![]() |
| Wafuasi wa Shekhe Ponda wakiwa katika Mahakama ya Kisutu. |
Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Salvatory Bongole, alisema adhabu ya kosa hilo haikuwa sahihi kulingana kifungu cha sheria kinachohusu kosa la kula njama.
Wafuasi hao walihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Machi 21, mwaka huu baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walifungwa kutokana na kukutwa na hatia ya kula njama ya kutenda kosa, kukaidi amri ya Polisi kabla na baada ya kufanya maandamano yaliyozuiwa, kufanya mikusanyiko na kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi.
"Kwa kosa la pili, baada ya kupitia ushahidi na vifungu vya sheria, nimeona upande wa Jamhuri ulithibitisha na kuonesha mliandamana huku mkikaidi agizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa la kuwataka kutoandamana. Kwa maana hiyo kosa la kuandamana bila kibali mna hatia," alisema Jaji Bongole.
Aidha alisema katika kosa la tatu ambalo ni kufanya mikusanyiko na kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi, anakubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kuwatia hatiani.
Akizungumzia juu ya adhabu iliyotolewa, Jaji Bongole alisema awali Wakili wa washitakiwa, Mohammed Tibanyendera, alidai baada ya Mahakama ya Kisutu kuwatia hatiani, ilipaswa kuzingatia sheria ili kufikia adhabu inayostahili.
“Nimepitia mwenendo wa kesi kwa makini na ninakubaliana na Tibanyendera kuwa utetezi wa kupunguziwa adhabu, haukutiliwa maanani na Kifungu sahihi Namba 46 cha mwongozo wa Jeshi la Polisi hakikufuatwa.
"Ninachokiona mimi kutiwa kwenu hatiani kwa kosa la kwanza si sahihi, hivyo adhabu ya mwaka mmoja jela naifutilia mbali, kwa upande wa kosa la pili na la tatu nakubaliana na nyinyi kutiwa hatiani, lakini adhabu ninaibadilisha," alisema.
Alifafanua kwamba anaibadilisha adhabu hiyo kutoka kifungo cha mwaka mmoja jela, na kuwa kifungo cha miezi mitatu jela.
Kwa mujibu wa sheria makosa hayo adhabu yake ni kifungo cha miezi mitatu jela au kulipa faini ya Sh 50,000 na sio mwaka mmoja jela kama walivyohukumiwa.
"Mlifungwa Machi 21, mwaka huu na leo ni Oktoba 21 ni zaidi ya miezi mitatu, hivyo natamka waachiwe wote kutoka gerezani kwa sababu adhabu wameshaitumikia na zaidi," alisema Jaji Bongole.
Nje ya Mahakama baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki walionekana kuwa na furaha huku wakimshukuru Mungu kwa kile kilichotokea mahakamani.

No comments:
Post a Comment