Saturday, October 12, 2013

OPERESHENI KIMBUNGA YASOMBA WAHAMIAJI ZAIDI...

Kamanda Simon Sirro.
Awamu ya pili ya Operesheni Kimbunga ya kuondoa wahamiaji haramu iliyodumu kwa takribani mwezi mmoja, imewakamata watu 1,237 huku ng’ombe 156 wakitaifishwa kwa amri ya mahakama na faini ya Sh milioni 12.9 ikitozwa kwa ajili ya ng’ombe.

Hayo yalielezwa jana na Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambapo alisema operesheni hiyo ilihusisha mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera.
Kamanda Sirro alisema watu 907 walirudishwa nchini kwao chini ya uangalizi (PI) huku 173 walirudishwa kwa hiari yao na wengine 141 waliachiwa huru kwa mujibu wa taarifa za Uhamiaji baada ya kuonekana kuwa ni Watanzania.
Alisema katika operesheni hiyo kwenye  mikoa ya Geita na Kigoma idadi wahamiaji haramu imeendelea kupungua, licha ya kufanikiwa kukamata majambazi 329 wenye  silaha 329.
Alisema majambazi hayo yalikiri na silaha zao kukamatwa, ikiwa ni pamoja na silaha nyingine 30 zilikamatwa zikiwemo SMG saba, shotgun 1, pistol 2, pamoja na magobori 20 huku risasi 687 zilikamatwa zilizokuwa zikitumika katika uharifu katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo.
“Idadi imepungua hasa  katika mikoa ya Geita, Kigoma na operesheni inaendelea vizuri kuhakikisha inafanikiwa na kuwafanya watu wetu waishi kwa amani kama mababu zetu walivyotuacha,”  alisema Kamanda Siro.
Sambamba na hayo, ng’ombe 6,559 walikamatwa kwenye hifadhi huku ng’ombe 156 wakitaifishwa kwa amri ya mahakama na faini yake Sh milioni 12.9.
Hata hivyo, Kamanda Sirro amewaomba watanzania kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao  na kuwataka majambazi wote kumrudia Mungu wao kwani hirizi na waganga wa kienyeji hawawezi kusaidia chochote  isipokuwa ni wao kuachana na vitendo hivyo.

No comments: