Wednesday, October 16, 2013

ULINZI WAIMARISHWA, DISKO TOTO MARUFUKU IDD EL HAJI...

Kamanda Suleiman Kova.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam itaimarisha ulinzi wakati wa Sikukuu ya Idd el Haji, ambayo inafanyika leo.

Pia, polisi wamepiga marufuku disko toto katika kumbi mbalimbali jijini humo.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi Suleiman Kova alisema watashirikiana na wananchi pamoja na wadau mbalimbali katika kupambana na kuzuia uhalifu, utakaoweza kujitokeza, ambapo hatua za haraka zitachukuliwa ili kuweza kukamata watuhumiwa.
“Pamoja na jitihada hizo polisi inatoa wito kwa wadau na wananchi kuwa macho katika kipindi hicho na kujiepusha na vitendo vya uvunjaji wa amani, ikiwa ni pamoja na kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha kuwa na hasira kali au uonevu,” alisema.
Aidha, Kova aliwataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani na wasipakie watu wengi kinyume cha taratibu katika vyombo vya usafiri.
“Magari yaendeshwe na watu wenye leseni na magari yawe na bima   na yawe na kumbukumbu zote kama leseni ya matumizi barabarani na pia madereva waepuke kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, kuongea na simu za mkononi au kusoma magazeti,” alisema.
Pia, alitoa tahadhari katika maeneo ya fukwe watoto kuzagaa bila ya uangalizi wa wazazi au walezi wao ambapo pia alisema polisi watakuwa doria maeneo mbalimbali ili kuhakikisha vitendo vyote vinavyoweza kuleta madhara au kutokea kwa uhalifu vinazuiliwa mapema.
“Tutaimarisha misako na doria saa 24 pamoja na ukamataji wa wahalifu sugu kutokana na taarifa za kiintelijensia zitakazotufikia kutoka kwa wananchi au taasisi mbalimbali na kuwataka wananchi wenye taarifa za uhalifu kutoa taarifa kupitia Namba 111 na 112,” alisema.

No comments: