![]() |
| Rais Uhuru Kenyatta (kulia) na William Ruto. |
Hatua hiyo inatokana na Azimio la Umoja wa Afrika (AU), kwamba hakuna kiongozi wa nchi yoyote barani Afrika atakayepelekwa ICC akiwa madarakani.
Azimio hilo ni sehemu ya maazimio ya viongozi wakuu wa Afrika yaliyofikiwa wakati wa kikao cha dharura kilichofanyika kwa siku nzima juzi mjini Addis Ababa Ethiopia, kujadili uhusiano uliopo kati ya AU na ICC.
Viongozi hao wamejiridhisha pasipo shaka kwamba ICC inafanya kazi zake kwa kuwaandama viongozi wa Afrika zaidi, kuliko wa mataifa mengine, hata pale panapokuwa na ushahidi kwao kufanya makosa ya jinai ya wazi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alisema Dar es Salaam jana kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya mjadala wa kina uliowahusisha marais wote wa Afrika, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, mawaziri wakuu watendaji wote na Mfalme Mswati wa Swaziland.
Ili kudhihirisha kuwa viongozi wa Afrika hawana mzaha katika suala hilo, Membe alisema tayari AU imemuandikia barua Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambaye ndiye mlezi wa ICC, ikimueleza msimamo wao huo na ametakiwa kujibu barua hiyo ifikapo Novemba 10, mwaka huu.
Pamoja na azimio hilo la kuzuia viongozi wa Afrika walio madarakani kwenda ICC au katika Mahakama yoyote wakiwa madarakani, AU pia imezuia kiongozi yoyote ambaye Katiba ya nchi yake inampa uwezo wa kukaimu nafasi ya Rais, kushitakiwa katika Mahakama hiyo.
Hata hivyo AU imesema kwa viongozi wakuu wa Afrika wanaofanya makosa yanayoshitakika, wanaweza kufikishwa kwenye Mahakama zozote zile, baada ya kumaliza kutumikia vipindi vyao vya uongozi.
"Viongozi wa Afrika wameeleza kusikitishwa kwao na namna ICC inavyofanya kazi yake kwa kuwaandama viongozi wa Bara la Afrika zaidi kuliko wa mataifa mengine hata panapokuwa na ushahidi wa viongozi hao kufanya makosa.
"Mahakama hiyo kwa mfano, imekuwa na kesi takribani 30 tangu mwaka 2004 hadi sasa na katika hizo, kesi 27 ni za kutoka nchi mbalimbali barani Afrika," alisema Waziri Membe.
Kuhusu pendekezo la kujitoa kutoka kwenye uanachama wa Mahakama hiyo, Waziri Membe alisema AU imesema ni mapema mno kuchukua hatua hiyo na kwa vyovyote vile hatua hiyo inapaswa kuchukuliwa na wanachama husika kwa kufuata utaratibu wa nchi husika.
"Nchi 34 za Afrika ambazo ni wanachama wa ICC zitakuwa na mkutano wa wanachama wote utakaofanyika Uholanzi Novemba 29, mwaka huu ambapo mawaziri wa Mambo ya Nje na mawaziri wa Sheria watakutana kujadili hatma yao," alisema Membe.
Alisema kwa kuwa taasisi mlezi wa ICC ni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kwa kuwa baraza hilo lina uwezo wa kuahirisha kesi za Mahakama hiyo, AU imeandika barua iliyotiwa saini na nchi zote za Afrika kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuomba kuahirishwa kesi inayowakabili Rais Uhuru na Naibu wake Rutto mpaka watakapomaliza uongozi wao Kenya.
"Watanzania wenzangu mtakumbuka kuwa viongozi hawa wa juu wa Serikali ya Kenya wanakabiliwa na kesi ya jinai kwenye Mahakama hiyo kabla na baada ya kuingia madarakani Aprili 2013.
"Safari za nenda rudi kati ya Nairobi na The Hague, zimesababisha usumbufu mkubwa katika uongozi nchini Kenya. Mtakumbuka pia kwamba mapema Septemba, 2013, nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania kwa pamoja ziliiomba ICC ikubali ombi la Kenya la kutaka kesi hiyo iwe inahudhuriwa na mawakili wao badala ya wao wenyewe, ombi hilo lilikataliwa.
"Aidha Novemba 12, mwaka huu, Rais Kenyatta kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ICC atatakiwa kuondoka nchini Kenya kwenda The Hague, kwa muda usiopungua wiki nne kuisikiliza kesi hiyo na kuna uwezekano mkubwa wa viongozi wote wawili kujikuta wapo Uholanzi na hivyo kusababisha ombwe la uongozi nchini humo," alisema Membe.
Kuhusu msimamo wa Tanzania kuhusiana na ICC kwa kuzingatia mjadala huo wa viongozi wa Afrika, Membe alisema kwa vile wakati wa kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Rome uliozaa ICC, mchakato wake ulianzia bungeni, ni lazima suala hilo likarejeshwa bungeni kabla ya nchi kutoa uamuzi wake.
"Kwa vile ni suala lililoanzia bungeni ni lazima lirejeshwe tena bungeni, ili wananchi kupitia kwa wawakilishi wao bungeni watoe uamuzi kama wanaona kuna sababu ya Tanzania kuendelea kuwa mwanachama wa ICC au la," alisema Membe.

No comments:
Post a Comment