![]() |
| Bendera za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. |
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo, ambayo ni Uganda, ametakiwa kutoa taarifa ya kina kuhusu majadiliano hayo na athari zake ambayo yalihusisha Kenya, Rwanda na Uganda.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Wizara ya Afrika Mashariki, Vedastina Justinian, alisema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mikutano ya utatu iliyoshirikisha nchi hizo za Kenya, Uganda na Rwanda.
“Hivi karibuni wananchi wengi wamekuwa wakitaka taarifa juu ya hatua ya baadhi ya nchi wanachama kufanya mikutano ya utatu kujadili masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pasipo kushirikisha nchi za Tanzania na Burundi,” alisema Vedastina na kuongeza kuwa dalili hizo zinaonesha kutengwa kwa Tanzania.
Alisema mikutano hiyo iliyozikutanisha nchi hizo tatu iliandaliwa kupitia wizara za mambo ya nje za nchi hizo badala ya kupitia mfumo wa sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Vedastina alisema katika mkutano uliofanywa na nchi hizo tatu Juni 25, 2013, Entebbe nchini Uganda, masuala yaliyojadiliwa na kutolewa uamuzi na mwongozo wa utekelezaji ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa-Kampala-Kigali yenye urefu wa Kilometa 2,784.
Alitaja masuala mengine kuwa ni ujenzi wa bomba la mafuta la South Sudan-Kampala-Kenya, ujenzi wa mitambo ya kusafisha mafuta Uganda, kuongeza upatikanaji wa umeme na kuanzisha himaya moja ya forodha.
Pia walijadili kuharakisha shirikisho la kisiasa, vitambulisho vya kitaifa kutumika kama hati ya kusafiria na hati ya kuishi katika nchi hizo ya pamoja kwa ajili ya utalii.
Hata hivyo, alisema pamoja na kuwa na Ibara ya 7(1) (e)ya mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inaruhusu nchi wanachama kuwa na ubia, ni lazima suala linaloenda kutekelezwa nchini ya mfumo huo, liwe limejadiliwa na kukubalika na nchi zote wanachama.

1 comment:
tatizo Nchi yetu ya Tanzania "uswahili ni mwingi mno kuliko matendo". Wenzetu wameliona hilo na kuamua kutuweka pembeni. Wao wanataka maendeleo na si longolongo.
Post a Comment