu, iliyoko Kata ya Mlangarini wilayani Arumeru. Mradi huo umefadhiliwa na Kampuni ya maua ya Kiliflora.
Waziri Mkuu alisema mashine hizo ni za uhakika na hazina tatizo na zinauzwa Sh 800,000 lakini baada ya wafanyabiashara hao kulalamika bei kubwa TRA ilipunguza bei hadi Sh 600,000.
Aliongeza kuwa wazabuni walijitokeza kuomba zabuni za uuzaji wa mashine hizo, lakini 11 ndio walipitishwa na TRA kuziagiza na kuuzia wafanyabiashara nchini.
Alihoji, "ufisadi uko wapi wakati kampuni 11 ziliteuliwa kuuza mashine hizo? Pia mkumbuke kuwa gharama za ununuzi wa mashine hizo mtarudishiwa kadri mnavyokusanya mapato na kuisaidia Serikali.
"Hakuna sababu ya kuona jambo hili kama kero bali ni elimu tu kwa maana mnaponunua mashine hizo mnarudishiwa fedha zenu, hivyo nakuombeni wafanyabiashara muachane na masuala ya kudai kuwa kuna ufisadi, hapana," alisema.
Aliendelea: "Elimu itolewe zaidi ili watu wajue faida za mashine hizi, pia Serikali itaendelea kuhakikisha maji yanapatikana kwa wingi ili kupunguzia wanawake kero ya kutembea umbali mrefu kufuata maji".
Katika hatua nyingine, Serikali imebaini kuwapo baadhi ya wafanyabiashara wenye uwezo mkubwa kuchochea mgogoro huo kwa kuwa hawataki kulipa kodi.
Sambamba na hilo, Serikali imetaka wafanyabiashara hao kusitisha mgomo wao na kuendelea kulipa kodi kwa sababu ni wajibu wa kila mtu.
Aidha, Serikali imesema malalamiko ya wafanyabiashara hao kuhusu bei ya mashine za kutolea stakabadhi EFDs yanajadilika na kwa sasa iko katika majadiliano na msambazaji wa mashine hizo kwa ajili ya kuhakikisha zinashuka bei zaidi.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kwa ajili ya kutolea ufafanuzi wa mashine hizo na pia kutoa majibu ya malalamiko ya wafanyabiashara, baada ya mgomo wa karibu siku mbili, Naibu Waziri Wizara ya Fedha, Saada Salum Mkuya na Janeth Mbene walisema Serikali inataka watu wanaochochea mgomo huo waache.
Juzi na jana mamia ya wafanyabiashara wa Kariakoo waligoma kufungua maduka na kusababisha shughuli zote za biashara kusimama wakipinga matumizi ya mashine, hatua hiyo mbali na kusababisha adha kwa wananchi wa ndani na nje ya Jiji na nchi jirani waliofika kununua bidhaa.
Akitoa ufafanuzi, Mkuya alisema mashine za EFDs zinatumiwa kwa wafanyabiashara ambao mauzo yao ni kuanzia Sh milioni 14 hadi Sh milioni 40 kwa mwezi, lakini wafanyabiashara wanaogoma Kariakoo wengi wao ni wafanyabiashara ambao hawahusiki na mashine hizo.
"Kuna wafanyabiashara wachache tu wanachochea mgomo huu, kwa sababu tu hawataki kulipa kodi wakati wakijua wafanyabiashara wengine hawahusiki na mashine hizo, lakini wakitaka kufungua maduka yao wanaambiwa yatachomwa moto, huu ni ukiukwaji wa sheria zaidi," alisema Mkuya.
Alisema mfumo wa kutumia mashine za kodi za kielektroniki ulianza awamu ya kwanza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na awamu ya pili ni hii ya mwaka huu, ikihusu wafanyabiashara ambao hawakusajiliwa kwenye VAT ambao mauzo yao ghafi kwa mwezi ni Sh milioni 14 hadi 40.
"Ikumbukwe kuwa gharama zote za ununuzi wa mashine hizi zitarudishwa kwa mfanyabiashara atakapowasilisha mahesabu yake ya kodi atasamehewa pindi atakapowasilisha mahesabu yake, hivyo itafanya Serikali kulipia gharama za mashine kupitia kodi," alisema.
Alisema malalamiko kuwa mashine hizo zinapatikana kwa bei nafuu Dubai na China, kuwa taarifa hizo si sahihi na kwamba mashine hizo zilitengenezwa maalumu kwa ajili ya matumizi ya Tanzania kulingana na mahitaji haziwezi kufanana.
