Friday, November 8, 2013

DK. SENGONDO MVUNGI AHAMISHIWA AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU ZAIDI...

Dk Sengondo Mvungi akiwa kwenye gari la wagonjwa tayari kuelekea Uwanja wa Ndege kwa safari ya Afrika Kusini jana.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dk Sengondo Mvungi, amesafirishwa  jana kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi, kutokana na kujeruhiwa vibaya na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi mwanzoni mwa wiki hii.

Ofisa Uhusiano wa Kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Almas Jumaa, alisema Dk Mvungi amehamishiwa katika Hospitali ya Millpark ya Afrika Kusini.
“Ni kweli ameondoka hapa majira ya saa nne akifuatana na daktari wetu mmoja ambaye ni Dk Clement Mugisha kwenda katika Hospitali ya Millpark kwa matibabu zaidi, hali yake haijabadilika bado hajapata fahamu vizuri,” alisema Jumaa.
Dk Mvungi aliondoka nchini kwa ndege ya kukodi ya Kampuni ya Flightlink namba 5H-ETG 560, ambayo ni maalumu kubeba wagonjwa . Aliondoka saa 5  mchana akifuatana na  Deogratius Mwarabu, ambaye ni ndugu yake.
Pamoja na mtoto huyo, pia alifuatana na madaktari wengine wawili na muuguzi mmoja kutoka Kampuni ya bima ya PR.
Aidha baadhi ya viongozi waliokuwepo wakati wa kumsindikiza hadi uwanja wa ndege mwanasiasa huyo ni pamoja na Mwenyekiti wa chama cha NCCR –Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Asaah Rashid na watendaji wengine wa tume hiyo.
Akizungumza na mwandishi, Mbatia alisema kutokana na taarifa za wataalamu, hali ya Dk Mvungi inaendelea kuimarika, lakini ni vyema akapata matibabu zaidi  Afrika Kusini, ambako kuna wataalamu na vifaa vya teknolojia ya hali ya juu zaidi.
Dk Mvungi mwishoni mwa wiki, alijeruhiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi waliovamia nyumbani kwake usiku wa manane. Walipora fedha na baadhi ya vitu.
 Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam inashikilia watu sita wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, huku Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, akisisitiza kuwa bado uchunguzi zaidi unaendelea.

No comments: