![]() |
| Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani katika moja ya mikutano ya pamoja. Kutoka kulia ni James Mbatia (NCCR), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema). |
Mkutano huo ndio utakaomaliza sintofahamu kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesabu za vyama hivyo za miaka minne iliyopita, ambazo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto, alisema hakuna chama chochote kilichowasilisha ripoti hizo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kama vinavyopaswa kufanya kisheria.
Wakati Zitto akisisitiza kuwa hakuna chama kilichotekeleza wajibu huo wa kisheria, na kutishia kuvinyima ruzuku ya mwezi huu kama havitafanya hivyo, vyama hivyo kila kimoja kiliitisha mkutano na vyombo vya habari na kujinasibu kwamba vilishatekeleza wajibu huo.
Kutokana na mvutano huo wa maneno kati ya Zitto na wasemaji wa vyama hivyo, Mwenyekiti huyo wa PAC alimuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuwaandikia barua ya kisheria viongozi wa vyama tisa vinavyopata ruzuku ya Serikali, ya kuwaita mbele ya kamati hiyo kesho kutwa kujieleza kwa nini hawajawasilisha ripoti hizo kwa Msajili kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
Kwa mujibu wa Zitto katika miaka hiyo minne, vyama vilivyopokea ruzuku kutoka serikalini ni pamoja na CCM iliyopokea Sh bilioni 50.9, Chadema Sh bilioni 9.2, CUF bilioni 6.3, NCCR-Mageuzi Sh milioni 677, TLP Sh milioni 217, UDP Sh milioni 333, DP Sh milioni 3.3, APPT-Maendeleo Sh milioni 11 na Chausta Sh milioni 2.4.
Mpaka juzi vyombo vya habari vilikariri wasemaji wa vyama hivyo wakidai hawajapata mwaliko wa aina yoyote huku wakisisitiza kwamba bila kupata barua hiyo, hawatahudhuria.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, yeye alikaririwa akisema amepata mwaliko wa kukutana na Msajili kesho, lakini kwa masuala tofauti kabisa yasiyohusu PAC.
Jana Ofisa Uhusiano wa chama hicho, Tumaini Makene, alisema wamekuwa wakisikia habari za kuwepo kwa kikao hicho cha vyama vya siasa, Msajili na PAC kupitia vyombo vya habari.
"Habari hizi tunaziona kwenye mitandao tu na magazeti, mpaka sasa hatujapata barua yoyote ya kuitwa na Msajili, na iwapo hatutapata barua hiyo, hatutohudhuria mkutano huo," alisema Makene.
Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Samuel Ruhuza alikaririwa juzi akisema hajapata mwaliko huo lakini akasisitiza akipata, atahudhuria mwaliko huo.
Hata hivyo Msemaji wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya, alithibitisha jana kupokea barua ya mwito huo tangu juzi na hivyo kujiandaa kuhudhuria mkutano huo.
Sheria ya Vyama vya Siasa ya 2009 inaweka wazi kuwa ni wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua hesabu za vyama vya siasa na kuwasilisha ripoti yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye naye anatakiwa atoe ripoti hizo kwenye gazeti la Serikali kila mwaka.
Kutokana na CAG kutokuwa na fungu la fedha la kufanya ukaguzi huo, aliagiza vyama hivyo kuteua kampuni ya kufanya ukaguzi na kuipeleka kwake kwa uthibitisho.
Hata hivyo kwa mujibu wa Zitto, ni CCM na TLP tu vilivyoteua kampuni za kufanya ukaguzi huo na kupeleka kwa CAG kwa ajili ya uthibitisho, ingawa hata baada ya kuteua kampuni hizo, havikupeleka ripoti kama vilivyopaswa kufanya kisheria.
Lakini Katibu wa Baraza la Wadhamini la Chadema ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha wa chama hicho, Antony Komu alisema taarifa za ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012 ilishakabidhiwa huku akionesha barua aliyodai ni ya Msajili wa Vyama vya Siasa yenye kumbukumbu CDA.112/123/01a/37 ya Septemba 4 mwaka 2012 kama uthibitisho.
Naye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Jumapili iliyopita alisema chama hicho kiko tayari kwenda mbele ya PAC na hesabu zilizokaguliwa na wakaguzi wa nje, Shirika la Ukaguzi la Taifa (TAC).
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema mahesabu yao yako safi, ila wameshindwa kukaguliwa na mkaguzi wa nje kwa kuwa Serikali haijatoa fedha za kufanya ukaguzi huo.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza, alisema chama hicho kiko tayari kuwasilisha hesabu zake, ila walishindwa kuwasilisha baada ya kuelezwa kuwa CAG, ndiye aliyepaswa kukagua.

No comments:
Post a Comment