![]() |
| Kamanda Liberatus Sabas. |
Mtuhumiwa wa ujambazi aliyepigwa kichwa ni mwanamke raia wa Tanzania mwenye asili ya Asia aliyetajwa na jeshi la polisi kuwa ni Anita Kaburu (27).
Kaburu na wenzake walikamatwa jijini hapa kwa kile kilichoelezwa kuwa walikuwa wakijiandaa kuiba fedha kwenye duka la M-Pesa maeneo ya Shamsi.
Polisi wamesema kwamba mwanamke huyo na wenzake wanne, wakiwemo walinzi wa KK Security, walikutwa na bunduki aina ya shotgun, bastola aina ya Beretta pamoja na risasi sita za bastola.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliyesema watuhumiwa hao wa ujambazi walikamatwa juzi saa sita mchana maeneo ya Shamsi.
Mbali ya Kaburu, aliwataja wengine kuwa ni Abdulrahman Idd (27) ambaye ni Mwangalizi wa Kampuni ya Ulinzi ya KK Security mkazi wa Shamsi, Anita Kaburu (27), Simon Martin maarufu kwa jina la Mapanki (45), Hashim Ally (30), Charles Luangano (24) ambaye ni mlinzi wa Kampuni ya KK Security.
Alisema Stella Lema (26) ambaye ni mkazi wa Majengo Chini, akiwa dukani kwake ghafla walifika watu wawili mwanamke na mwanaume na kujifanya kuhitaji huduma ya M-Pesa.
Alisema kabla hawajapatiwa huduma hiyo, ghafla Kaburu alitoa bastola kwenye mkoba wake na mwanaume naye alitoa bunduki na kuwaamuru Lema na mteja wake watoe fedha na simu na hapo ndipo mteja mwanaume aliyekuwa na Lema dukani alifanikiwa kumpiga kichwani Kaburu na kupiga kelele za kuomba msaada.
Hapo ndipo walifanikiwa kumdhibiti Kaburu ambaye alikuwa na bastola huku wenzake walifanikiwa kutoroka na hapo ndipo polisi walipofika na kumkamata Kaburu ambaye alitoa ushirikiano kwa kuwataja walipo wenzake.
Alisema polisi walifanya upekuzi kwenye nyumba zao ikiwemo ya mtuhumiwa Iddi ambaye ni mpangaji katika nyumba inayomilikiwa na Isaya Pinga (47) ambaye ni Mchimbaji wa madini na kufanikiwa kupata silaha aina ya shotgun yenye namba 7352605787 CAL .458 WIN aina ya Brno ZKK-602 iliyokuwa imekatwa mtutu wake na kitako cha bunduki, risasi sita za bastola na radio call aina ya HYT-TC 610 pamoja na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
"Tumefanikiwa kukamata watuhumiwa hawa na Jumatatu tutawafikisha mahakamani maana walikuwa wanajiandaa kuiba lakini hawakufanikiwa idadi ya fedha haijajulikana," alisema.
Pia polisi inawashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa na kusaidia kupatikana kwa silaha ambayo ilikuwa imetelekezwa kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Shauri Moyo chumba namba tatu maeneo ya Olmatejoo.
Alisema silaha hiyo iliyokuwa imekatwa kitako ikiwa na risasi moja ilipatikana baada ya mtu mmoja kwenda katika nyumba hiyo na kuhitaji chumba cha kulala akiwa na begi jeusi na alipopewa chumba na mhudumu wa nyumba hiyo ambaye hakutajwa alilipia chumba hicho kiasi cha Sh, 8,000 huku akiambiwa kuwa utaratibu wa mteja kulala hapo ni lazima akaguliwe.
Alisema baada ya kuambiwa hivyo mtu huyo aliamua kutoka nje na kuacha mzigo huo ndani na hapo ndipo wahudumu wa nyumba hiyo walipofanya ukaguzi na kugundua kuwa ilikuwa silaha kisha kutoa taarifa polisi ambao walifika kuichukua.

No comments:
Post a Comment