Naibu Waziri huyo alisema kumekuwa na malalamiko kuwa utumiaji wa mashine utasababisha wafanyabiashara kutozwa kodi ya VAT ya asilimia 18, alisema ukweli ni kwamba awamu hii ya pili hawakati bali ni kwa ajili ya kodi ya mapato.
Alisema wafanyabiashara zisizo rasmi aina ya mama lishe, wamachinga na wengine ambao hawana sehemu maalumu ya kufanyia biashara na wasiofikia mauzo ya Sh milioni 14 hawahusiki katika mashine hizo hivyo waendelee na shughuli zao.
Wanaolengwa ni wenye maduka makubwa ya spea, mawakili, maduka ya jumla, wafanyabiashara wakubwa wa mbao, migahawa mikubwa, maduka ya simu na spea zake, baa na vinywaji baridi, studio za picha, wauza pikipiki na biashara nyingine.
"Kwa nchi nzima tumelenga wafanyabiashara 200,000 tu kwa awamu hii ya pili kati ya wafanyabiashara zaidi ya milioni moja na nusu waliosajiliwa kulipa kodi," alisema.
Alisema tuhuma kwamba mfumo wa EFD ni mradi wa mtu, tuhuma hizo si za kweli, kwa sababu mchakato wa ununuzi wa mashine ulifanyika kwa wazi kupitia zabuni ya kimataifa na kupatikana wasambazaji 11 na watengenezaji mashine.
Alisema TRA pamoja na wasambazaji na watengenezaji walifikia mwafaka, kwamba bei za mashine ziuzwe kuanzia Sh 600,000 na bei kikomo ni Sh 778,377 bei ambayo ni nafuu ikilinganishwa na nchi zingine zinazotumia mashine hizo.
"Ili kumrahisishia mfanyabiashara urahisi wa manunuzi ya kifaa hicho, TRA iliongea na wasambazaji ambao wamekubali kuuza mashine hizi kwa kupokea malipo kwa awamu na hata hivyo, gharama halisi ya mashine hii itabaki kwa Serikali kwa sababu mwisho wa mwaka itakatwa katika kodi yake," alisema.
Kuhusu gharama za utengenezaji alisema watengenezaji wametoa waranti ya miaka mitatu kwa mashine itakayoharibika pasipo makusudi hivyo wasambazaji watawajibika na matengenezo.
Mbene alitaja faida za mashine hizo kuwa zinasaidia kukadiria kwa usahihi kodi ya mfanyabiashara anayotakiwa kulipa tofauti na awali TRA ilikuwa ikikadiria tu, zina uwezo wa kutunza kumbukumbu za mauzo ya mfanyabiashara kwa miaka mitano na pia kutuma taarifa moja kwa moja TRA, EWURA, Benki Kuu na SUMATRA.
Hata hivyo mgomo huo jana uliingia katika siku yake ya pili huku ukisababisha usumbufu kwa wananchi waliohitaji huduma na vilio kutoka kwa wafanyakazi katika maduka hayo.
Mbali na hatua hiyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maeneo hayo pia ulibaini upatikanaji wa kiasi fulani kwa baadhi ya bidhaa kutoka kwa wauzaji wa maduka wanaofanya biashara hiyo kwa siri wakihofia vurugu kutoka miongoni mwao.
Mamia ya wafanyabiashara hao juzi walianza mgomo kwa kufunga maduka wakipinga utaratibu mpya wa utumiaji wa mashine za kieletroniki zinazotolewa na Serikali kupitia TRA. Hatua iliyosababisha kusimama kwa shughuli zote za kibiashara mahali hapo.
"Tunaomba Serikali ichukue hatua za haraka kutatua mgogoro huu, tangu jana baadhi yetu hatujaingiza kiasi chochote cha fedha yakizingatiwa majukumu ya kifamilia tuliyonayo," alisema kijana aliyejitambulisha kwa jina la Jamal Abdalla.
Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara imeitaka Serikali kuunda kwa haraka Tume huru ya kuchunguza utaratibu wa kupata mashine hizo ili kutafuta ufumbuzi wa malalamiko yanayotolewa na wafanyabiashara.
Imesema baada ya kukutana na Waziri mwenye dhamana (Waziri wa Fedha), itatoa hadidu za rejea kwa Tume, lengo likiwa ni kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki na wafanyabiashara hawaumizwi na mfumo wa matumizi ya mashine hizo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini alisema hayo jana kwa niaba ya Kamati wakati akitoa maelekezo kwa Serikali baada ya kikao cha majadiliano ya muda mrefu wakipokea taarifa ya suala hilo kutoka TRA.

No comments:
Post a Comment