![]() |
| Bunge la Jamhuri ya Muungano. |
Akizungumza jana baada ya kamati hiyo kukutana na Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alisema kufanya hivyo kutasaidia kuiboresha TTCL.
Alisema katika ubia huo, Serikali kupitia TTCL inamiliki hisa asilimia 65 jambo ambalo linafanya kampuni hiyo kushindwa kukopesheka na kudhaminiwa.
Serukamba pia ameipa miezi mitatu TTCL kuhakikisha inakusanya deni la zaidi ya Sh bilioni 10 inayoidai Serikali na taasisi zake.
"Deni hili la Serikali linaifanya TTCL kuendelea kupoteza fedha. Huwezi kuendelea kutoa huduma wakati mteja halipi. Kuanzia leo (jana) fuatilieni hili ili mpaka Desemba muwe mmekusanya madeni yenu na kuleta mrejesho kwa kamati," alisema.
Baadhi ya taasisi zinazodaiwa na TTCL na kiasi cha fedha kwenye mabano ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) (Sh milioni 775.9), Jeshi la Polisi (Sh bilioni 1.2), Shirika Hodhi la Mali za Umma (Sh milioni 273), Wizara ya Fedha (Sh milioni 231.1) na Ofisi ya Rais (Sh milioni 180).
Wadaiwa wengine ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) (Sh milioni 201.1), Wizara Mambo ya Ndani (Sh milioni 99.4), Ofisi ya Makamu wa Rais (Sh milioni 94), Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma (Sh milioni 82), Wizara ya Elimu (Sh milioni 71), Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam-DIT (Sh milioni 63) na Chuo Kikuu Dodoma (Sh milioni 58).
Taasisi zingine ni Wizara ya Ulinzi (Sh milioni 49.4), Wizara ya Katiba na Sheria (Sh milioni 69), Wizara ya Mawasiliano (Sh milioni 28), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Sh milioni 24.4) na dola za Marekani milioni 3.1 ambazo TTCL inazidai ofisi za Serikali kama malimbikizo ya madeni.
Serukamba alisema pia kunahaja ya Serikali kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili TTCL iingizwe kwenye mfumo wa mawasiliano ya kisasa wa GSM ili kampuni iingie katika ushindani wa biashara.

No comments:
Post a Comment