![]() |
| Kabwe Zitto. |
Naibu Mkaguzi Mkuu anayehusika na Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu, Francis Mwakabalila akizungumza na mwandishijana kwa simu, alisema ofisi hiyo ina taarifa ya baadhi ya vyama kufanyiwa ukaguzi ikiwemo TLP na CCM, lakini inapitia faili la chama kimoja baada ya kingine ili kujiridhisha kabla ya kusema au kutoa taarifa yoyote.
"Hapa tunazungumzia ripoti iliyokaguliwa na CAG, tuna baadhi ya vyama vimekaguliwa kama TLP na CCM, ila inahitaji muda kupitia maana tunapaswa kujiridhisha, tunapitia faili moja moja hivyo unipe muda, lakini pia tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari (press release) kuhusu suala hili," alisema Mwakabalila huku akidai lazima apate maelekezo kwa CAG ambaye alisema yupo nchini India kwa matibabu.
Mwakabalila alisema atawasiliana na CAG baada ya gazeti hili kuongea naye jana, ili atoe kibali cha kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ufafanuzi wa suala hilo kabla ya Oktoba 25, Ijumaa ijayo, vyama na ofisi yake itakapokutana mbele ya PAC kwa ufafanuzi zaidi.
Kwa upande wake, Zitto kupitia mitandao ya kijamii jana, alisema kuwa masuala yote ya nani aliwajibika wapi ama alipaswa kufanya nini, yatajulikana hiyo Ijumaa huku akisisitiza kuwa ikiwa vyama vina nyaraka zilizokaguliwa na CAG na waliziwasilisha kwa Msajili, wanapaswa kuwa na vielelezo hivyo mbele ya Kamati.
"Ofisi ya CAG ina mamlaka ya kuhakikisha vyama vinapeleka hesabu zao kwake. Yeye alisema alivitaka vyama vipeleke majina ya wakaguzi wao ili awathibitishe, vyama havikufanya hivyo. Akaishia hapo hapo. Msajili naye anapaswa kupokea ripoti iliyokaguliwa na CAG kutoka kwenye vyama, hajapokea. Nani hakufanya kitu," alisema Zitto akichangia hoja katika mtandao wa kijamii wa Wanamabadiliko.
Zitto aliongeza kuwa, kutokana na hilo, vyama navyo vikachukua fursa hiyo kukaa kimya bila kutekeleza sheria hivyo kabla ya ufafanuzi wake, si CAG wala Msajili wanaoweza kukwepa lawama kuhusu hili huku akisisitiza kuwa, ukweli wa hayo yote utajulikana Ijumaa katika PAC.
Hata hivyo Zitto alisema PAC haitafuti wa kumlaumu bali inataka sheria ifuatwe. "Tupige mstari na mahesabu hayo ya nyuma yakaguliwe na kisha yanayofuata yafuate sheria. Tunataka kumaliza "impunity" (kuepuka adhabu) hii ya kudharau sheria".
Akizungumza kwa simu na mwandishi jana, Zitto aliendelea kusisitizia suala la Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2009 izingatiwe na kueleza kuwa kama kuna chama kina nyaraka za ukaguzi wa hesabu zake, zilizokaguliwa na CAG, wazipeleke kwa Msajili ili kamati izipate badala ya kupiga kelele bila vielelezo sahihi.
"Narudia kusema, kama kuna chama kina nyaraka za hesabu zilizokaguliwa na CAG kama inavyoagiza sheria, wataleta, hakuna mtu anayetafuta ushindi wala manufaa binafsi, hili ni suala la kisheria na tulisimamie hivyo," alisema Zitto akizungumza na gazeti hili jana.
Juzi, Zitto alisema amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi, kuwaandikia barua ya kisheria viongozi wa vyama tisa vinavyopata ruzuku ya serikali ya kuwaita mbele ya PAC Oktoba 25 mwaka huu ili kujieleza kwanini hawajawasilisha ripoti hizo kwa Msajili kwa kipindi cha miaka minne iliyopita na kama waliwasilisha, kutoa nyaraka zao.
Juhudi za kumtafuta Msajili wa Vyama, Jaji Francis Mutungi jana kujua kama ameshaanza kuchukua hatua hiyo na kama ameviandikia vyama barua ya kisheria kuviita mbele ya PAC kama ilivyoelekeza Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge. Awali Mutungi alinukuliwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa ofisi yake inafanyia kazi maelekezo ya PAC.
Jana, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliliambia mwandishi kwa simu kuwa, hakuna siasa katika hilo kama anavyodai Zitto, bali yeye anamuunga mkono Mwenyekiti huyo wa PAC kwa kuwa anasimamia sheria isipokuwa anachokiona ni kamati hiyo kutokuwa na taarifa sahihi.
Kwa upande wao, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Mkurugenzi wa Fedha, Anthony Komu, alisema taarifa za ukaguzi wa fedha za chama hicho kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012 ilishakabidhiwa kwa Msajili wa Vyama Siasa na kupata barua ya uthibitisho yenye kumbukumbu namba CDA.112/123/01a/37 ya Septemba 4 mwaka 2012.

No comments:
Post a Comment