Sunday, October 13, 2013

POLISI YAMSAKA TAPELI WA MAGARI MADOGO...

Kamanda Engelbert Kiondo.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamsaka ‘tapeli’ wa magari madogo ambaye amekuwa akiwaibia magari mazuri watu mbalimbali kwa ulaghai, akiwatelekezea gari la wizi lenye thamani ndogo.

Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Juma Athuman, amekuwa akijitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, ACP Engelbert Kiondo, mbinu zinazotumiwa na mtu huyo ni kupeleka gari bovu katika gereji fulani na kuomba gari jingine la kutembelea hata kwa kukodisha wakati gari lake likifanyiwa matengenezo.
Alisema mara baada ya kupatiwa gari, huondoka nalo moja kwa moja na kutelekeza gari lake linalotengenezwa ambalo nalo kwa wakati huo linakuwa ni la wizi.
Kamanda Kiondo amesema mara nyingi mtu anayetapeliwa hataweza kufahamu hadi gari aliloliacha katika gereji husika litakapokamatwa na Polisi baada ya kuibwa katika mazingira kama hayo katika maeneo mengine.
Kamanda Kiondo alisema kwa mara ya kwanza alitelekeza gari aina ya Daihatsu lenye namba za usajili T 856 BTM katika gereji moja iliyopo eneo la nyumba za Bandari Barabara ya Kilwa, Kurasini na kupatiwa gari jingine, Toyota Corolla lenye namba za usajili T 209 ATP.
Alisema wakati akiendelea kutafutwa kwa utapeli huo mtuhumiwa alikwenda katika gereji nyingine iliyopo eneo la Mwenge na kwenda kutelekeza gari la awali, huko akachukua gari jingine aina ya Toyota Sprinter kwa mtindo huo huo na kuondoka nayo.
Alisema baadaye mtuhumiwa huyo alikwenda katika gereji moja iliyopo eneo la Ilala na kulitelekeza gari hiyo na kuchukua gari nyingine ndogo aina ya Toyota Vitz lenye namba za usajili T 946  BLW ambalo mpaka sasa linatafutwa.
Kamanda Kiondo aliongeza kuwa, mtuhumiwa huyo amekuwa akitumia simu yenye namba 0656 654167 iliyosajiliwa kwa jina la Juma Athuman, kwa sasa kila ikipigwa inakuwa imezimwa.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Kiondo amewataka wananchi wakiwemo wamiliki wa gereji na maeneo ya kulaza magari kuwa macho na mtu huyo na kutoa taarifa Polisi kama watabaini gari lililoegeshwa kwa muda mrefu katika maeneo yao ili lifanyiwe uchunguzi na kutoa wito pia kwa mtu mwenye vielelezo vya gari T.856 BTM aina ya Daihatsu kufika kituo cha Polisi barabara ya Kilwa kuitambua.
Naye mmoja ya watu waliotapeliwa magari yao kwa mtindo huo jijini Dar es Salaam  John Isack, akielezea jinsi alivyotapeliwa gari yake T 946 BLW Vitz rangi ya bluu alisema siku ya tukio, tapeli huyo alifika kwake eneo la Tabata Kimanga kutaka gari la kukodi, lakini baada ya kumwambia linauzwa alilichukua kwa lengo la kulijaribu na kumuachia gari jingine ambalo ni la wizi na kutoweka nalo moja kwa moja.
John amesema baada ya kuona siku nyingi zimepita huku akijaribu kumpigia simu lakini hapatikani aliamua kulipeleka gari hilo kituo cha Polisi Pangani, Ilala ambako Polisi walibaini kuwa gari hilo pia lilikuwa ni la wizi. Hata hivyo, baadaye gari hiyo ilipata mwenyewe.
Hadi sasa mtu huyo amebainika kutapeli magari manne na kufunguliwa kesi katika vituo vya Polisi Barabara ya Kilwa mkoa wa Temeke, Kijitonyama mkoa wa Kinondoni na Kituo cha Pangani mkoa wa Ilala vyote katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

No comments: