Friday, October 18, 2013

UTATA WATANDA KUJIUA KWA MZAZI MWENZAKE UFOO SARO...

Ufoo Saro akiwa wodini baada ya kufanyiwa upasuaji.
Familia ya marehemu Anthery Mushi, anayedaiwa kujiua kwa kujipiga risasi, imeomba Polisi kutumia busara wakati wa uchunguzi wa kifo hicho, kwa sababu ndugu yao amekutwa na matundu mawili ya risasi, baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi.
Anthery ambaye ni mzazi mweza na mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro, anadaiwa kumuua mama wa Ufoo, Anastazia Saro, na baadae kumjeruhi Ufoo kwa risasi na hatimame kujiua mwenyewe kwa kujipiga risasi.
Akizungumza wakati wa kuuaga mwili wa Anthery jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, msemaji wa familia, Isaya Mushi, alisema wamesikitishwa na msiba huo na hawakutarajia kijana huyo afanye hayo kutokana na upole wake.
Alidai kifo cha Anthery kilisababishwa na ugomvi kati yake na mzazi mwenzake, ambapo baadae walienda kwa mama mzazi wa mzazi mwenzake, ili kupata suluhisho lakini baadae ulichukuliwa uamuzi mgumu na kutokea yaliyotokea.
“Tunaomba Polisi itumie busara wakati wa uchunguzi wa tukio hili kwa sababu Anthery baada ya kufanyiwa uchunguzi, amekutwa na matundu mawili ya risasi, wakati katika hali ya kawaida mtu hawezi kujipiga risasi mara mbili.
 “Marehemu alikutwa na matundu mawili, moja kwenye kidevu na lingine usoni upande wa kushoto...siyo rahisi mtu kujipiga risasi mara mbili... siri anayo mzazi mwenzie aliyebaki hai  ambae kwa sasa bado yupo hospitalini,” alidai.
Alisema Anthery alipenda sana kujiendeleza na alikuwa  muadilifu na mtu wa kupenda kuwasaidia watu na wao familia wamepata pigo na hawakutazamia kilichotokea.
Alishukuru kwa ushirikiano wa ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza kumuaga Anthery, pamoja na ushirikiano walioupata kutoka Umoja wa Mataifa (UN), alikokuwa akifanya kazi Anthery.
Kwa upande wake mdogo wa marehemu, Happy Mushi, alielezea kusikitishwa na taarifa za msiba huo kwa sababu kwa mara ya kwanza aliusikia katika vyombo vya habari na baadae aliwasiliana na ndugu na kuthibitishiwa kuwa ni kweli kaka yake amefariki.
“Niliongea na kaka mwanzoni mwa mwezi huu na aliniambia anafurahi kwamba baada ya kufanya kazi katika mazingira magumu, sasa karibu atarudi Tanzania na tukaendelea kuongea mambo yetu, lakini nilikuja kupata taarifa ya kifo chake kwenye vyombo vya habari.
“Napata mazingira magumu kuamini kwamba kaka alijipiga risasi mara mbili, lakini pia familia inapata wakati mgumu kuamini hilo,” alidai Happy na kuongeza kuwa hakuwahi kuona ugomvi kati ya kaka yake na mzazi mwenzie kwani hata vikao vya ukoo wao, Ufoo amekuwa akishiriki.
Anthery alizaliwa Januari 3, 1973 na alifariki Oktoba 13 mwaka huu na ameacha mtoto mmoja wa kiume, Alvin Mushi.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Ongoma kuanzia   1981 hadi mwaka 1987 na elimu ya sekondari aliipata katika shule ya sekondari huko Zanzibar.
Baadae alisoma uandishi wa habari ambapo mwaka 1994 alijiunga na ITV, na mwaka 2002 alihamia ICTR na baadae alijiunga na  UN akiwa kama mtaalamu wa mambo ya mawasiliano.
Mwili wa Anthery ulisafirishwa jana mchana baada ya mamia ya ndugu jamaa na marafiki kujitokeza kumuaga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, na hatimae msafara kuelekea kijijini kwao Uru Ongoma Timbirini, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo leo mchana ndiyo mwili huo utahifadhiwa katika nyumba yake ya milele.
Wakati huo huo taarifa zilizopatikana hospitalini hapo, zilieleza kuwa Ufoo anaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi, lakini uongozi umezuia asizungumze na waandishi wa habari.

No comments: