Monday, November 18, 2013

KILIO CHA UKOSEFU WA AJIRA CHATESA WANAOHITIMU VYUONI...

Baadhi ya wanafunzi waliohitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka huu.
Kutokana na upungufu wa ajira kwa wanafunzi wanaohitimu vyuo na taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, baadhi ya taasisi hizo zimependekeza wahitimu wao kuajiriwa moja kwa moja na Serikali, huku zingine zikiwapa changamoto wahitimu wao kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine.

Juzi katika mahafali ya 19 ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) kilichopo Bagamoyo, chuo hicho kilitoa rai kwa mgeni rasmi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuona uwezekano wa kuwapatia nafasi za ajira za moja kwa moja wanafunzi wa chuo hicho serikalini.
Akizungumzia ombi hilo, Pinda alisema ofisi yake itazungumza na Idara ya Utumishi na Rais Jakaya Kikwete kuangalia uwezekano wa kutoa ajira hizo moja kwa moja kama ilivyo kwa walimu.
"Hili moja nitalichukua, nitazungumza na Idara ya Utumishi na Rais wangu tuangalie namna ya kundi hili kulipa nafasi kama ilivyo kwa walimu.
"Kundi hili lina mchango mkubwa katika kukuza elimu yetu hapa nchini tukiwa na maktaba na wataalamu itawasaidia hata walimu wetu kujifunza na kwenda kutoa elimu bora kwa wanafunzi," alisema.
Pinda pia aliagiza halmashauri katika mipango ya maendeleo kuhakikisha wanajenga maktaba za wilaya.
Alisema wilaya 19 pekee ndizo zenye maktaba ya wilaya na zilizobaki; 133 hazina huduma hiyo jambo alilosema linawakosesha wananchi wa maeneo hayo kupata maarifa, stadi na taarifa mbalimbali.
"Wakurugenzi wanatakiwa kubebeshwa lawama kwa halmashauri zao kukosa maktaba, kuwa na huduma hii kutasaidia hata wafanyakazi wa halmashauri kuwa na sehemu ya kujifunza zaidi," alisema.
Inakadiriwa nchini kuna maktaba 600 za ngazi tofauti  zikiwemo zaidi ya maktaba 26 za vyuo vikuu, 22 za mikoa kati ya mikoa 25 na wilaya 19. Takwimu zinaonesha upo upungufu wa maktaba zaidi ya 13,000 nchini.
Wakati SLADS wakiomba ajira za moja kwa moja serikalini, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala amewataka wahitimu katika chuo hicho kwenda kuzalisha ajira kwa wengine.
Profesa Mukandala amewataka wahitimu hao katika mahafali ya 43 ya chuo hicho yaliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam,  kutumia elimu waliyoipata kutoa ajira kwa vijana wengine, kwa kuwa elimu hiyo ni ya jamii na siyo yao binafsi.
Alisema ukosefu wa ajira kwa vijana unakadiriwa kuwa asilimia 14.3 kwa wanawake na asilimia 12.3 kwa wanaume, huku maeneo ya mijini  yakiongoza kwa kukumbwa na tatizo hilo tofauti na vijijini ambako ukosefu wa ajira unakadiriwa kuwa asilimia 7.1.
Kutokana na hali hiyo, amewataka kuacha kasumba ya kubagua maeneo ya vijijini hali inayosababisha wengi wao kukaa na elimu zao bila kutumia kwa manufaa.
Alisisitiza kuwa ongezeko la wataalamu wanaozalishwa ni kubwa ikilinganishwa na nafasi za ajira kwa kuwa inakadiriwa wataalamu wanaozalishwa ni kati ya 800,000 mpaka 1,000,000 kwa mwaka.

No comments: