Sunday, November 17, 2013

MAMIA WAJITOKEZA KUMUAGA DK SENGONDO MVUNGI LICHA YA MVUA KUBWA...

Mke wa marehemu, Anne akilia kwa uchungu mbele ya jeneza lenye mwili wa mumewe, Dk. Sengondo Mvungi wakati wa kutoa heshima za mwisho katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana.
Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, marehemu Dk Sengondo Mvungi ametajwa kuwa nguzo muhimu katika Tume hiyo kutokana na mchango wa ziada aliokuwa nao kulinganishwa na  wajumbe wengine.

Kati ya mambo ya ziada aliyokuwa nayo ni pamoja na kufanya utafiti wa masuala kadhaa ya kikatiba   yalipohitajika pamoja na kuamini kufanya uamuzi kwa njia ya maridhiano.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba katika ibada maalumu ya kumuaga marehemu iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa  wananchi wa kada mbalimbali, licha ya mvua kubwa kunyesha.
Warioba alisema katika kubainisha hilo, mara ya mwisho kabla ya kujeruhiwa aliombwa kufanya utafiti kwa jambo muhimu  na kulikamilisha kabla ya kwenda mapumziko ya mwisho wa wiki na Jumatatu Tume ilishughulikia utafiti huo kwa mafanikio makubwa na muhimu.
"Kutokana na kuwa mwanaharakati wa haki za binadamu, aliamini katika kuamua mambo kwa maridhiano, jambo lililochangia Tume kufikia uamuzi wake mbalimbali kwa maridhiano," alisema Warioba.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, Taifa linatakiwa kumuenzi Mvungi kwa kuhakikisha Katiba mpya inapatikana kwa njia ya maridhiano na si mapambano.
Jambo hilo lilibainika pia katika waraka maalumu wa Rais Jakaya Kikwete uliosomwa na Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal aliyeongoza mamia ya watu katika shughuli hiyo.
Katika waraka huo Rais Kikwete ambaye yuko Colombo, Siri Lanka akihudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola,  alisema Dk Mvungi alikuwa mzalendo kwa nchi na ndiyo maana yeye hakusita kumchagua katika Tume baada ya jina lake kupendekezwa na NCCR-Mageuzi.
"Nchi imepoteza moja ya hazina muhimu, akiwa bado anahitajika na ambaye alikuwa na ujuzi na uzoefu katika masuala ya sheria, siasa na Katiba," alisema Rais.
Shughuli hizo za kumuaga mjumbe huyo wa tume ambaye mwili wake uliwasili juzi jioni kutoka Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu baada ya kujeruhiwa na majambazi ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali.
Miongoni mwao ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wastaafu Fredrick Sumaye, Cleopa Msuya;  viongozi wa vyama vya siasa, mawaziri, wabunge na watendaji wakuu wa idara na taasisi za serikali na binafsi.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia ambako Dk Mvungi alikuwa Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu, alisema limekuwapo ongezeko la vifo vya wanataaluma wa sheria vinavyotokana kwa kupigwa kama ilivyotokea kwa Mvungi.
Alisema Dk Mvungi anakuwa mwanasheria wa tatu tangu mwaka 2002 kupoteza maisha kutokana na  kipigo cha majambazi na kutaka kila mtu atekeleze wajibu wake na kuwa na ulinzi wa uhai wa binadamu kwa gharama yoyote bila kujadiliana.
Aliitaka Serikali na wanaolalamika kwa kitendo hiki, kuhakikisha vitendo hivi havitokei tena wakielekeza nguvu kubwa kwenye kinga badala ya kusubiri itokee.
Alisema Dk Mvungi alikuwa mzalendo na  mtetezi wa wanyonge lakini majahili wametoa uhai wake  na alimshukuru Rais Kikwete kuwa pamoja na familia ya marehemu na chama chake tangu alipojeruhiwa  hadi kufariki dunia.
Mtoto mkubwa wa marehemu, Natujwa Mvungi alimwimbia shairi baba yake akieleza bayana kuwa familia itaendelea kumuenzi kwa upendo na uzalendo aliokuwa nao kwa nchi na Watanzania wote.
Alisema baba yao hakuwa mwoga katika kila jambo hata alipokabiliwa na kifo hakukiogopa.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema marehemu ni mmoja wa waasisi wa mageuzi ya siasa nchini na hakuna kitu cha bahati mbaya, huku akiamini kuwa mvua kubwa iliyonyesha jana ni ishara ya kuwa alitolewa roho bila kuwa na  hatia.
Alisema kitendo cha watu kukutana bila kujali tofauti za dini, siasa wala kabila, kinaashiria utaifa hivyo ni vema kumuenzi kwa kudumisha utaifa uliopo.
"Marehemu alitamani kuwapo ashuhudie Katiba mpya ikipatikana hivyo tumuenzi kwa kumaliza mchakato huu kwa amani," alisema Mutungi.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, ambako marehemu alikuwa Makamu Mkuu wake, Costa Mahalu alisema katika chuo chao wameondokewa na mtu muhimu aliyekuwa na mvuto.
Alisema walianzisha chuo hicho wakiwa na wanafunzi 65 lakini sasa wamefika 880 kwa miaka mitatu tu ambapo kesho walitarajia kuanza kozi ya Uzamili katika fani ya sheria huku wakimtegemea yeye aanze kufundisha wanafunzi hao.
Alisema kwa sasa wameachwa na sintofahamu huku akibainisha kuwa majengo mapya ya chuo hicho yanayojengwa Bagamoyo eneo la Kiromo, yatapewa jina lake ili kumuenzi na kuwakumbusha siku zote juhudi zake chuoni hapo.
Wakili Peter Kibatala kwa niaba ya Chama cha Wanasheria na Mawakili Tanganyika, alitoa mwito wa kusimamia dhana ya utawala bora kwa kuondoa hofu kwenye jamii kwa watetezi kama Dk Mvungi kupata majanga.
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema Mvungi alikuwa mshauri mkubwa wa masuala ya Katiba na Rasimu yao ya vyama vya siasa huku akiwa mwepesi kukubali matokeo ya uchaguzi bila kulalamika. Dk Mvungi aligombea urais wa nchi mwaka 2005.
Alisema njia pekee ya kumuenzi ni kupata Katiba mpya yenye misingi ya matakwa ya Watanzania kwa amani huku akitaka kwa pamoja kushirikiana kukabiliana na wimbi la ujambazi nchini.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, alisema Dk Mvungi alikuwa na uthubutu na kusimamia alichoamini, hivyo ili kumuenzi ni vema watu wakawa na ujasiri bila kutetereka huku unyenyekevu na upendo unaooneshwa katika misiba ndio uwe utamaduni wa nchi.
Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bara, Mwigulu Nchemba, alitoa rai kwa Watanzania kuliombea Taifa kwa kuwa anaona roho ya pepo na uuaji inalizonga Taifa.
Huku akitaka wasomi nchini kuiga mfano wa Dk Mvungi ambaye ni msomi aliyeingia kwenye siasa na kuendeleza misingi ya taaluma na uzalendo wa nchi.
Ibada hiyo iliongozwa na Paroko wa Kanisa Katoliki la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Mosinyori Deogratius Mbiku akisaidiwa na mtoto wa marehemu Padri Gallen Mvungi.
Mbiku alisema kila mtu anatakiwa kuomba toba kabla ya kulala, kwani hawezi kujua siku wala saa kwani bila toba hataingia peponi na hapana toba baada ya kifo.
Baada ya kumalizika kwa ibada hiyo na kuaga, mwili ulipelekwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi tayari kwa safari leo kwenda kijiji cha Chanjale Kisangala Juu wilayani Mwanga, Kilimanjaro kwa maziko.
Dk Mvungi alifariki dunia Jumanne kwenye Hospitali ya Milpark, Afrika Kusini baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake usiku wa Novemba 2.
Baada ya kujeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani kabla ya kuhamishiwa Muhimbili katika taasisi ya mifupa (MOI) na hatimaye Milpark. Marehemu ameacha mjane na watoto watano.

No comments: