Monday, November 18, 2013

SHERIA YA KUWABANA MADAKTARI ILI WATIMIZE WAJIBU WAO YAJA...

Baadhi ya madaktari na wauguzi wakiandamana kudai haki zao hivi karibuni.
Baada ya kubainika nguvu za Serikali kusomesha madaktari zimeshindwa kukabili upungufu wa kada hiyo ya watumishi wa umma nchini, wadau wa sekta ya Afya wamependekeza kuundwe sheria ya kulazimisha madaktari kutimiza wajibu wao.

Mapendekezo hayo yametolewa baada ya utafiti ulioshirikisha Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kubaini kuwa madaktari wengi wakihitimu taaluma yao hawapendi kufanya kazi ya utabibu.
Utafiti huo umebaini hali hiyo wakati kada hiyo ya utumishi wa umma ikiongoza kwa kupewa uzito wa juu katika kulipwa vizuri kuliko kada nyingine za utumishi wa umma serikalini.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sikika iliyoshiriki katika utafiti huo, Irenei Kiria, kwanza alipendekeza kuwepo kwa juhudi za makusudi za Serikali na wadau wa afya, kuwavutia madaktari kufanya kazi za kitabibu katika vituo vya kutolea huduma.
Pili alipendekeza Serikali iunde sheria ya kuwalazimisha madaktari kutekeleza jukumu lao la kitaaluma, ambalo ni kutibu wagonjwa.
"Kuna haja ya kuwepo kwa mfumo, sheria na utaratibu mpya utakaowezesha madaktari walioko katika sekta nyingine, watumie muda fulani kufanya kazi ya utabibu, ili kupunguza mzigo wa kazi kwa madaktari wanaotoa huduma hizo hospitalini," alisisitiza Kiria.
Hata hivyo Katibu Msaidizi wa MAT, Dk Francis Furia, alisema chama hicho na Sikika walichofanya, ni kutafuta wapi wahitimu wa udaktari wanaenda kwani katika maeneo ya afya hawaonekani, huku tatizo la upungufu wa madaktari likibaki palepale.
"Tumeona Serikali inawekeza fedha nyingi katika eneo hili la elimu na kujitahidi kutoa wataalamu hawa kwa wingi lakini bado hawafanyi ile kazi wanayotakiwa kuifanya, sasa tumejua waliko, ni jukumu la Serikali na wadau kutafuta kile kinachowakimbiza na kukipatia ufumbuzi," alisema.
Utafiti huo umetokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuendelea kuonesha kuwa daktari mmoja nchini, anahudumia wagonjwa 30,000 wakati ilitarajiwa idadi ya wagonjwa kwa daktari mmoja kupungua, kutokana na wahitimu wa udaktari nchini kuongezeka karibu kila mwaka.
Kutokana na sintofahamu hiyo, Rais wa MAT, Dk Primus Saidia, alisema chama hicho na Sikika waliamua kufanya utafiti kwa lengo la kubaini madaktari wanaohitimu nchini wanaenda wapi.
"Tumefanya utafiti ili kujua kulikoni kwani uwiano huo wa daktari mmoja kwa wagonjwa 30,000 haubadiliki kwa miaka mingi sasa wakati vyuo vinatoa madaktari na kila mwaka wanaongezeka, sasa wanaenda wapi?" Alihoji.
Utafiti huo uliofanyika kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka jana, ulishirikisha madaktari 2,246 waliohitimu shahada zao nchini ambao walipatikana kupitia vyuo walivyosomea.
Matokeo ya utafiti huo kwa mujibu wa Dk Saidia, yalibaini kuwa madaktari 890 kati ya 2,246, sawa na asilimia 39.6 ya wataalamu hao wa tiba nchini, hawafanyi kazi ya kitabibu.
Pia imebainika kuwa ni madaktari 964 kati ya 2,246 sawa na asilimia 42.9, ndio wanaofanya kazi katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya.
"Utafiti huu pia umeonesha kuwa karibu nusu ya madaktari wote wanaishi mijini, yaani Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam na Kilimanjaro na kwa Dar es Salaam pekee wapo madaktari 725 kati ya hao 2,246 waliohojiwa," alisema Dk Saidia.
Uchambuzi wa matokeo hayo kwa kutumia kigezo cha idadi ya wahitimu kila mwaka, ulibaini wahitimu wa zamani ndio wanaoongoza kukimbia majukumu ya utabibu, ikilinganishwa na wahitimu wa hivi karibuni.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo, karibu nusu ya madaktari waliohitimu mwaka 2003, hawafanyi kazi ya utabibu. Mwaka huo madaktari 107 walihitimu nchini na kati ya hao, wahitimu 48 hawafanyi kazi za kitabibu.
Mwaka 2004, walihitimu madaktari 102 na kati ya hao, 68  sawa na theluthi mbili ya wahitimu katika mwaka huo, hawafanyi kazi za utabibu.
Mwaka 2008, wahitimu 224, wanaofanya kazi ya utabibu ni 176 na 2009 wahitimu 206, wanaofanya kazi ya utabibu 155.
Kwa mwaka 2011, wahitimu walikuwa 290 na kati ya hao, 246 wanafanya kazi za kitabibu sawa na asilimia 80 na kwa mwaka jana, Dk Saidia alisema takribani madaktari wote waliohitimu shahada zao wanafanya kazi ya kitabibu ambao ni 96 kati ya 101.
Akizungumza mwaka jana bungeni, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alibainisha kuwa udaktari ndio kada inayopewa uzito mkubwa kimaslahi serikalini kuliko kada zote.
"Tathmini ya kazi iliyofanyika serikalini mwaka 2000 inaonesha kuwa kada ya udaktari ilikuwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na kada nyingine na ndiyo maana ikatengewa mshahara mkubwa ikilinganishwa na kada nyingine.
"Pamoja na kwamba viwango vya elimu miongoni mwa watumishi wa kada mbalimbali vinaweza kufanana, ni ukweli usiopingika kwamba uzito wa majukumu (ya Daktari) hauwezi kulingana na kada nyingine.
"Kwa mfano, uzito wa kazi ya daktari hauwezi kuwa sawa na uzito wa kazi ya Ofisa Utumishi pamoja na ukweli kwamba wote ni wahitimu wenye shahada ya chuo kikuu," alisema Ghasia alipokuwa akijibu swali bungeni.
Katika swali hilo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) alitaka kufahamu kwa nini mwalimu mwenye shahada analipwa Sh 400,000, wakati Daktari mwenye shahada analipwa Sh 900,000 wanapoanza kazi.
Katika ufafanuzi wake, alibainisha kuwa kada ya pili kwa uzito serikalini ni Uanasheria ikifuatiwa na Uhandisi na mishahara yao ni mikubwa kuliko kada zingine.

No comments: