Saturday, November 16, 2013

CCM WAMPIGIA KURA MGOMBEA WA CHADEMA UNAIBU DIWANI ARUSHA...

Prosper Msofe.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetwaa kiti cha Naibu Meya wa Jiji la Arusha baada ya mgombea wake kuibuka na ushindi mnono katika uchaguzi huo ambao CCM haikusimamisha mgombea, huku mgombea wa TLP akijitoa dakika za mwisho kabla ya uchaguzi.

Katika uchaguzi huo, mgombea wa Chadema, Diwani wa Daraja Mbili, Prosper Msofe, alichaguliwa kushika nafasi hiyo, baada ya kupata kura 25, kati ya kura 28, huku mbili zikimkataa na moja iliharibika. Kwa ujumla, Chadema ina jumla ya madiwani 15, CCM 14 na mmoja wa TLP.
TLP yenye Diwani mmoja, Michael Kivuyo ambaye awali alitangaza kugombea lakini alipima upepo na kuamua kujitoa kabla ya uchaguzi kufanyika.
Aidha, uchaguzi huo ulikwenda sambamba na uchaguzi wa kamati mbalimbali, ambapo mgombea wa Chadema, Isaya Doita alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya Elimu, Afya na Uchumi, baada ya kupata kura 11, wakati mgombea wa CCM, Paulo Matthysen akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya mipango miji.
Uchaguzi huo umefanyika takribani miaka mitatu, tangu kufanyika uchaguzi ambao ulizua vurugu kubwa katika Jiji la Arusha na baadaye kufukuzwa madiwani watano wa Chadema walioingia mwafaka na CCM.
Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, baada ya uchaguzi huo akizungumza akiwa ofisini kwake, alisema uchaguzi huo umefuata sheria na kanuni za uchaguzi na sio kama ule wa Meya uliompitisha Gaudence Lyimo.
Alisema kwa sasa chama kina Naibu Meya, Mwenyekiti wa kamati muhimu na Mbunge, hivyo wataweza kusukuma mbele maendeleo.
Hata hivyo alisema kuwa baada ya uchaguzi huo Kamati Kuu itakaa na kutoa tamko la hatima ya mwafaka wa kumtambua Meya Lyimo au la, kwani jana wamefanya uchaguzi wa Naibu Meya  bali uchaguzi huo  si muafaka  wa kuendelea kumtambua Meya bali ni uchaguzi  kama chaguzi nyingine na Kamati Kuu itakaa Novemba 20, 21 na 22 kisha watatoa tamko la kumtambua Meya au la.

No comments: