Monday, October 14, 2013

HIVI NDIVYO MWANDISHI WA ITV ALIVYONUSURIKA SHAMBULIO LA RISASI...

KUSHOTO: Ufoo Saro. KULIA: Nyumba yalikotokea mauaji hayo.
Mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro, aliyejeruhiwa kwa risasi jana asubuhi, alilazimika kuvumilia majeraha ili kujiokoa yeye mwenyewe na wadogo zake watatu waliokuwa wakipigwa risasi, baada ya mama yake mzazi, Anastazia Saro (58), kuuawa.

Mauaji hayo ya kusikitisha, yalifanyika katika eneo la Mbezi Kibwerere, nyumbani kwa mama yake Ufoo, ambako alikuwa akiishi na wadogo zake Ufoo ambao ni Goodluck, Innocent na Jonas.
Mtuhumiwa wa unyama huo ametajwa kuwa ni Anthery Mushi, ambaye ni baba mtoto wa Ufoo na siku ya tukio wawili hao walitokea Mbezi Magari Saba nyumbani kwa Ufoo, kwenda kuzungumza kifamilia na mama mzazi wa mwandishi huyo.
Mushi (40) ni Mhandisi wa Kitengo cha Mawasiliano katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan na aliwasili nchini juzi na  kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Ufoo eneo la Mbezi Magari Saba.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, Ufoo amejeruhiwa katika paja na tumboni, mama yake mzazi alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi ya kifuani na mtuhumiwa Mushi ambaye naye alijiua baada ya kujipiga risasi kichwani katika eneo la kidevuni.
Akizungumza na mwandishi jana mdogo wake Ufoo, Goodluck alisema: "Walikuja wakiwa pamoja (Ufoo na Mushi) mapema alfajiri wakiwa ndani ya gari ya Ufoo, saa 12 na kabla ya kuingia ndani, alitusalimia kisha wakaingia sebuleni na kuanza  mazungumzo na mama." 
Goodluck alidai baada ya muda, walisikia milio ya risasi iliyokuwa ikiambatana na sauti ya mama yao akisema "jamani nakufaa," na walipotaka kufungua mlango ili kujua kulikoni, mlio wa risasi uliendelea kusikika kutoka sebuleni. "Pengine muda huo Ufoo ndio alikuwa akifyatuliwa risasi," alisimulia.
"Tulipotaka kujua kulikoni, tulimuona dada (Ufoo ) akijiburuza chini kuja katika mlango wa chumba tulichokuwa tumelala akatuambia jifungieni mlango atatua wote huyu."
"Tulifunga mlango lakini zilipigwa risasi mbili mlangoni huku Mushi akisema tokeni nje niwamalize. Tulitafuta namna ya kujiokoa na kuamua kupanda juu ya dari la nyumba," alisimulia Goodluck.
Kwa mujibu wa madai ya Goodluck, walipanda darini kujiokoa kwa kuwa Mushi alifungua mtungi wa gesi na kusababisha hewa kuwa nzito na nahisi alilenga kulipua nyumba ili kututeketeza wote.
"Tulipoanza kupanda juu, alianza kufyatua risani kupitia dirishani lakini wakati huu akiwa nje ya nyumba, tunamshukuru Mungu kwani muda huo wote tayari tulikuwa juu kwenye dari tukijaribu kutoka nje ya nyumba na tulipofanikiwa kutoka, tulikimbilia kwa majirani kutoa taarifa," alisema.
Hata hivyo alisema majirani hao walikuja lakini hakuna hata mmoja aliyejaribu kuisogelea nyumba hiyo, wakihofia  kushambuliwa kwa risasi hadi walipofika polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Mbezi Mwisho na kuingia ndani ya nyumba hiyo.
Goodluck alisema wakiongozana na askari Polisi, waliingia ndani na kumkuta muuaji akiwa amekaa katika moja ya sofa akiwa tayari ameshakufa huku mwili wa mama yao ukiwa sakafuni.
Alisema walijaribu kuangalia ndani kumtafuta dada yao bila mafanikio, ndipo walipotoka nje na kukutana na mmoja wa waendesha pikipiki aliyewaeleza kuwa amemuona dada mmoja akiwa ametapakaa damu akiomba kupelekwa Hospitali ya Tumbi.
"Polisi waliingia ndani na kuchukua bastola iliyotumika kwa mauaji pamoja na kuokota maganda ya risasi na walipopekua mfuko aliokuja nao Mushi, ndani yake walikuta kuna pingu, shoka lenye mpini mfupi pamoja na kamba. Hata hivyo hatukujua alivibeba vitu hivyo kwa sababu gani," alisema Goodluck.
Alisema baadaye Polisi waliichukua miili ya marehemu wote wawili na kuondoka nayo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ufoo alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa  Muhimbili  jana akitokea Tumbi Kibaha, na  alifanyiwa upasuaji na juhudi nyingine zilikuwa zikiendelea  kuokoa maisha yake.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka Muhimbili, zilieleza kuwa  Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi aliruhusiwa kumuona Ufoo ambapo alisema anazungumza na hali yake inaendelea kuimarika.
Aidha askari Polisi wamegawanyika katika timu tatu, moja Muhimbili, ya pili Kibamba na ya tatu mtaani kutafuta taarifa muhimu za mauaji.

No comments: