![]() |
| Sehemu ya njia ya Reli ya Kati. |
Kwa sasa, Reli ya Kati imechakaa kiasi cha kuifanya ishindwe kuhimili shehena kubwa ya mizigo.
Mbali ya uchakavu wa reli, injini na mabehewa ya reli hiyo kongwe nchini ambayo licha ya kuwa ni tegemeo kubwa la abiria wa mikoa mingi nchini na hata nchi jirani, pia inapaswa kuwa tegemeo kubwa la uchumi wa nchi.
Rais wa CCECC, Yuan Li alimweleza Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa tayari wameanza mazungumzo na Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania na iwapo watakubaliana wako tayari kuja kuijenga reli hiyo. CCECC ndio kampuni iliyojenga Reli ya Tanzania- Zambia (Tazara) baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuiomba serikali ya China kusaidia katika ujenzi wa reli hiyo inayounganisha nchi hizo mbili.
Li alisema kampuni yake haijaondoka Tanzania, kwani kuna miradi mbalimbali ambayo wanaendelea kuijenga hasa ya majengo, lakini akasema angefurahi zaidi kama atapewa mradi huo wa Reli ya Kati ili aje kufanya kazi katika nchi ambayo wamezoea kufanya kazi.
Alisema ujenzi wa reli kwa kiwango ambacho Tanzania inahitaji ndicho ambacho kampuni hiyo inaufanya katika nchi za Ethiopia na Djibouti ambako alisema wameanza kujenga na watakamilisha ujenzi huo ndani ya miaka miwili chini ya mkopo wa Benki ya Exim.
"Hadi Oktoba 2015 tutakuwa tumekamilisha ujenzi katika nchi ya Djibouti na watakuwa na reli ya kisasa, hivyo na ninyi kama mnataka Standard Gauge tuko tayari kuja kufanya kazi hiyo," alisema Li.
Alisema ujenzi wa kiwango hicho kinachotakiwa ni gharama na kwamba hawawezi kufumua reli yote kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma na Mwanza, bali watafanya kwa awamu ili usafirishaji wa mizigo na abiria uweze kuendelea na ujenzi pia ukiendelea.
"Tunaweza kufanya katika awamu ya kwanza tunajenga kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na hatua ya pili hadi Dodoma," alisema Li.
Pinda alisema kampuni kadhaa kutoka mataifa mengine nao wameonesha nia ya kujenga reli hiyo, lakini akasema wameona wawasiliane kwanza na China kutokana na historia ya ushirikiano iliyopo hasa ya ujenzi wa reli ya Tazara.
"Tumeona tulete ombi hili kwenu na nyinyi mtupe gharama zenu tuone kama tutaweza, lakini lengo la ziara hii ni kunadi ujenzi wa reli hii ya kati na tunawakaribisha sana leteni maombi yenu haraka," alisema Pinda.
Alisema ndio maana amefuatana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe katika ziara hiyo ili atafute kampuni za uhakika ambazo zinaweza kuja nchini kufanya ujenzi wa reli hiyo ambayo alisema ndio uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa, kwa sasa reli hiyo imechakaa hali inayofanya mizigo mingi kutoka bandarini kusafirishwa kwa barabara hivyo kuongeza gharama kwa wasafirishaji na kuharibu barabara kutokana na uzito wa magari yanayobeba mizigo. "Nimeelezwa hapa China kuwa kiwango chenu cha mwisho cha kusafirisha mizigo katika barabara ni tani 25, lakini sisi ni tani 56! Na hii ni kutokana na ukosefu wa reli," alisema Pinda.
Reli ya Kati inahudumia mikoa mingi ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Katavi, Shinyanga, Mwanza na Kigoma.
Mbali ya kuitegemea kwa usafiri, wakazi wa maeneo hayo wamekuwa wakinufaika pia kiuchumi kutokana na kufanya shughuli nyingi zinazofanyika wakati treni zinapofanya kazi kwa ufanisi.
Hata hivyo, kutokana na uchakavu wa reli hiyo kiwango cha mizigo ya ndani na nje ya nchi inayosafirishwa kimeporomoka mno, huku siku za safari za treni ya abiria zikishuka kutoka saba, kwa maana usafiri wa kila siku kutoka na kwenda Dar es Salaam na Mwanza na Kigoma, hadi safari mbili tu kwa wiki.

No comments:
Post a Comment